Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amekitaka Chuo cha Ualimu Butimba
kilichopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza kufanya tafakari ya namna gani kinakuwa
chachu ya mabadiliko katika kuandaa walimu wanaoendana na mahitaji ya sasa.
Naibu Waziri Ole Nasha
ameyasema hayo Jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 80 ya
kuanzishwa Chuo hicho ambapo amesema mijadala itakayoendeshwa ijikite zaidi
katika kujua ni namna gani wanabadili mfumo wa kufundisha ili wanafunzi waweze
kuwa wabunifu na wanaojiamini.
“Nimeona katika maonesho
yenu mna jaribu kufanya masuala ya ubunifu, ubunifu unaanza mwanafunzi akiwa
mdogo na ndio maana tunasema lazima kufanya ufundishaji ambao toka mwanzo
unampa mwanafunzi nafasi ya kuwa mbunifu. Usimbane mwanafunzi jaribu
kumfungulia fursa mbalimbali kwani anapozaliwa anakulia katika mazingira
mbalimbali ya ubunifu hapo utatoa nafasi ya kuweza kuendeleza ubunifu alio nao,”
alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akizungumza katika Kumbukizi ya Miaka
80 ya Chuo cha Ualimu Butimba iliyofanyika katika chuoni hicho
Jijini Mwanza.
Alisema Chuo cha Butimba pamoja na kwamba ni
chuo cha ualimu historia yake hasa iko katika ualimu ule wa Sanaa za maonesho,
Sanaa za ufundi ni vizuri kuangalia ni namna gani Chuo hicho kinarudi katika
msatri na kuendelea kutoa walimu ambao watasaidia katika kufundisha masomo
hayo.
“Kwa bahati mbaya kuna
mahali tulikosea kufikiri kwamba music, ufundi, Sanaa za maonesho hazina nafasi
katika elimu, sio vibaya tukarekebisha sababu kama unataka kumfundisha
mwanafunzi ubunifu huwezi kukwepa kutumia Sanaa za maonesho, music na tamaduni
zake zote kwani zinamsaidia kuwa mwanafunzi kamilifu anaeweza kubuni,”
aliongeza Naibua Waziri Ole Nasha.
Washiriki wakifuatilia
hotuba ya Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati
wa kuadhimisha kumbukizi ya miaka 80 ya Chuo cha Ualimu Butimba kilichopo
Wilaya ya Nayamagana Jijini Mwanza
Akizungumzia Jitihada
zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira ya kufundishia na
kujifunzia Ole Nasha amesema Serikali ya Awamu ya Tano imeweka historia ya
kufanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya elimu kwa kujenga, kukarabati na
kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwenye shule.
Aliongeza kuwa pamoja na
mambo mengine Serikali kuanzia mwaka 2016 inatekeleza Mpango wa Elimu bila
malipo, mpango ambao haujawahi kuwepo ni mara ya kwanza katika historia ya nchi
yetu ambapo inatumia zaidi ya shilingi bil. 20 kila mwezi kugharamia elimu bila
malipo.
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Butimba
ya namna wanavyotumia vifaa
vinavyopatikana katika mazingira wanayoishi kufundishia.
Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu
Butimba Huruma Mageni amesema katika kuadhimisha miaka 80 ya Chuo hicho
kinajivunia mambo mengi ikiwemo eneo la chuo kupimwa na kwamba rasimu ya hati
ya chuo iko tayari. Pia inajivunia kuwa na vitengo ambavyo vinachangia
kuboresha elimu nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.