Jumapili, 24 Novemba 2019

VYUO BINAFSI VINA MCHANGO MKUBWA KWENYE UTOAJI WA ELIMU YA JUU: PROF. NDALICHAKO

Serikali imesema inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na vyuo binafsi katika kuleta maendeleo ya elimu ya juu kikiwemo Chuo Kikuu cha St. John’s cha hapa nchini.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa Jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s ambapo amesema kuwepo kwa vyuo binafsi hapa nchini kunasaidia na kuwezesha nchi yetu kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaopata mafunzo ya elimu ya juu.

Waziri Ndalichako amesema Chuo hicho kimekuwa kikitoa mchango mkubwa katika utayarishaji wa wataalamu katika fani mbalimbali ikiwemo fani ya ufamasia, uuguzi, ualimu wa Sayansi na Sanaa, kilimo, usimamizi wa fedha, uendeshaji katika utawala, masoko, uhasibu na wataalamu wa maabara.

“Nimeelezwa kuwa tangu chuo hichi kuanza mwaka 2007 hadi hivi sasa kimeweza kutoa wahitimu wasiopuungua elfu kumi na mbili, huu ni mchango mkubwa kwa Taifa letu, hongereni sana,” alisema Prof Ndalichako.


Amewapongeza wahadhiri wa Chuo hicho kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya ya kuwafundisha vijana ambapo amewataka kuendelea kuwaandaa vema wahitimu ili wakawe chachu na mfano wa kuigwa katika jamii wanazokwenda kuishi baada ya kuhitimu masomo yao.

“Nimefurahi kusikia kuwa Chuo hiki pamoja na masuala ya kitaaluma kinatilia mkazo suala la maadili, kinasisitiza umuhimu wa wanachuo kumuheshimu Mungu, kuwa waadilifu, kufanya kazi kwa bidii na kuwa tayari kuhudumia wengine,” aliongeza Prof. Ndalichako.


Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako amesema suala la utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya juu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ili kuhakikisha wanafunzi wote wanaostahili kupata mikopo wanapata na kuwawezesha kusoma bila changamoto yoyote.

“Nimefarijika kusikia kwamba idadi ya wanafunzi wanaopata mikopo katika chuo cha St. John’s imeongezeka na kwamba mikopo hiyo inatoka kwa wakati, na hii niwaambie ukweli ni mpango wa Mhe. Rais. Mtakumbuka wakati akifanya kampeni aliahidi na kueleza namna alivyokuwa akisononeka kuona watoto wa kitanzania, wanafunzi wa elimu ya Juu walivyokuwa wakihangaika kupata fedha za mikopo, hivyo jambo la kwanza aliliolifanya alipoingia madarakani ni kuongeza kiasi cha fedha kinachotolewa kwa ajili ya mikopo kutoka bilioni 341 mwaka 2014/15 na sasa fedha zilizotengwa  kwa mwaka 2019/20 ni sh bilioni 450,” alisema Waziri Ndalichako.




Waziri Ndalichako aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatoa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa wakati akitolea mfano wanafunzi  ambao wameanza masomo mwanzoni mwa mwezi Novemba 2019 Serikali imetoa fedha zao tangu mwezi Septemba.

“Hadi kufikia Oktoba 15, 2019 Serikali ilikuwa imekwishatoa jumla ya sh bilioni 185 sawa na asilimia 41 ya fedha ambazo zimepangwa kwa ajili ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa mwaka 2019/20,” alisema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ametumia fursa hiyo kuviagiza vyuo vyote nchini ambavyo kwa namna moja au nyingine bado havijatoa fedha kwa wanafunzi kutoa fedha hizo kwani Serikali inatoa fedha kwa ajili ya wanafunzi na sio kwa ajili ya vyuo.

Aidha Waziri Ndalichako amewataka wanafunzi wanaohitimu masomo ya elimu ya juu kuwa mabalozi wazuri wa vyuo walivyosoma na Taifa kwa ujumla huku akiwataka kuwa wazalendo na watu ambao wanaweka maslahi ya taifa mbele na kupinga vitendo vya aina yoyote vyenye lengo la kuvuruga amani na mshikamano wa Taifa letu.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha St.John’s, Prof. Yohana Msanjila amesema wanafunzi wanaohitimu katika Chuo hicho kwa mwaka 2019 wako 1,730 huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza idadi ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanaopata mikopo ikiwa ni pamoja na kuwa na usimamizi mzuri wa utoaji mikopo ya elimu ya juu.

“Fedha za wanafunzi na ada zao zinatolewa mapema tofauti na miaka ya nyuma. Nakuomba mgeni rasmi Mhe. Prof. Joyce Ndalichako utufikishie pongezi zetu kwa Mhe. Rais kwamba siku hizi fedha za mikopo na ada za wanafunzi zinafika kwa wakati na hii imesaidia kudumisha utulivu chuoni. Hongera kwa Serikali yetu, hongera Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu,” alisema Prof Msanjila.

Mahafali ya kumi ya Chuo Kikuu cha St. John’s kwa mwaka 2019 yalikuwa na Kauli mbiu isemayo “Udijitalishaji wa Elimu ya Juu kwa Vyuo binafsi: Kiungo Bora kwa Uchumi wa Viwanda.”

Ijumaa, 15 Novemba 2019

TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA KIMATAIFA WA *GIRL*GUIDES*


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi ambayo imejizatiti  na ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba  inaondoa fikra potofu kuhusiana na masuala ya kijinsia.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo jijni Dar e Salaam alipomuwakilisha Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike (Girl Guides) katika masuala ya Uongozi ijulikanayo kama Julitte Low Seminar.

Amesema lengo la semina ni kupanua na kuimarisha ushiriki wa wasichana katika masuala ya girl guides lakini pia kuwawezesha kushirikiana katika masula ya kiutamaduni na uongozi ikiwa ni pamoja na kuwatia moyo wasichana hao ili wazidi kufanya vizuri zaidi katika Jamii wanazotoka.

“Naamini baada ya semina hii ya siku saba wasichana watakuwa na uwezo kushiriki katika masuala ya uongozi na kukemea imani potofu ambazo zinakuwa zikionesha kuwa mwanamke ni kiumbe dhaifu na kutengeneza mtazamo chanya kuwa wanawake ni viumbe kama wanaume na wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko katika ulimwengu huu,”Alisema Prof Ndalichako.

Prof Ndalichako amesema Nchi ya Tanzania inatekeleza mipango inayozingatia usawa wa kijinsia na kuwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanawake na wanaume wana fursa sawa katika maendeleo.

“Mhe Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu asingeweza kupata nafasi aliyo nayo kama nchi ingekuwa bado ina dhana potofu , uwepo wake ktk nafasi ya Makamu wa Rais, viongozi na wataamu  wengine katika nyanja mbalimbali  inaonesha kuwa nchi yetu imepiga hatua katika kuweka usawa wa kijinsia ”aliongeza Prof ndalichako

Amewapongeza Waandaaji wa Semina hiyo kwa kuchagua Tanzania kuwa nchi mwenyeji na kwamba Tanzania ina historia ya kutoa wanawake ambao ni wa nguvu akiwataja viongozi hao kwa uchache  kuwa ni marehemu bibi Titi Mohamed ambaye amekuwa kiongozi wa nchi yetu wakati wa uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Getrude Mongela ambaye alishiriki kwenye mkutano wa Beijing, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Asha-Rose Migiro, Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anna makinda na  sasa Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Nae Mwenyekiti wa Chama cha Girl Guides Taifa Prof Martha Qorro amesema semina  ya mafunzo ya uongozi kwa vijana wa kike (Girl Guides) inafanyika ulimwengu mzima na itasaidia wasichana hao  kujitegemea, kujitambua, kujithamini, kupenda taifa lao kumpenda Mungu kuhesimu wengine na kusaidia mahali popote panapohitaji msaada.

Kwa upande wake mwakilishi wa Bodi ya Dunia katika "World Association of Girl Guide and Girl Scout" kwa kanda ya Afrika  Florentina Mganga amesema semina hii inaendelea ulimwenguni kote na vijana wa kike 700 watapata mafunzo juu wa uongozi  na itawawezesha kujua kuwa mtoto wa kike anaweza kuwa kiongozi wanachotakiwa ni kujiamini.

Semina ya Kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya masula ya uongozi inashirikisha nchi 17 ambazo ni Marekani, Uingereza, Ujerumani  Swizaland, Ghana, Zimbawe, Malawi, Rwanda, Burundi, Kenya, Madagascar, Egypt, Germany,Uganda,  Sierra Leone, Poland, Hong Kong, Philippines na Tanzania ikiwa kama Mwenyeji wao.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako na Prof Martha Qorro ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Girl Guides Taifa wakifurahia ngoma kutoka kwa wanafunzi wa shule ya msingi Diomond (hawapo pichani)wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya masuala ya uongozi inayofanyika jijini Dar es Salaam
Girl Guides kutoka shule ya Msingi Oasis ya jijini Dar es Salaam wakiimba ngonjera mbele ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana hao  iliyofanyika Jijini Dar es Salaam

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa kwenye picha ya pamoja na Girl Guides   wa shule ya msingi Oasisi ya jijini Dar es salaam mara baada ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo vijana wa kike kwenye masuala ya uongozi inayofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya Makamishna na Volunteers wa Girl Guides Tanzania wakipita mbele ya mgeni rasmi (hayupo pichani)wakiwa wameshika bendera za nchi mbalimbali wakati wa ufunguzi wa semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo vijana wa kike juu ya uongozi iitwayo Juliette Low Seminar Jijini Dar es Salaam
Baadhi  ya Girl Guides kutoka nchi mbalimbali wanaoshiriki semina ya kimataifa ya kuwajengea uwezo watoto wa kike juu ya masuala ya uongozi ijulikanayo kama Juliette Low  inayofanyika jijini Dar es Salaam wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa seminia hiyo


Alhamisi, 14 Novemba 2019

ZAIDI YA MILIONI 280 ZATUMIKA KUJENGA NA KUKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE YA MSINGI BUHANGIJA





Serikali kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) imetumia kiasi cha shilingi milioni 286.6 kwa ajili ya kukarabati na kujenga miundombinu katika shule ya msingi Buhangija ya Mkoani Shinyanga.

Akizungumza shuleni hapo Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Selemani Kipanya amesema mwaka 2018 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliipatia shule hiyo fedha hizo kwa ajili ya kujenga vyumba vinne vya madarasa, mabweni mawili na matundu 18  ya vyoo.

"Majengo haya yamesaidia sana kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani na vyooni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundushia na kujifunzia," amesema Mwalimu Kipanya.

Mwalimu Kipanya amesema shule hiyo ambayo ni jumuishi ina jumla ya wanafunzi 1,052 ambapo kati yao 230 ni wenye mahitaji maalum na kwamba wanafunzi hao wenye mahitaji maalum wanaishi bweni wakati wengine wanasoma kutwa.

Naye Mwalimu Mohamed Makana ameishukuru serikali kwa kuikumbuka shule hiyo ambayo ilikuwa na changamoto nyingi za miundombinu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia hasa kwa upande wa wanafunzi wenye mahitaji maalum.

Mwalimu Makana amesema shule hiyo imepatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya kutosha kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum ikiwemo kofia pamoja na miwani kwa ajili ya watoto wenye ualbino.

Mwanafunzi Jesca Michael mwenye ualbino ameishukuru Serikali kwa kuwalinda pamoja na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia huku akiiomba serikali kuendelea kuwaangalia kwa ukaribu wanafunzi wenye mahitaji maalum ili nao waendelee kupata elimu bora.


Darasa lililojumuisha watoto wenye mahitaji maalum na wale wa kawaida katika shule ya msingi Buhangija



Baadhi ya miundombinu iliyojengwa na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R) katika shule ya msingi Buhangija iyopo mkoani Shinyanga 
Mtoto mwenye ulemavu wa kutokuona akitumia kifaa maalum kwa ajili ya kuandikia katika shule ya msingi Buhingili. Kifaa hicho ni moja ya vifaa vilivyonunuliwa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum .


ZAIDI YA MILIONI 280 ZATUMIKA KUJENGA NA KUKARABATI MIUNDOMBINU YA SHULE...