Serikali za Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano
ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu
100 nchini ambao watakuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi 5,000 wa
Kitanzania katika ngazi ya sekondari.
Makubaliano
hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe.
Frederic Clavier na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia,
Dkt. Leonard Akwilapo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla
ya Dola za Kimarekani 250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.
Katika
kikao hicho wamekubaliana kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa
(Alliance Francais) ili kupanga utekelezaji wa mafunzo hayo ya walimu.
Aidha,
Balozi Clavier ameonesha kuwepo kwa fursa za Watanzania kusoma programu
zisizopungua 2,000 za Kiingereza nchini Ufaransa. Ameeleza kuwa
Ufaransa inaandaa Maonesho ya Elimu ya Juu (Higher Education Fair)
yatakayofanyika nchini Mei 2021 ambapo vyuo 20 vya Ufaransa vitashiriki
kutafuta ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania na Sekta binafsi.
Akizungumza
katika kikao hicho, Katibu Mkuu Akwilapo ameushukuru Ubalozi wa
Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano katika kukuza na kuimarisha elimu ya
Juu nchini kupitia ufadhili wa mafunzo hayo na kuagiza wahusika katika
Wizara anayoisimamia kuhakikisha vikao vya kitaaluma vinafanyika ili
mafunzo hayo yaweze kuanza kwa wakati uliopangwa.
Katibu
Mkuu Akwilapo pia ameahidi kuweka wazi kwa Watanzania kuhusu kuwepo kwa
fursa hiyo ya kusoma programu za Kiingereza nchini Ufaransa ili
Watanzania waweze kuchangamkia fursa hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.