Jumanne, 25 Septemba 2018

WAZIRI NDALICHAKO ASISITIZA WADAU KUTUMIA TAKWIMU SAHIHI KATIKA MACHAPISHO YAO.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka wadau wa Elimu kuhakikisha wanatumia takwimu sahihi zilizotolewa na Mamlaka husika wakati wa kuandaa machapisho yao ili kuepuka kupotosha umma.


Waziri Ndalichako amesema hayo leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu unaoshirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi kuwa kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu na ndio maana Wizara hiyo imekuwa ikitengewa bajeti ya kutosha na bajeti ya Wizara hiyo haijawahi kushuka.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu uliofanyika Jijini Dodoma. Waziri Ndalichako amewataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina mafanikio, changamoto na kuwa na mikakati ya pamoja itakayosaidia Serikali kufikia malengo waliojiwekea katika Sekta ya Elimu.

Waziri Ndalichako amesema kumekuwa na upotoshwaji wa takwimu zinazotolewa kwenye machapisho mbalimbali kuwa bajeti ya Wizara ya Elimu imeshuka hadi kufikia asimilia 56 suala ambalo Waziri Ndalichako amelikanusha na kueleza kuwa bajeti ya Wizara hiyo haijawahi kushuka na mpaka Juni 2018 bajeti ya Wizara hiyo ni asilimia 86.5.

“Bajeti ya Wizara ya Elimu haijawahi kushuka kwa kuwa kipaumbele cha serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli ni Elimu, hivyo takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye machapisho mbalimbali sio sahihi  na badala yake takwimu sahihi za bajeti ya Wizara ya Elimu ni asilimia 86.5 hadi kufikia Juni 2018,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu unaofanyika Jijini Dodoma. 

Waziri Ndalichako amewaambia wadau wa Mkutano huo wa AJESR unaofanyika Jijini Dodoma kuwa Elimu ndio nyenzo muhimu inayotoa dira na muongozo ili kuhakikisha Taifa linakuwa na watu walioelimika kwa maendeleo ya Taifa katika kufikia uchumi wa viwanda na uchumi wa kati ifikapo 2025.

Waziri Ndalichako amewataka washiriki wa mkutano huo kujadili kwa kina mafanikio, changamoto na kuwa na mikakati ya pamoja itakayosaidia Serikali kufikia malengo waliojiwekea katika Sekta ya Elimu.
Wadau wa Elimu walioshiriki Mkutano Mkuu wa mwaka wa kutathmini Sekta ya Elimu wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa Ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Jijini Dodoma.  

Mkutano huo wa mwaka wa kutathmini  Sekta ya Elimu umekuwa ukishirikisha wadau mbambali wa ndani nan je ya nchi  ulianza mwaka 2008 na umekuwa ukifanyika kila mwaka.

Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Upatikanaji wa Elimu bora kufikia Tanzania ya Viwanda” umeanza leo  na utakamilika Septemba 28, 2018. 

Alhamisi, 20 Septemba 2018

OLE NASHA: TCU NA BODI YA MIKOPO SHIRIKIANENI WANAFUNZI WAPATE MIKOPO KWA WAKATI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia mheshimiwa William Ole Nasha ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu nchini  (TCU) kuhakikisha  inakamilisha uratibu wa udahili wa wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuwezesha zoezi la upangaji wa mikopo kufanyika  katika muda uliopangwa.

Naibu Waziri ametoa agizo hilo alipokutana na viongozi wa TCU  jijini Dar es Salaam ili kupata taarifa ya maendeleo ya udahili huo ambapo amesema kukamilika mapema kwa taratibu za udahili itawezesha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)  kupanga na kutoa mikopo kwa wanafunzi hao mapema.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe.Wiliam Ole Nasha akizungumza na viongozi wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini alipokutana nao Jijini Dar es Salaam ili kupata taarifaya uratibu wa udahili wa wanafunzi wa Elimu ya juu.
“TCU mkifanya vibaya katika uratibu wa udahili Bodi ya Mikopo ndio inayoathirika kwani lawama zote huishia huko na  siyo TCU, hivyo ili kuweka utaratibu mzuri ni vyema mkafanyakazi kwa ukaribu na kushirikiana ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza,” amesisitiza Naibu Waziri huyo.

 Katika hatua nyingine,  Naibu Waziri amekutana na watendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na kuwataka kuhakikisha wanashughulikia kwa haraka upangaji na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi ikiwa ni pamoja na kuwasadia wanafunzi pale zinapotokea changamoto .
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Abdul Razaq Badru akizungumza na Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam.

Jumatano, 19 Septemba 2018

PROF MDOE AMESEMA TANZANIA IKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA IAEA KATIKA KUENDELEZA MATUMIZI SALAMA YA NGUVU ZA NYUKLIA


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe ameongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano Mkuu wa 62 wa kimataifa wa kuendeleza matumizi salama ya nguvu za nyuklia unaofanyika mjini Vienna nchini Austria.

Akizungumza katika mkutano huo mjini Vienna Profesa Mdoe ameishukuru IAEA kwa kuisaidia nchi ya Tanzania mashine ya kuchunguza na kutibu saratani ambayo inatumika katika hospitali ya Bugando iliyopo mkoani Mwanza na misaada ya kiufundi katika hospitali ya Saratani ya Ocean Road iliyopo jijini Dar es salama pamoja na misaada ya kuwasomesha  wataalam kwenye eneo la Teknolojia  ya nguvu za nyuklia. 
     
Naibu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe akizungumza katika mkutano wa kimataifa unaofanyika mjini Vienna, nchini Austria kuhusu matumizi salama ya nyuklia.

Profesa Mdoe pia amekieleza kikao hicho cha kimataifa kuwa nchi ya Tanzania iko tayari  kushirikiana na IAEA katika kuendeleza matumizi salama ya nguvu ya nyuklia. 

Balozi wa kudumu kwenye Mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva nchini Uswis James Msekele naye anashiriki mkutano huo.

Mkutano huo ulioanza Septemba 17 utahitimishwa Septemba 21, 2018 huko mjini Vienna nchini Austria.


Jumatano, 12 Septemba 2018

WIZARA YA ELIMU YAWAJENGEA UWEZO WABUNGE WA KAMATI YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII KUHUSU MAJUKUMU YANAYOTEKELEZWA NA WIZARA HIYO


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia leo imewajengea uwezo Wabunge wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa kuwasilisha majukumu 14 yanayotekelezwa na Wizara hiyo kwa mujibu wa hati idhini iliyotolewa April 22, 2016.

Akiwasilisha majukumu hayo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Makuru Petro ametaja majukumu hayo kuwa ni pamoja na kutunga na kutekeleza Sera za Elimu, utafiti, Huduma za Maktaba, Sayansi na Teknolojia na uendelezaji wa mafunzo ya Ufundi, kuendeleza Elimu kwa kutoa ithibati ya mafunzo ya Ualimu na Maendeleo ya kitaalamu ya Walimu, Kusimamia uendelezaji wa mafunzo katika vyuo vya Maendeleo ya wananchi, na kusimamia mfumo wa tuzo wa Taifa.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akifafanua jambo kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Wizara hiyo wakati wa kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii mkoani Dodoma.

Majukumu mengine ni kuainisha mahitaji ya nchi katika ujuzi, kuweka viwango vya Taaluma ya Ualimu ikiwemo kuanzisha bodi ya kitaalamu ya walimu, kusimami ithibati na uthibiti ubora wa shule kwa kuweka viwango, kusimamia Huduma za machapisho ya kielimu ikiwemo mitaala na vitabu, kuimarisha utumiaji wa Sayansi, Teknolojia na hisabati, kuendeleza wataalamu wa ndani katika Sayansi na Teknolojia, kuratibu na kusimamia utafiti, ubunifu katika fani za Sayansi na Teknolojia, kusimamia Tume ya Taifa ya UNESCO, uendelezaji wa Rasilimali watu na kuratibu shughuli za Idara, mashirika, wakala, programu na miradi iliyo chini ya Wizara.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt. Aneth Komba akiwasilisha utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo wakati wa kikao na  Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika mkoani Dodoma.

Kupitia uwasilishaji wa majukumu hayo ya Wizara wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo walipata fursa ya kujibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na Wabunge kwa lengo la kupata uelewa.

Baadhi ya Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakishiriki kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika mkoani Dodoma
Taasisi zilizoshiriki katika kujibu maswali mbalimbali ya Wabunge ni pamoja na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, (NACTE), Tume ya vyuo Vikuu Tanzania, (TCU), Taaaisi ya Elimu Tanzania (TET).
1.      Baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakishiriki kikao cha pamoja na Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kilichofanyika mkoani Dodoma

Jumamosi, 8 Septemba 2018

WAZIRI NDALICHAKO ASEMA SERIKALI IKO TAYARI KUSHIRIKIANA NA TAASISI BINAFSI


Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa , Joyce Ndalichako amesema  serikali iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano katika Taasisi binafsi ambazo zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya Elimu hapa nchini.

Waziri Ndalichako amesema hayo mkoani Dodoma wakati akizindua jengo la shule ya Msingi Misercodia inayomilikiwa na kanisa katoliki Shirika la Watawa wa Misericordia.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wkiwa na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda wakati wa uzinduzi wa  Jengo la Shule ya Msingi Misercordia Mkoani Dodoma

Waziri Ndalichako amesema Serikali imekuwa ikitambua na kuheshimu kazi kubwa inayofanywa na kanisa hilo katika kusaidia ujenzi wa miundombinu kwenye sekta ya Afya na Elimu hapa nchini na ikiwa ni pamoja na  kutatua changamoto mbalimbali kwa wakati.

"Wakati nakuja kuzindua shule hii  nilimtaarifu Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli na ametuma salamu, amesema niwaambie anawashukuru sana Maaskofu na Watawa kwa kuwa  mnaunga mkono juhudi za Serikali katika  ushiriki wa miradi mbalimbali ya maendelea kwa vitendo,”amesema Waziri Ndalichako.
Waziri akiwa aa Watawa wakati wa kuzindua Shule ya Kanisa ya Misercordia iliyopo Mkoani Dodoma ambapo Serikali imesema iko tayari kushirikiana na Taasisi Binafsi katika maendeleo.

Waziri huyo wa Elimu amesema , ujenzi wa Miundombinu hiyo umekuja wakati muafaka ambapo uhitaji wa shule za mchepuo wa kingereza ni mkubwa , kutokana na watumishi wengi wa serikali kuhamia Dodoma na hivyo kuhitaji shule kwa ajili ya watoto wao.

Kuhusu malezi ya wazazi, Waziri amesema hivi sasa wazazi wamesahau majukumu yao na badala yake wamekuwa wakifanya kazi zote ambazo zilipaswa kufanywa na watoto jambo ambalo sio sawa kwani wanajenga taifa la wavivu.


Wanafunzi na Walimu wa Shule hiyo ya Misercordia wakati wa uzinduzi wa Jengo la gorofa katika shule hiyo.

Waziri Ndalichako pia amezipongeza shule  nyingine za dini kwa kusimamia maadili kwa wanafunzi, ambapo ametumia  nafasi hiyo kuwakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwa kujenga miundombinu ya shule za msingi na sekondari kwani hivi sasa Dodoma inauhitaji mkubwa wa shule kwa sasa.

Waziri Ndalichako ameipongeza shule kwa kufanya vizuri katika matokeo ya kidato Cha Nne na Sita na kuongoza kitaifa katika somo la kiingereza, pia amezipongeza shule nyingine za dini kwa kusimamia maadili kwa wanafunzi.


Uzinduzi Jengo la   Shule ya Misercordia, iliyopo Mkoani Dodoma uzinduzi huo umefanywa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Prof. Joyce Ndalichako ambapo Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda pia alishiriki shughuli hiyo.

Alhamisi, 6 Septemba 2018

ALIYOYASEMA WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA PROF. JOYCE NDALICHAKO LEO WAKATI WA MAHOJIANO NA TBC TAIFA KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA BODI YA KITAALAMU YA WALIMU


- Lengo la Bodi ni kuwa na Muundo na Chombo Cha Kisheria ili kutambua rasmi taaluma ya Ualimu kama zilivyo taaluma nyingine

- Ili kutimiza malengo yaliyowekwa na Serikali katika Elimu, thamani ya walimu ni jambo ambalo linapewa kipaumbele sana.

-Muswada wa Sheria ya bodi ya kitaalamu ya walimu umekuwa shirikishi katika hatua zote ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha Walimu,Maafisa Elimu wa Wilaya, Mikoa,Wathibiti Ubora,Chama Cha Walimu Tanzania,Taasisi mbalimbali na Wizara ikiwemo ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI).

- Wadau wengine walioshirikishwa Kuanzia hatua za awali ni pamoja na Haki Elimu, CHAKAMWAKA, TAPIE, TAMONGSCO na Mtandao wa Elimu Tanzania(TEN/MET)

- Malengo ya Bodi hii ya walimu hayafanani na chombo kingine, vyama vingine vinaangalia maslahi ya walimu wakati bodi inaenda kuleta hadhi kwa kutambua walimu wote waliopo na wasiokuwepo madarasani.

-Tume ya Utumishi wa walimu imejikita katika utumishi kwa maana ya kuangalia orodha ya walimu walioajiriwa na serikali na uratibu wa masomo wakati bodi itaangalia mabadiliko mbalimbali katika dunia ikiwa ni pamoja na kuangalia nafasi za kuwaendeleza walimu.

-Bodi pia itasimamia vigezo kwa kuhakikisha mwalimu lazima awe amehitimu katika Chuo kinachotoa mafunzo, pia bodi itasimamia suala la maadili kwa walimu.

-Bodi ya kitaalamu ya walimu itakuwa na jukumu la kupokea malalamiko, kuchambua na kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya Walimu wachache ambao wamekuwa wakifanya matendo ambayo ni kinyume na maadili ya Ualimu.

-Bodi itatoa fursa kwa walimu kujadili kwa kina masuala yao ya kitaalamu kwa lengo la kuyapatia ufumbuzi.

-Waziri Ndalichako pia amelaani vikali vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu vya kutoa adhabu kwa wanafunzi na ameonya walimu kuacha kumalizia hasira zao kwa wanafunzi.

-Waziri amesema uchapaji  hovyo  wa viboko kwa wanafunzi ni kinyume na taratibu za Wizara, sasa kuwepo kwa Bodi ya kitaalamu itahakikisha inawabana walimu watakaokwenda kinyume na taratibu.

- Waziri amewataka walimu kuacha mara moja tabia za kuchapa wanafunzi hovyo na badala yake wawapende watoto na wahakikishe wanawasidia katika kuwakuza kwenye maadili na malezi yanayokubalika kwenye Taifa.

Jumanne, 4 Septemba 2018

RAIS MAGUFULI AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA CHUO CHA UALIMU MURUTUNGURU


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Magufuli leo ameweka jiwe la msingi kwa ajili ya upanuzi wa Chuo Cha Ualimu Murutunguru, kilichopo Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Rais Magufuli amesema Chuo Cha Murutunguru kwa sasa walimu wanaohitimu ni ngazi ya cheti, lengo la serikali ni kianze kutoa ngazi ya Diploma na baadae kikiongezewa miundombinu kiweze kutoa shahada.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli akiweka Jiwe la Msingi katika Chuo cha Ualimu Murutunguru Wilayani Ukerewe mkoani Mwanza ambapo amewapongeza Viongozi wa Wizara ya Elimu kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo.

Rais Magfuli pia amewapongeza Viongozi wa Wizara ya Elimu kwa kusimamia vizuri miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo.

Pia Rais amewashukuru  washirika wa Maendeleo hususan nchi ya Uingereza kwa kuendelea kufadhili miradi ya Elimu.
Baadhi ya Watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakishuhudia uwekaji wa jiwe la Msingi kwa ajili ya upanuzi wa Chuo cha Ualimu Murutunguru kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza. 

Upanuzi wa ujenzi wa Chuo hicho unahusisha jengo la Utawala, vyumba vya madarasa, bwalo la Chakula, hosteli za wanafunzi, jengo maalumu la kupokelea umeme na ujenzi wa mifumo ya Maji na umeme.
Muda mfupi baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kumpokea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli kwa ajili ya kuweka Jiwe la Msingi la upanuzi wa Chuo cha Ualimu Murutunguru. 

Ujenzi huo utagharimu takriban bilioni mbili nukta Tatu na inatarajia kukamilika oktoba mwaka huu.
Muonekano wa vyumba vya madarasa katika Chuo cha Ualimu Murutunguru, ambapo leo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. John Pombe Magufuli ameweka jiwe la msingi ambalo linahusisha ujenzi wa Jengo la utawala, bwalo la chakula, hosteli za wanafunzi, jengo maalum la kupokelea umeme na ujenzi wa mifumo ya maji na umeme.