Serikali imesema inatambua
changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye mahitaji maalum na ndio maana
inachukua juhudi za makusudi kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia
ili yawe rafiki kwao kupata elimu.
Kauli hiyo ya Serikali
imetolewa jijini Mwanza na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William
Ole Nasha wakati akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi walio katika
Kambi ya Joto (Summer Camp) inayoratibiwa na Taasisi ya Under the Same Sun.
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na wanafunzi wenye ulemavu
wa ngozi walio kwenye ‘summer camp’ katika Chuo cha Ualimu Butimba Jijini
Mwanza. Ametumia fursa hiyo kuelezea juhudi ambazo Serikali imekuwa ikizifanya
katika kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu ili waweze kupata elimu.
Naibu Waziri Ole Nasha
alisema katika kuendelea kutatua changamoto zinazowakabili wanafunzi wenye
mahitaji maalumu kwa sasa Wizara anayoiongoza inatekeleza Programu ya Elimu
Jumuishi ambayo inamuweka shuleni mtoto mwenye ulemavu na yule asie na ulemavu
kwa lengo la kuondoa fikra za kunyanyapaliwa lakini pia kujenga umoja upendo na
urafiki baina yao utakaowawezesha kulindana kwani siku zote mlinzi mzuri ni
rafiki na ndugu hivyo inasaidia kuondoa changamoto zilizopo.
Aidha, Serikali pia inatoa
mikopo kwa asilimia mia moja kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma
elimu ya juu kwa lengo la kuwasadia waweze kupata elimu zaidi kwani watu wenye
ulemavu wakipata elimu wanaweza sio tu kujikomboa wenyewe lakini kuwasaidia watu
wengine wenye changamoto hizo.
“Ninyi wenyewe mtakuwa
mashahidi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
katika Serikali yake kuna viongozi ambao wana ulemavu lakini kutokana na
umahiri na uwezo walio nao katika utendaji wameteuliwa katika nafasi hizo.
Tambueni kuwa watu wote wana haki sawa na hilo liko wazi,” alisema Naibu Waziri
ole Nasha.
Kiongozi huyo amewataka wanafunzi
hao kutambua kuwa wao ni watoto wa kitanzania hivyo wanatakiwa kuwa huru kwenye
nchi yao na kwamba Serikali itaendelea kuwalinda ili waweze kuishi lakini pia kusoma kama watu
wengine bila kudhuriwa na kitu chochote.
”wote ni mashahidi kwamba
kwa sasa Serikali imefanya jitihada
mbalimbali za kuhakikisha kwamba mnakuwa na usalama wa maisha yenu, sidhani
kama kuna kosa ambalo sasa ukipatikana nalo unachukuliwa hatua kubwa zaidi kama
kujaribu kuwadhuru watu wenye ualbino, na ndio maana sasa mnapata ulinzi kaeni
mkiwa huru kwa kuwa serikali inawajali,”aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.
Katika hatua nyingine Naibu
Waziri Ole Nasha amelitaka Shirika la Under The Same Sun kutambua kuwa Serikali inathamini mchango mkubwa
wanaoutoa katika kuwasaidia wanafunzi na
watoto wenye mahitaji maalum hasa watoto
ambao wana changamoto ya ulemavu wa ngozi na kuwataka kuhakikisha mafunzo wanayoyatoa
katika kambi za joto (summer camp) kila wanapokutana pamoja na mambo mengine yalenge katika kuwaonesha
watoto hao kuwa jamii inawajali na sio vinginevyo.
Wanafunzi wenye ulemavu wa
ngozi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole
Nasha wakati alipokutana nao kuzungumzia juhudi ambazo Serikali imekuwa
ikizifanya kutatua changamoto za watoto wenye ulemavu katika kupata elimu.
Nae Afisa kutoka Idara ya
Elimu ya Shirika la Under the Same Sun Omary Mfaume amesema Shirika hilo
linafadhili wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi kupitia programu za elimu
zinazojihusisha na ufadhili wa elimu na ile ya uhamasishaji jamii ambayo
inayowafundisha kwanini mtu anazaliwa na ualbino, changamoto zake na namna ya
kuzikabili changamoto hizo.
Akizungumza kwa niaba ya
wanafunzi wenzake Clara Maliwa ameiomba Wizara kuwa na utaratibu wa kuwatambua
Wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi wanaofanya vizuri katika masomo ili kutoa
changamoto kwa wengine ili waweze kufanya vizuri zaidi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.