Jumanne, 2 Julai 2019

NDALICHAKO ATAKA SKAUTI ITUMIKE KUJENGA UZALENDO KWA VIJANA NCHINI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako, ameuagiza uongozi wa Skauti nchini kuhahakikisha, wanatumia vijana wa skauti kuelimisha na kujenga uzalendo miongoni mwa makundi ya Vijana nchini .

Amesema hayo, katika uzinduzi wa semina elekezi ya Makamishna wa Skauti wa mikoa, Wilaya, Wajumbe wa Bodi na Kamati Tendaji za Skauti Nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Skauti wakati wa uzinduzi wa semina elekezi ya Makamishna wa Skauti wa mikoa, Wilaya,  Wajumbe wa Bodi na Kamati Tendaji za Skauti Nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Ndalichako amepongeza Chama cha Skauti Tanzania pamoja na Zanzibar kwa kushiriki na kufanikisha sherehe za maadhimisho ya Miaka 107 ya Skauti Zanzibar na kwa kuandaa semina hiyo elekezi, ili kuwangejea uwezo viongozi wake hususan katika mambo muhimu katika taifa ambayo kwa kiasi kikubwa yanahitajika kutolewa elimu juu yake kwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa.


Aidha amewataka viongozi hao kutumia Semina hiyo kama nyenzo muhimu itakayowasaidia kuelewa misingi, miongozo, sera na mikakati mbalimbali ili kuwalea vijana wanaowaongoza katika maadii mema ya chama cha Skauti na kupata ujuzi wa kitaalam utakaowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Waziri Ndalichako ambae pia ni rais wa Skauti Nchini, amesema Wizara ya Elimu kwa kutambua umuhimu wa Skauti Nchini katika malezi ya Vijana imetoa waraka wa kuhuisha uskauti shuleni na vyuoni hivyo kuagiza viongozi katika asasi na taasisi hizo kuhakikisha ustawi wa shughuli za uskauti unaendelea kwa kasi zaidi, huku akiwataka Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya kuratibu shughuli za Skauti katika maeneo yao, ikiwemo kuhakikisha kuwa walimu wanaosimamia shughuli za Skauti wanapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kusimamia vema shughuli hizo.

Waziri Ndalichako amepongeza hatua ya kushirikisha Vyombo vya Serikali kutoa elimu kuhusu masuala muhimu ya mtambuka kwa Taifa, ikiwa ni pamoja na masuala ya mapambano dhidi ya Rushwa na Madawa ya kulevya. Aidha ametumia nafasi hiyo kushukuru vyombo vilivyoshiriki kutoa elimu ikiwemo TAKUKURU, Jeshi la Zimamoto na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na  Dawa za Kulevya.
“Natoa wito kwa washiriki wote kusikiliza kwa makini mada hizo muhimu ili mkazitumie katika kutekeleza jukumu la kuwajengea vijana uzalendo, uadilifu na kuwa mstari wa mbele katika kufanya kazi na kupambana na majanga yanayolikabili Taifa letu.”
Skauti Mkuu Chama Cha Skauti Tanzania Mheshimiwa Mwantumu Mahiza akimkaribisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa uzinduzi wa semina elekezi ya Makamishna wa Skauti wa mikoa, Wilaya,  Wajumbe wa Bodi na Kamati Tendaji za Skauti Nchini iliyofanyika katika ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine Ndalichako kwa nafasi yake kama Rais wa chama cha Skauti na Waziri mwenye dhamana ya Elimu, amewaagiza wa Wakuu wa Shule na Wakuu wa Taasisi nyingine zenye vyama vya skauti kusimamia kwa makini shughuli za uskauti na kuepuka matumizi mabaya ya Skauti, ikiwemo kuwapa jukumu la utoaji wa adhabu kwa vijana wenzao.

“ Niombe sana uongozi suala la kutumia vibaya skauti kwa ajili ya kuumiza vijana wenzao lisijirudie tena  kwani lengo la Skauti ni upendo, jambo hili halikunifurhisha, Viongozi simamieni na fundisheni , upendo, amani , umoja na mshikamano ambazo ni nguzo kuu za taifa letu, kwa jinsi hii tukuwa na vijana shupavu wazalendo wachapakazi,ambapo tutakuwa tunaunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambae anasisitiza juu ya amani na uchapakazi katika kuifikisha nchi yetu katika uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia viwanda.”

Akizungumza kabla ya kumkaribisha waziri Ndalichako  Skauti Mkuu - Chama Cha Skauti Tanzania Mheshimiwa Mwantumu Mahiza, alimshukuru Waziri kwa kukubali mualiko na kusema kuwa Chama hicho kinaendelea kufanya kazi zake kimkakati  ikiwemo kutekeleza jukumu lake kubwa la kulea vijana, kuwajenga kuwa wazalendo walio tayari kulitumikia taifa.

Nae mlezi mteule wa Chama hicho Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Askofu Mkuu Jimbo la Mbeya Kanisa katoliki na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),lakini pia ni Skauti, ameishukuru Serikali kwa uteuzi wake akiwa mlezi wa tatu  katika Chama hicho. Walezi wengine, ni Rais Msataafu Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na Mheshimiwa Balozi Salim Ahmed Salim.  Aidha Askofu Nyaisonga ameahidi kuwa Skauti itayafanyia kazi maagizo ya Waziri kwa wakati na kuendelea kutoa kuduma bora kwa weledi popote watakapo hitajika.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua gwaride la Skauti lililoandaliwa kwa ajili yake wakati wa wakati wa uzinduzi wa semina elekezi ya Makamishna wa Skauti wa mikoa, Wilaya,  Wajumbe wa Bodi na Kamati Tendaji za Skauti.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.