Jumatano, 3 Oktoba 2018

WIZARA YA ELIMU YAVUNJA MKATABA NA MKANDARASI HERKIN BUILDERS LTD


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imevunja mkataba na mkandarasi Herkin Builders anayejenga Chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa kutokana na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati hali iliyopelekea kuchelewesha utoaji huduma na kuitia Serikali hasara.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametangaza kuvunjwa kwa mkataba huo leo alipofanya ziara katika eneo la mradi na kukuta hakuna kazi inayoendelea zaidi ya kuchimba msingi. 

"Mkandarasi huyu amekabidhiwa kazi Novemba 15, 2016 na alitakiwa akabidhi kazi hiyo Septemba 10, 2017 hajakabidhi Serikali ikamuongezea muda mara mbili lakini hata muda ulioongezwa hakuna atakachofanya, hali halisi inaonekana tunavunja mkataba huu leo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea taarifa ya Mradi wa ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa kutoka kwa Msimamizi wa Mradi Mhandisi Peter Sizya kutoka VETA Makao Makuu.

Ole Nasha amesema hatambui tathmini ya Mradi iliyofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo ndani ya wiki moja kuunda timu ya wataalamu watakaofanya tathmini ya mradi huo.

"Ninyi VETA ndio mmeendelea kusisitiza kupewa kandarasi kwa kampuni hii pamoja na kuonyesha udhaifu katika kazi kadhaa ambazo amewahi kufanya na kuharibu bado ninyi mnafanya tathmini ya mradi hadi ilipofikia jambo hili halikubaliki na kampuni hii haifai kupewa kazi” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.  
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa kinachojengwa na Mkandarasi Herkins Builders Limited

Awali Mhandisi wa mradi kutoka VETA makao makuu Peter Sizya alimweleza Naibu Waziri tathmini iliyofanyika inaonesha kazi imetekelezwa kwa asilimia 6 ambapo zaidi ya milioni 590 zimetumika kumlipa mkandarasi.


Gharama za ujenzi wa mradi wa chuo hicho ni zaidi ya shilingi bilioni 9 na unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kutumia fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na fedha za ndani.
Muonekano wa sasa wa hatua ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni