Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli amefurahishwa
na mradi wa ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Mpuguso kilichopo katika Wilaya
ya Rungwe Mkoani Mbeya na ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia kwa mradi huo.
Rais Magufuli
amesema hayo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi
wa majengo mapya na ukarabati katika Chuo hicho kwa lengo la kuboresha na
kuongeza miundo mbinu ili kuongeza nafasi na kuweka mazingira bora ya
ufundishaji na ujifunzaji.
“Niwapongeze
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kukiboresha Chuo hiki ambacho ni cha
zamani kilianza mwaka 1926 ikiwa ni shule ya awali hadi mwaka 1975
kilipobadilishwa kuwa Chuo cha Ualimu na sasa kuna wanafunzi zaidi ya 900,”
amesema Rais Magufuli.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akivuta
utepe pamoja na viongozi wengine kuashiria uwekaji wa jiwe la msingi ujenzi wa
Majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Mpuguso Rungwe mkoani Mbeya.
Katika hatua
nyingine akizungumza na wananchi baada ya uwekaji jiwe la msingi amesema
Serikali yake imeamua kuboresha Vyuo vya Ualimu ili viweze kuandaa walimu bora
na kusisitiza kuwa ajira za waalimu watumishi wengine kwenye sekta ya elimu
zinaendelea kutolewa ambapo zaidi ya watumishi 19,000 wenye sifa wameajiriwa
mwaka huu, huku akiwataka waalimu
wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo na kutembea kifua mbele kwani Serikali
iko pamoja.
Rais Magufuli
pia amewataka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, pamoja na Mkandarasi
anaejenga Chuo hicho kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na kwa ubora
unaolingana na thamani ya fedha ya mradi. Aidha ameagiza Barabara inayoingia
katika Chuo hicho kurekebishwa na baadae kutengewa fedha ili iweze kujengwa kwa
kiwango cha lami.
Awali akitoa
taarifa ya mradi wa Mpuguso, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
Dkt. Leornard Akwilapo amesema unagharimu shilingi Bilioni 9.6 na unahusisha
ujenzi wa vyumba vya madarasa 16, maktaba, maabara 2 za sayansi, kumbi za
mihadhara 2, bwalo la chakula, mabweni 2 ya wanafunzi 154 kila moja na nyumba
za walimu zinazochukua familia 13.
Amesema mradi huo pia unahusisha ukarabati wa nyumba 4 za walimu,
mabweni 2 , vyoo na mabafu7.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli
akiwasalimia wananchi wa Mpuguso Rungwe mkoani Mbeya mara baada ya kuweka jiwe
la msingi msingi ujenzi wa Majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Mpuguso.
Mradi wa Ukarabati na ujenzi wa majengo mapya
katika Vyuo vya Ualimu unagharamiwa na Serikali ya Tanzania na Canada, ambapo
unahusisha vyuo vya ualimu 4 kikiwemo Mpuguso.
Vingine ni Kitangali Mtwara, Shinyanga na Ndala kilichopo Tabora. Kwa
ujumla Mradi huu utagharimu shilingi Bilioni 36.4
Nae Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (Mb)
amepongeza wana Mpuguso kwa kupata mradi
huo mkubwa na kuwaasa kuhahakikisha wanatumia vizuri majengo hayo na kuyatunza.
Hafla hiyo ilihudhuriwa
mamia ya wananchi wa Rungwe na viongozi akiwemo Mhe. Dkt. Tulia Akson Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania, Mhe. Suleiman Jafo(Mb) Waziri
wa TAMISEMI, Mhe. Japhet Hasunga(Mb) Waziri wa Kilimo, Mhe Joseph Kakunda(Mb)
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Mary Mwanjelwa(Mb) Naibu Waziri Utumishi na
Mh Elias Kwandikwa(Mb) Naibu Waziri wa Ujenzi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiimba
pamoja na wananchi waliokusanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Mpuguso
mara baada ya kuwasili chuoni hapo.