Jumapili, 20 Agosti 2017
Jumatano, 9 Agosti 2017
TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI.
1.0 Serikali
inatarajia kuajiri Walimu 92 wa
Shahada na 174 wa Stashahada wa
masomo ya Fizikia, Hisabati, Kilimo na Biashara kwa Shule za Sekondari na
Walimu 2,767 wa Cheti kwa Shule za
Msingi.
2.0 Waombaji kwa
shule za Sekondari wawe waliohitimu mafunzo ya Ualimu mwaka 2016 au kabla, na
wale wa Shule za Msingi wawe waliohitimu mafunzo yao mwaka 2014 au kabla.
3.0 Sifa za
Waombaji:
3.1
Walimu wa Sekondari:
(i)
Shahada
ya Elimu (Bachelor with Education) au Shahada ya Ualimu (Bachelor of Education)
yenye somo moja la kufundishia au zaidi au Shahada isiyo ya Ualimu/Elimu yenye
somo moja la kufundishia au zaidi pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu
(Postgraduate Diploma in Education) kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu
vinavyotambulika na Serikali. Masomo ya kufundishia ni kati ya Fizikia, Hisabati, Kilimo au Biashara.
(ii)
Stashahada
ya Ualimu katika masomo yaliyoainishwa kwenye kipengele Na. 2.1 (i) hapo juu.
(iii)
Cheti
cha Kidato cha Sita
(iv)
Cheti cha Kidato cha Nne
3.2
Walimu wa Shule za Msingi:
(i)
Astashahada
ya Ualimu iliyotolewa na Chuo kinachotambuliwa na Serikali.
(ii)
Cheti
cha Kidato cha Nne (wenye cheti Kidato cha Sita watapewa kipaumbele).
4.0 Utaratibu wa
Kutuma Maombi:
(a)
Maombi
yatumwe kupitia Posta kwa njia ya Rejesta (EMS). Juu ya bahasha iandikwe kwa mkono "Maombi ya Kazi ya Ualimu - Sekondari au Maombi ya Kazi ya Ualimu - Msingi".
(b)
Mwombaji
aambatishe nakala za Vyeti vilivyothibitishwa (Certified) na Mwanasheria pamoja
na "Transcript".
NB: Barua za maombi zisiwasilishwe kwa
mkono. Barua zitakazowasilishwa kwa
mkono hazitapokelewa.
5.0 Masuala Mengine
ya Kuzingatia:
(a)
Mwombaji
aandike majina yake yote matatu. Kama
Vyeti vina majina mawili, utaratibu wa kisheria wa kuongeza jina uzingatiwe.
(b)
Mwombaji
aambatishe nakala ya Cheti cha Kuzaliwa.
Mwisho wa kupokelewa
maombi ni tarehe 31/08/2017.
Maombi yatumwe kwa:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia,
S. L. P.
10,
40479 DODOMA.
Imetolewa na:
KATIBU MKUU
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alhamisi, 27 Julai 2017
Waziri Mkuu afungua Maonyesho ya 12 ya Vyuo vya Elimu ya Juu
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu
Tanzania TCU kuhakikisha programu za masomo zinazoanzishwa na Vyuo vya elimu ya
juu nchini zinazingatia mahitaji ya Taifa na soko la ajira.
Waziri Mkuu ametoa agizo
hilo leo katika ufunguzi wa maonyesho ya kumi na mbili (12) ya vyuo vya elimu
ya juu yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam ambapo
amesema serikali inayathamini maonesho hayo kwa kuwa yanatoa fursa ya vijana
kujifunza na kupata taarifa za vyuo na programu wanazoendesha moja kwa moja
Naye Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Saimon Msanjila ameitaka TCU
kuhakikisha utaratibu uliotumika kufanya uhakiki wa vyuo na programu na kupelekea
baadhi ya vyuo na programu kufungiwa utumike huohuo kuhakiki pindi
vitakaporekebisha mapungufu
yaliyojitokeza awali. Aidha, amevitaka vyuo vyote vilivyofungiwa kupeleka TCU
majibu ya maeneo walioambiwa yana
mapungufu kama utaratibu unavyotaka
badala ya kuyapeleka Wizarani.
Ijumaa, 21 Julai 2017
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ampongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwa kusimamia vizuuri ujenzi wa miundombinu ya shule
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya amempongeza Mkuu wa Wilaya ya
Korongwe Mhandisi Robert Gabriel kwa kuhamasisha wananchi kuchangia katika
sekta ya elimu ambapo mchango huo wa wananchi umewezesha mradi wa ujenzi madarasa
uliofadhiliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Mradi
wa lipa kulingana na matokeo kufanikiwa kwa kiwango kikubwa pamoja na ujenzi wa
miundombinu mengine ya elimu inayofanywa na Halmashauri.
Mhandisi Manyanya ametoa
pongezi hizo leo wilayani Korongwe Mkoani Tanga katika wakati wa ziara yake
wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati
unaofanywa na Mradi wa Lipa kwa Matokeo (P4R). Amesema Mkuu wa wilaya huyo
pamoja na kamati yake wameweza kuhamasisha wananchi kuchangia katika mradi huo
na kuwezesha kujengwa madarasa zaidi ya yaliyokuwa yamelengwa hapo awali kwani
wananchi walichangia nguvu kazi zao, mifuko ya saruji na vifaa vinine vya
ujenzi.
Naibu Waziri ametolea mfano
wa ujenzi wa miundombinu ya vyoo katika shule ya Msingi Kilimani ambapo
wameweza kuijenga matundu ya vyoo 12 kwa gharama ya shilingi milioni 11 wakati sehemu
nyingine ambazo ameshazitembelea wameshindwa kumaliza ujenzi wa vyoo kama hvyo kwa
gharama hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya
Korongwe Mhandisi Robert Gabriel amemueleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri yake
imejipanga kuhakikisha wanaondoa tatizo la miundombinu ya madarasa katika wilaya
yake kwa kujenga madarasa 360 pamoja na ofisi za walimu 70 ndani ya kipindi cha
miezi 12 kwa kutumia nguvu za wananchi.
Katika ziara hiyo Mhe Naibu
Waziri alitembelea shule za Msingi Kilimani, Bagamoyo, Matondoro, Kilole, Kwasemangube,
Shule ya Sekondari Semkiwa pamoja na Chuo cha Ualimu Korogwe.
Ijumaa, 14 Julai 2017
Naibu Waziri wa Elimu akagua ujenzi na Ukarabati katika shule ya Sekondari Mbweni Tete
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya ameonyesha
kutokuridhishwa na hatua ya Halmashauri ya Kinondoni kuhamisha fedha za ujenzi
wa madarasa, mabweni na vyoo zilizokuwa zimetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknlojia kupitia mradi wa lipa kwa matokeo kwa shule ya Sekondari ya
Kambwangwa na kupelekwa katika Shule ya sekondari Mbweni tete bila kufuata
utaratibu wa kuitaarifu wizara iliyotoa fedha hizo.
Mhandisi
Manyanya ameyaeleza hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya
kuzitembelea shule mbalimbali kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi na
ukarabati unaofanywa na Mradi wa Lipa kwa Matokeo (P4R). Amesema kuhamishwa kwa
mradi si tatizo lakini kuhamisha bila kutoa taarifa ndo tatizo lilipo kwani
wizara imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi huo hivyo ni lazima kufanya
ufatiliaji ili kuweza kujirizisha kama ujenzi unafanyika lakini wakati
najiandaa kwenda Kambagwa ndipo alipotaarifa kuhusu kuhamishwa kwa mradi huo.
“Leo
wakati tunataka kuanza kwenda kuangalia ujenzi ulipofikia lakini tukapewa
taarifa kuwa mradi huo haupo Kambangwa na ulihamishwa kupelekwa eneo jingine,
hivyo ni muhimu kupeana taarifa maana kuhamishwa kwa mradi kunaleta hoja za
ukaguzi” alisisitiza Mhandisi Manyanya.
Naibu
Waziri amesema ujenzi wa miundombinu hiyo katika Halmashauri mbali mbali
imekuja baada ya wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI uwepo wa umuhimu
wa kuongeza miundombinu ya madarasa,
mabweni na vyoo katika baadhi ya shule ili kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahili kwa ajili ya kujiunga na masomo ya
kidato cha tano. Amesma lengo la serikali ni kuona wanafunzi wote waliofaulu
wanapata nafasi ya kuendelea na masomo yao ya kidato cha tano bila mmoja
kuachwa.
Naibu Waziri wa Elimu agiza shule zilizotengwa kwa ajili ya elimu maalum kupatiwa mahitaji muhimu
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya ameziagiza
Halmashauri zote nchini kuhakikisha shule zilizotengwa kwa ajili ya wanafunzi
wenye mahitaji maalum zinapewa haki zake ikiwa ni pamoja na kupatiwa vifaa vya
kufundishia na kujifunzia ili kuwezesha
wanafunzi hao kupata elimu sawa na wanafunzi wengine.
Naibu
Waziri Manyanya ametoa agizo hilo alipofanya ziara kwenye shule ya msingi Sinza Maalum iliyopo jijini Dar es Salaam kwa
lengo la kujionea mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika shule hiyo,
mbapo pia amezitaka halmashauri hizo
kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni yatakayosaidia kupunguza ugumu wa
wanafunzi hao kuhudhuri masomo kutokana
na sababu mbalimbali za kimaumbile za watoto hao na hivyo kuwafanya wengine kushindwa
kutembea umbali mrefu kufuata shule.
Pia
Naibu waziri alitembelea shule ya sekondari ya Mbweni Teta kukagua ujenzi wa
madarasa, mabweni na vyoo unaofanywa na Wizara ya Elimu, Sayasni na Teknolojia
Kupitia Programu ya lipa kulingana na matokeo, P4R kwa ajili ya wanafunzi wa
kidato cha Tano wanaotarajiwa kuanza shule Julai 17, mwaka huu.
Jumanne, 11 Julai 2017
Naibu Waziri wa Elimu akabidhi Bendera ya Taifa kwa wanafunzi wa Sayansi
Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya leo amekabidhi Bendera ya Taifa
kwa wanafunzi saba wanaosoma masomo ya sayansi wanaokwenda kuiwakilisha nchi
katika mashindano ya First Global Challenges nchini Marekani. Makabidhiano hayo
yamefanyika katika shule ya Sekondari ya wasichana Jangwani.
Katika makabidhiano hayo
Mhandisi Manyanya amewataka wanafunzi wote nchini kusoma kwa bidii masomo ya
sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha ndoto ya Tanzania ya kuwa na
uchumi wa kati kupitia viwanda na biashara inafanikiwa na kwamba wizara
tutaendelea na jukumu lake la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia
ili wanafunzi wote waendelee kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.
Shule zilizotoa wanafunzi
watakaoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Jangwani, Azania, Jamhuri,
Benjamini Mkapa, Feza na Kisutu.
Naye mratibu wa mashindano hayo
kwa upande wa Tanzania ndugu Mkufu Shabani Tindi alisema mashindano haya
yameanzishwa na kufadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Marekani
liitwalo FIRST yenye maana ya for
inspiration and recognition of science and technology lenye lengo la
kuhamasisha ulimwenguni kote vijana wanaosoma masomo ya sayansi, uhandisi,
teknolojia na hesabu kuweza kutatua changamoto mbalimbali ulimwenguni
Wanafunzi watakaoshiriki
wanatarajia kuondoka kesho Juni 12, 2017 na watakuwa nchini Marekani kwa ajilia
ya mashindano hayo makubwa kiulimwengu ambapo
zaidi ya nchi 170 zitashiriki.
Naye mmoja wa washiriki
Raymond Benedict kutoka Shule ya Sekondari Jamhuri amesema yeye wenzake
wamejiandaa vizuri katika kuhakikisha wanaiwakilisha nchi katika mashindano
hayo vizuri na kwa ufahari.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)