Ijumaa, 5 Aprili 2019
Jumatatu, 1 Aprili 2019
WAZIRI WA ELIMU AZINDUA UKUMBI WA KISASA WA MIHADHARA CHUO CHA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako
amezindua ukumbi wa mihadhara wa kisasa katika Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere
uliojengwa mapato ya ndani ya Chuo hicho.
Akizundua ukumbi huo wa Mihadhara kigamboni jijini Dar es
salaam Waziri Ndalichako amepongeza Bodi ya Utawala na Uongozi wa Chuo hicho kwa
kusimamia vema matumizi ya fedha zinazotokana na Mapato ya ndani na kutumia kutekeleza
miradi yenye tija kwa Chuo na Taifa kama ilivyofanyika katika ujenzi wa Ukumbi huo
na pia amewataka uongozi kusimamia Dira na Dhima ya uanzishwaji wake kwa kujikita
katika kutoa mafunzo ya Uongozi, Utawala na Maadili.
Waziri Ndalichako amewapongeza Watendaji wa Chuo kwa kusimamia
kwa karibu utekelezaji wa Mradi huo hadi kufikia hatua ya kukamilisha japo kwa kuchelewa
kwa karibu miezi tisa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Ukumbi mpya wa Mihadhara
uliyojengwa katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Kivukoni uliojengwa
kwa kutumia mapato ya ndani ya Chuo hicho.
“ nimefurahishwa na kazi hii nzuri iliyofanyika hapa, kwakweli
ni jengo zuri lenye ubora wa hali ya juu na ambalo litawafanya wanafunzi kuongeza
ari ya kujifunza na ninategemea kuona jengo hili likituzwa vizuri ili litumike kwa
miaka mingi likiwa na ubora uleule”. Amesisitiza Ndalichako
Aidha Ndalichako amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuthamini na kutumia vizuri mapato yake ya ndani
kwa ajili ya kutekeleza mipango na Miradi mbalimbali ya Maendeleo katika taasisi
hizo ili kuleta maendeleo ya haraka badala ya kuzitumia fedha hizo kwa matumizi
mengine yasiyo na tija.
Wakati huo amewataka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambao
ni wakandarasi wa ujenzi wa Ukumbi huo kukamilisha
miradi mingine iliyo chini ya Wizara ya Elimu ikiwemo ukarabati wa shule Kongwe
mfano Kibaha Sekondari, Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea pamoja na ujenzi
wa Hosteli na miundombinu mingine katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.
Nae Mwenyekiti wa Bodi ya Utawala ya Chuo hicho Stephen Wasira,
amesema Chuo hicho kimejipanga kuhahakisha kinatoa elimu bora na wahitimu walio
bora wenye weledi hasa katika eneo la uongozi na utawala ili kuenzi fikra na maono
ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alieanzisha chuo hicho Mwaka 1961
kwa lengo la kuandaa viongozi na watawala.
Awali, Mkuu wa Chuo Prof. Shadrack Mwakalila akitoa taarifa
ya mradi amesema jengo hilo limegharimu zaidi ya Shilingi za Tanzania Bilioni 1.1 na kwamba lina uwezo wa kuchukua wanafunzi 330
kwa wakati mmoja. Ameongeza kuwa pamoja na ukumbi wa Mihadhara jengo hilo lina ofisi
nane za wahadhiri na mifumo ya kisasa ya sauti.
Jumapili, 31 Machi 2019
WIZARA YA ELIMU KUJENGA MAABARA YA FIZIKIA KATIKA SHULE MAALUM YA WASICHANA KISARAWE
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kujenga maabara ya Fizikia katika shule mpya maalum ya wasichana
inayotarajiwa kujengwa katika wilaya ya Kisarawe.
Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya
uchangiaji fedha kwa ajili ya kujenga shule hiyo ambapo Waziri Ndalichako
amesema pamoja na kujenga Maabara pia itatoa vifaa vyote vya maabara hiyo lengo
likiwa kuhamasisha na kuongeza fursa za watoto wa kike kisarawe na kwingine
nchini kusoma masomo ya sayansi.
Akizungumzia hafla ya kuchangia fedha kwa ajili ya
kujenga shule hiyo maalum Waziri Ndalichako ameipongeza wilaya ya Kisarawe kwa
kuja na kampeni ya Tokomeza Zero yenye lengo la kuboresha elimu katika wilaya
hiyo huku mkazo ukiwekwa katika
kumuondolea mtoto wa kike changamoto anazokabiliana nazo wakati wa
kujifunza kwa kuhakikisha anapata mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.
“Mtoto wa kike anapokuwa anatembea umbali mrefu kutoka
shuleni kwenda nyumbani njiani anakutana na majaribu na vishawishi vingi
vinavyokwamisha lengo lake la kupata elimu, kwa hiyo kuamua kujenga shule
maalum kwa ajili ya mtoto wa kike ni uamuzi mzuri kwani itawapa fursa kuweza kukaa na kusoma vizuri
zaidi na hii ni hatua kubwa sana katika kuunga mkono Jitihada zinazofanywa na
Rais wetu” Amesema Ndalichako.
Ndalichako amesemea
tathimini inaonyesha ufaulu kwa ujumla kwa mtoto wa kike uko chini
ukilinganisha na watoto wa kiume kwa hiyo ujio wa shule hii maalum kwa ajili ya
mtoto wa kike ni muhimu kutokana na mazingira wanayoishi ambapo wanaporudi
kutoka shule wanakuwa na majukumu mengi ya nyumbani na kuwanyima muda wa
kujisomea.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo amesema wilaya ya Kisarawe imeweka
mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inapunguza ziro na kuboresha mazingira ya
kujifunzia na kufundishia ikiwemo kuondoa changamoto ambazo zimekuwa
zikikwamisha wanafunzi kujifunza hasa kwa mtoto wa kike.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako, Waziri wa Maliasili na
Utalii na Mbunge wa Viti maalum wa Kisarawe Zainabu Vulu wakifatilia kwa makini
zoezi la wa kuchangia ujenzi wa shule
maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe
“Wilaya ya Kisarawe imekuwa na utaratibu wa kufanya
tathimini kila matokeo yanapotoka ili kuona nafasi ya wilaya katika ufaulu na
kuziangalia changamoto ambazo zinakwamisha faulu na kuziwekea mikakati ili
kuboresha mazingira ya kfundishia na kujifunza ” amesema Waziri Jafo.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Joketi Mwegelo
alimweleza Waziri wa Elimu kuwa lengo la kuanzishwa kwa Kampeni ya Tokomeza
Zero ni kuongeza na kuboresha miundombinu ya shule ili kuifanya kuwa rafiki na
salama kwa utoaji wa elimu.
Mwegelo amesema ujenzi wa shule maalum katika wilaya ya
kisarawe ya uchangia ni moja ya mkakati
mahsusi wa kukabiliana na changamoto zinazowakabili watoto wa kike ili
kuwawezesha kupata muda wa ziada wa kujifunza zaidi.
Shule ya Sekondari maalum inayotarajiwa kujengwa katika
wilaya Kisarawe itachukua wanafunzia wa kidato cha kwanza mpaka cha sita na inakadiriwa
kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja na nusu ambazo zinahusisha ujenzi wa
miundombinu ya mabweni, madarasa, maabara, matundu ya vyoo pamoja na nyumba za
walimu.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Suleiman Jafo kwa pamoja wakipokea mfano wa
hundi ya shilingi milioni kmi iliyolewa na kampuni ya star times kwa ajili ya
ujenzi wa wa shule maalum kwa ajili ya watoto wa kike katika Wilaya ya Kisarawe
NDALICHAKO AZINDUA MAKTABA MTANDAO TAASISI YA ELIMU TANZANIA -TET
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce
Ndalichako amezindua Maktaba Mtandao ya Taasidi ya Elimu Tanzania (TET).
Akizindua Maktaba hiyo jijini Dar es salaam Waziri
Ndalichako amesema itasaidia kupunguza changamoto iliyopo ya usambazaji wa
vitabu kwani mara nyingi vimekuwa vikichelewa kufika katika shule kutokana na
ugumu wa miundombinu ya usafirishaji na kuleta usumbufu katika mchakato wa
ujifunzaji na ufundishaji.
Amesema Serikali imeiona changamoto hiyo na kuanzisha
Maktaba Mtandao kama moja ya njia ya
kurahisisha upatikanaji wa machapisho ya Kiada, Ziada, Mitaala Mhtasari,
Kiongozi cha Mwalimu, Miongozo mbalimbali na Moduli za Kufundishia na
kujifunzia kwa wanafunzi walimu na watumiaji wengine.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akizinduz Maktaba Mtandao ya
Taasisi ya Elimu Tanzania katika uzinduzi wa Maktaba hiyo iliyofanyika
jijini Dar es Salaam
“Kumekuwa na lawama katika suala la usambazaji wa vitabu
kwani havifiki kwa wakati, kawaida mwanafunzi anapaswa kukuta vitabu shuleni
lakini hali ilivyo sasa vitabu vinamkuta mwanafunzi shuleni hii si sawa, hivyo
kuwepo kwa Maktaba Mtandao itasaidia katika kupatikana kwa vitabu mapema na
kurahisisha mchakato wa kujifunza" amesisitiza Waziri Ndalichako.
Wakati huo huo Ndalichako ameiagiza Bodi ya Taasisi ya
Elimu Tanzania(TET) kuhakikisha inasimamia uandaaji wa machapisho ya mitaala,
vitabu na machapisho mengine ili yawe na
ubora.
Ameeleza kuwa pamoja na Bodi hiyo kufanya kazi nzuri ya
kusimamia na kuhakikisha vitabu vinavyochapishwa sasa vinakuwa na ubora lakini
bado inapaswa kongeza umakini kwa sababu suala la uandaaji wa vitabu ni endelevu.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia maonesho ya vitabu
vinavyoandaliwa na Taasisi ya Elimu Tanzania wakati wa uzinduzi wa Maktaba Mtandao jijini Dar es Salaam
Ndalichako amesisitiza kuwa TET ni moyo wa Elimu nchini kwa kuwa ndio inaandaa mitaala, vitabu, miongozo ya shule za msingi na sekondari pamoja na machapisho mbalimbali ya Elimu, hivyo kukiwa na kasoro katika mchapisho hayo watoto wa Kitanzania watakuwa wamefundishwa vitu ambavyo si sahihi na serikali haitavumilia hilo.
Awali Mkurgenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt Aneth
Komba alimweleza Waziri wa Elimu kuwa lengo la kuanzishwa maktaba mtandao hiyo
kurahisisha usambazaji wa machapisho ya Taasisi hiyo katika shule za Serikali,
Binafsi na kwa wadau wengine wa Elimu
Dkt Komba amesema
Maktaba Mtandao iliyozinduliwa inajumuisha vitabu mbalimbali vya kiada
kuanzia ngazi ya Elimu ya awali, msingi na sekondari (kidato cha kwanza mpaka
sita) vinavyochapishwa na taasisi hiyo.
Pia vitakuwepo vitabu vya ziada kutoka
Tanzania na Nchi nyingine.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akicheza na kufurahi na
wanafunzi wa shule ya Fountain Gate wakati wa uzinduzi wa Maktaba Mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania
katika uzinduzi wa Maktaba hiy iliyofanyika jijini Dar es Salaam
Jumanne, 26 Machi 2019
HALMASHAURI ZATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA KUMOTISHA WALIMU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha
zinaweka mikakati ya kuwamotisha walimu wapya wanaoripoti kazini kwa
kuwafikisha katika vituo vyao vya kazi ikiwa ni pamoja na kuwalipa maslahi yao
yote.
Waziri Mkuu ameyasema hayo
jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa sita wa Umoja wa Maafisa
Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA) na kusisitiza kuwa hatua hiyo iende sambamba na kuendelea
kuwatembelea walimu hao katika vituo vyao vya kazi kuwasikiliza, kushauriana na
kupatia ufumbuzi changamoto walizo nazo.
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akifungua Mkutano Mkuu
wa sita wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya
(hawapo pichani) Jijini Dodoma.
|
Amesema walimu hao
wanaporipoti wanakuwa ni wageni katika wilaya hizo hivyo kuwaelekeza tu
kuripoti katika shule walizopangwa haitoshi ni vyema kuweka utaratibu wa kutumia
magari ya Halmashauri kuwafikisha walimu hao katika vituo vyao vipya vya kazi.
“Ninyi Maafisa Elimu
hakikisheni walimu hao wanaporipoti wanalipwa maslahi yao ya msingi, lakini pia
hamasisheni Halmashauri zenu kuwamotisha walimu kwa kuwapa vianzilishi vya
maisha kama ambavyo Wilaya nyingine zinafanya. Wilaya za Mkoa wa Njombe tangu
mwaka 2013 zimekuwa zikitoa motisha kwa walimu wapya wanaoripoti kwa kuwapa kitanda,
godoro, gunia la mahindi, viazi na maharage, hii inamfanya mwalimu kujisikia
yuko nyumbani, muige mfano huu,” aliongeza Waziri Mkuu Majaliwa.
Katika hatua nyingine Mhe.
Majaliwa amewataka Maafisa Elimu hao kutumia mkutano huo kukumbushana wajibu
wao katika kusimamia Elimu na kubadilishana uzoefu na mbinu mbalimbali za
kusimamia elimu ili kuongeza ubora wa elimu hiyo.
“Mkutano huu umekuja kipindi
muafaka kwa sababu matokeo ya upimaji wa Taifa wa ngazi mbalimbali yameshatoka,
wote tunakumbuka upimaji umefanyika kwa mitihani ya darasa la nne, la saba, kidato
cha nne na ile ya kidato cha sita, hii itoe fursa kwenu kujipima na kuona kama hatua
mliyofikia ni nzuri na kama bado ni ya chini basi mbainishe changamoto
zilizopelekea kuwa hivyo na kuweka mipango ya kuboresha,” alisema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Waziri wa
Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka Maafisa Elimu
kusimamia Sera, Miongozo na Taratibu zinazosimamia utoaji wa elimu nchini huku
akiwasihi maafisa hao kutoa taarifa zilizo sahihi kwani wakati mwingine taarifa
zinazotolewa zinatofautiana na zile zinawasilishwa baada ya kufanyika kwa
ukaguzi katika maeneo mnayoyasimamia.
“Wakati mwingine mnatoa
taarifa zisizo sahihi, kwa sababu kaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika zinaonesha kuna baadhi ya
maeneo ambayo bado kuna mrundikano mkubwa wa wanafunzi kati ya 73 hadi 200 kwa
upande wa sekondari na mazingira yanapokuwa katika hali hiyo si rahisi kutoa
elimu bora, hivyo tutoe taarifa zilizo sahihi na taarifa hizi zikiwa sahihi
itasaidia hata wakati wa uchaguzi wa wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza
na kile cha tano,” aliongeza Waziri Ndalichako.
Nae Mwenyekiti wa Umoja wa
Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya Germana Mng’ao ameipongeza Serikali kwa kuboresha
mazingira ya kufundishia na kujifunzia
na kuahidi kufanya kazi kwa bidii katika nafasi yao ya kusimamia Elimu
Tanzania.
Kauli mbiu ya mkutano huo ni
“ELIMU BORA ITATUFIKISHA KATIKA UCHUMI WA KATI IFIKAPO 2025.”
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)