Serikali ya Awamu ya Tano
imeweka kipaumbele katika kuimarisha michezo kama eneo muhimu la mtaala wa
mafunzo ya ualimu kutokana na ukweli kwamba michezo inaimarisha stadi za
kujifunza, nidhamu na ni ajira pia.
Hayo yamesemwa Mkoani Mtwara
na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa
kufunga Mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania
Bara (UMISAVUTA).
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa kombe la ushindi wa mpira wa miguu kwa wachezaji wa Kanda ya Ziwa wakati wa ufungaji wa mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa ya Vyuo vya Ualimu UMISAVUTA yaliyomalizika mkoani Mtwara.
Amesema pamoja na kuwepo kwa
mchepuo wa michezo katika baadhi ya vyuo vya Ualimu ni vizuri vyuo hivyo
kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu wakaweka mikakati ya kuhakikisha kuwa
ufundishaji na ujifunzaji wa michezo na Sanaa unalenga kuwawezesha vijana
kufanya vizuri katika eneo hilo kwa maendeleo yao na Taifa.
Ametaja vyuo ambavyo kwa
sasa vinatoa mchepuo wa michezo kuwa ni Chuo cha Ualimu Tarime, Butiama,
Butiama Mtwara Kawaida na Ilonga na kwamba Wizara itahakikisha kuwa michezo
inaimarishwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini.
Naibu Waziri Ole Nasha amevitaka
vyuo vya ualimu kuhakikisha vinaendeleza michezo chuoni kutoka na faida
zitokanazo na michezo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wahitimu wa mafunzo ya ualimu wanapata
mafunzo ambayo wakihitimu wanakwenda kuwa walimu mahiri wa michezo katika shule
za msingi na sekondari ambapo ndipo wanamichezo na wasanii wanaandaliwa.
“Nimefarijika kuona mashindano
ya michezo na Sanaa kwa vyuo vya ualimu imerudi tena baada ya kutokuwepo kwa
miaka 20 iliyopita hatuna budi kuwekeza katika michezo kwa sababu ni fursa za kuweza
kusaidia kukua kiuchumi. Nchi nyingi duniani michezo imekuwa sehemu kubwa ya kusaidia
kukua kiuchumi,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akisalimiana na wachezaji kabla ya kuanza mechi ya fainali wakati wa ufungaji wa Mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara yaliyofanyika Mkoani Mtwara.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu
wa Mkoa wa Mtwara ambae pia ni Afisa Elimu Mkoa Germina Mng’aho amesema
kufanyika kwa michezo hiyo ni utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi
ambayo inataka kuwepo kwa mashindano ya michezo kwa shule na vyuo ili kuwezesha
kuinua vipaji ambavyo vitaleta mafanikio katika michezo ya kitaifa na kimataifa.
Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi
Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Agusta Lupokela amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutambua
faida zinazopatikana katika michezo ikiwemo stadi za kujifunza na kuamua
kurejesha mashindano ya michezo kwenye Vyuo vya Ualimu.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na TeknolojiaAgusta Lupokela akikabidhi kikombe kwa mwakilishi wa Kanda ya Kaskazini ambao ni washindi wa mbio wakati wa kufunga mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu, UMISAVUTA mkoani Mtwara
Akitoa taarifa ya mashindano
hayo kwa Naibu Waziri Mwenyekiti wa
UMISAVUTA Taifa Agustine Sahili amesema kuwa michezo hiyo imeendeshwa kulingna
na taratibu za michezo na matokeo yameamuliwa kwa weledi na haki katika kupata
washindi.
Sahili ameiomba Wizara kuimarisha kozi ya michezo na fani mbalimbali
za ndani katika vyuo vya ualimu ili wataalamu waweze kupatikana shuleni ambako
ndiko chimbuko halisi la vipaji linapatikana lakini pia kuwajengea uwezo
wasimamizi na waamuzi wa michezo kwa kuendesha kozi fupi na ndefu kwa
kushirikiana na Wizara ya Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Pia ameiomba Wizara kuongeza
wakufunzi wa michezo na Sanaa vyuoni kwani kwa sasa vyuo vingi havina wakufunzi
wa aina hiyo hali inayodunisha uendeshaji wa michezo na ukuzaji wa vipaji kwa
vijana chuoni ambapo pia inasababisha shule za msingi na sekondari kukosa
walimu mahiri katika michezo na Sanaa.
Wanamichezo wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa kufunga mashindano ya Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ulimu yaliyofanyika Mkoani Mtwara.
Nae Mshiriki wa Mashindano
ya Michezo na Sanaa Albert Thomas kutoka Kanda ya Ziwa ameishukuru Serikali kwa
kurejesha mashindano ya UMISAVUTA kwani inasaidia kujenga afya na akili lakini pia inasaidia kuwa na uelewa wa
masula ya michezo na kutoa elimu ya michezo kwa wanafunzi ambao watakwenda
kuwafundisha baada ya kumaliza masomo.
Ameiomba Serikali kuendeleza vipaji vya wanamichezo wanaoshindana katika
mashindano ya ngazi ya shule na vyuo na kuonekana washindi ili vipaji hivyo visiishie
kwenye ngazi ya kitaifa bali katika ngazi ya kimataifa.
Ufungaji wa mashindano ya
Kitaifa ya Michezo na Sanaa kwa vyuo vya ualimu yaliyoanza Oktoba 25, 2019 na
kuhitimishwa Oktoba 31, 2019 yamepambwa na mechi kati ya Kanda ya ziwa na kanda
ya kusini ambapo kanda ya ziwa wameibuka kidedea baada ya kuwafunga kanda ya
kusini goli moja kwa sifuri.
Kanda ya Ziwa wakifurahia kupata vikombe vya ushindi katika michezo mbalimbali ambayo wameshindania katika mashindano ya kitaifa ya michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu Tanzania Bara yaliyofanyika Mkoani Mtwara.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.