Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imevunja mkataba na mkandarasi Herkin Builders anayejenga Chuo
cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo
wilaya ya Ludewa kutokana na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati hali
iliyopelekea kuchelewesha utoaji huduma na kuitia Serikali hasara.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha ametangaza kuvunjwa kwa mkataba huo leo alipofanya
ziara katika eneo la mradi na kukuta hakuna kazi inayoendelea zaidi ya kuchimba
msingi.
"Mkandarasi huyu
amekabidhiwa kazi Novemba 15, 2016 na alitakiwa akabidhi kazi hiyo Septemba
10, 2017 hajakabidhi Serikali ikamuongezea muda mara mbili lakini hata muda
ulioongezwa hakuna atakachofanya, hali halisi inaonekana tunavunja mkataba
huu leo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea taarifa ya
Mradi wa ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo
eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa kutoka kwa Msimamizi wa Mradi Mhandisi
Peter Sizya kutoka VETA Makao Makuu.
Ole Nasha amesema hatambui
tathmini ya Mradi iliyofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi
(VETA) na kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo ndani ya
wiki moja kuunda timu ya wataalamu watakaofanya tathmini ya mradi huo.
"Ninyi VETA ndio mmeendelea
kusisitiza kupewa kandarasi kwa kampuni hii pamoja na kuonyesha udhaifu katika kazi
kadhaa ambazo amewahi kufanya na kuharibu bado ninyi mnafanya tathmini ya mradi
hadi ilipofikia jambo hili halikubaliki na kampuni hii haifai kupewa kazi” alisisitiza
Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha
akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Njombe
kilichopo eneo la Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa kinachojengwa na Mkandarasi
Herkins Builders Limited
Awali Mhandisi wa mradi kutoka VETA makao
makuu Peter Sizya alimweleza Naibu Waziri tathmini iliyofanyika inaonesha kazi
imetekelezwa kwa asilimia 6 ambapo zaidi ya milioni 590 zimetumika kumlipa
mkandarasi.
Gharama za ujenzi wa mradi
wa chuo hicho ni zaidi ya shilingi bilioni 9 na unagharamiwa na Serikali ya
Tanzania kwa kutumia fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
na fedha za ndani.
Muonekano
wa sasa wa hatua ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha mkoa wa Njombe kilichopo eneo la
Shaurimoyo wilaya ya Ludewa.