Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kujikita katika kutoa mafunzo ya fani zinazopendwa na zinazotoa ajira badala ya kuendelea kuwa na fani ambazo hazina wanafunzi katika eneo husika.
Dkt.
Semakafu ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua ukarabati na
uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same kilichopo Mkoani
Kilimanjaro ambapo amesema ni vizuri vyuo vikajiimarisha kwenye utoaji
mafunzo kwa fani zenye wanafunzi wengi na kuachana na zile zenye
wanafunzi wachache.
“Kuanzia
mwaka huu, kila chuo cha wananchi kitafundisha fani ambazo zinahitajika
katika maeneo husika kwa maana ya kuwa na wanafunzi wa kutosha, hakuna
chuo chochote kusajili fani ambazo zina wanafunzi wachache ama chini ya
kumi na mbili, Serikali haiajiri walimu kufundisha wanafunzi wawili
hivyo hakuna haja ya kuweka fani ambazo hazina wanafunzi wa kutosha,”
amesisitiza Dkt. Semakafu.
Aidha,
Naibu Katibu Mkuu huyo amesema mpango wa 'Elimu haina mwisho'
unaotolewa katika vyuo hivyo ni utaratibu wa kutoa fursa kwa watoto
waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi
na kijamii ili kuwasaidia kupata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuendelea
na masomo na kuendesha maisha yao pindi watakapohitimu hivyo wanapaswa
kufundishwa kama wanafunzi wengine bila kuwatenga.
Amesema
Serikali iliamua watoto hao wasome katika vyuo hivyo kupitia mfumo usio
rasmi bila malipo yoyote kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa
nyingine ya kuendelea na masomo na kuutaka Uongozi wa chuo cha Maendeleo
Same kuwarudisha chuoni wanafunzi wote walioacha masomo kwa sababu
mbalimbali ili waweze kumaliza masomo yao.
“Tumeanza
programu hii kwa lengo la kupata watoto wote walioacha shule na ndio
maana unaona hata wasichana walioacha shule kutokana na changamoto
mbalimbali tumewarudisha katika mfumo huu ili waje waendelee na masomo
na na wale wenye watoto hata tuna shule za chekechea kwa ajili ya watoto
wao,” amesema Dkt. Semakafu.
Naibu
Katibu Mkuu Dkt. Semakafu amekagua miundombinu iliyokarabatiwa na
kuboreshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo ameuagiza
uongozi wa chuo hicho kufanya marekebisho katika baadhi ya miundombinu
ambayo haikukarabatiwa vizuri.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Same, Edward Mdee akitoa taarifa ya chuo hicho kwa Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ave Maria Semakafu alipofika chuoni hapo kukagua maendeleo ya chuo hicho. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.