Serikali imeipongeza Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutekeleza agizo la kurudisha mashindano ya
Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu (UMISAVUTA) huku ikiitaka kuhakikisha kuwa
michezo na Sanaa vinapewa kipaumbele katika mipango endelevu ya Wizara.
Pongezi hizo zimetolewa
Mkoani Mtwara. na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Kassim Mjaliwa wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMISAVUTA.
Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akipiga mpira kuashiria uzinduzi rasmi wa
mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini katika viwanja vya
Nangwada Sijaona mkoani Mtwara.
Dkt. Mwakyembe amesema eneo
la michezo na Sanaa ni sehemu muhimu katika makuuzi ya watoto kwani yanajenga
na kuimarisha afya ya mwanadamu lakini pia yanaimarisha mahusiano baina ya
raia.
“Kwa sasa nchi imeonesha
mafanikio makubwa katika michezo hivyo ili Taifa lipate wataalamu na vipaji
sahihi katika michezo na Sanaa hatuna budi kuanza ngazi za awali za elimu, “alisema
Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. leonard Akwilapo amesema Wizara
imejipanga vyema katika kuendeleza michezo ili kuongeza furaha kwa wananchi wa
Tanzania kwa kuziona timu zinashiriki na kushinda mashindano makubwa ya
kimataifa.
“Kama Wizara tunasema muda
wa kushiriki sasa umetosha tunataka kuwa washindani na mashindano haya ni
sehemu ya maandalizi ya kutekeleza azma hiyo,” alisema Katibu mkuu Akwilapo.
Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana
na washiriki wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu
nchini wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo mkoani Mtwara.
Katibu Mkuu Akwilapo alisema
kupitia mashindano haya washiriki wataongeza ujuzi katika michezo na kuwa walimu ambao
wataimarisha michezo wakati watakapokuwa kazini huku wengine wakiendeleza
vipaji vyao na kuwa hazina ya Taifa kwa siku za usoni.
Michezo inayoshindaniwa ni
pamoja na mpira wa Pete, mpira wa miguu, wavu kikapu, riadha, mashindano ya
uchoraji, Sanaa za maonesho, ngoma pamoja na kwaya. Mingine ni pamoja na ile ya
kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kumjengea mwalimu
umahiri wa kuandaa na kutumia zana nzuri za kufundishia.
Baadhi ya Walimu Tarajali wakiingia katika uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara
wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini
mapema hii leo mkoani Mtwara.
Nae Kaimu Mkurugenzi
Msaidizi kutoka Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia Agusta Lupokela amesema mashindano hayo yaliyoanza Oktoba 25,
2019 yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, 2019 na yameshirikisha Kanda saba
ambazo ni Kanda ya Kati, Kusini, Mashariki, Magharibi, Kanda ya Ziwa, Kaskazini
na Kusini ambazo zimeundwa kulingana na vyuo vya ualimu.
Juni 10, 2019 katika Viwanja
vya Nagwanda Sijaona mkoani Mtwara wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania anafungua mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA alitoa agizo kwa
Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa mashindano ya michezo na Sanaa kwa Vyuo vya
Ualimu yanarejeshwa.
Baadhi ya Walimu Tarajali wakiandamana kuelekea katika
uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo
na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini mapema hii leo mkoani Mtwara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.