Jumapili, 27 Oktoba 2019

WIZARA YA ELIMU YAPONGEZWA KWA KUREJESHA MASHINDANO YA UMISAVUTA


Serikali imeipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutekeleza agizo la kurudisha mashindano ya Michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu (UMISAVUTA) huku ikiitaka kuhakikisha kuwa michezo na Sanaa vinapewa kipaumbele katika mipango endelevu ya Wizara.

Pongezi hizo zimetolewa Mkoani Mtwara. na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Mjaliwa wakati wa ufunguzi wa mashindano ya UMISAVUTA.
Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akipiga mpira kuashiria uzinduzi rasmi wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini katika viwanja vya Nangwada Sijaona mkoani Mtwara.

Dkt. Mwakyembe amesema eneo la michezo na Sanaa ni sehemu muhimu katika makuuzi ya watoto kwani yanajenga na kuimarisha afya ya mwanadamu lakini pia yanaimarisha mahusiano baina ya raia.

“Kwa sasa nchi imeonesha mafanikio makubwa katika michezo hivyo ili Taifa lipate wataalamu na vipaji sahihi katika michezo na Sanaa hatuna budi kuanza ngazi za awali za elimu, “alisema Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. leonard Akwilapo amesema Wizara imejipanga vyema katika kuendeleza michezo ili kuongeza furaha kwa wananchi wa Tanzania kwa kuziona timu zinashiriki na kushinda mashindano makubwa ya kimataifa.

“Kama Wizara tunasema muda wa kushiriki sasa umetosha tunataka kuwa washindani na mashindano haya ni sehemu ya maandalizi ya kutekeleza azma hiyo,” alisema Katibu mkuu Akwilapo.
Mgeni rasmi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe akisalimiana  na washiriki wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo mkoani Mtwara.

Katibu Mkuu Akwilapo alisema kupitia mashindano haya washiriki wataongeza ujuzi  katika michezo na kuwa walimu ambao wataimarisha michezo wakati watakapokuwa kazini huku wengine wakiendeleza vipaji vyao na kuwa hazina ya Taifa kwa siku za usoni.

Michezo inayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa Pete, mpira wa miguu, wavu kikapu, riadha, mashindano ya uchoraji, Sanaa za maonesho, ngoma pamoja na kwaya. Mingine ni pamoja na ile ya kutengeneza zana za kufundishia na kujifunzia kwa lengo la kumjengea mwalimu umahiri wa kuandaa na kutumia zana nzuri za kufundishia.
Baadhi ya Walimu Tarajali wakiingia  katika uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini mapema hii leo mkoani Mtwara.

Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi kutoka Seksheni ya Mafunzo ya Ualimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Agusta Lupokela amesema mashindano hayo yaliyoanza Oktoba 25, 2019 yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 31, 2019 na yameshirikisha Kanda saba ambazo ni Kanda ya Kati, Kusini, Mashariki, Magharibi, Kanda ya Ziwa, Kaskazini na Kusini ambazo zimeundwa kulingana na vyuo vya ualimu.

Juni 10, 2019 katika Viwanja vya Nagwanda Sijaona mkoani Mtwara wakati Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafungua mashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA alitoa agizo kwa Wizara ya Elimu kuhakikisha kuwa mashindano ya michezo na Sanaa kwa Vyuo vya Ualimu yanarejeshwa.
Baadhi ya Walimu Tarajali wakiandamana kuelekea katika uwanja wa Nangwanda mkoani Mtwara wakati wa ufunguzi wa mashindano ya michezo na sanaa kwa vyuo vya ualimu nchini mapema hii leo mkoani Mtwara.

Alhamisi, 17 Oktoba 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA MKUU WA SHULE KASANGEZI KUHAMISHWA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako ametilia shaka matumizi ya fedha za serikali zaidi ya shilingi milioni mia tano zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa shule ya sekondari Kasangezi iliyopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Akizungumza mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo waziri Ndalichako amesema shule hiyo imepatiwa zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 4, mabweni 4 yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 katika kila moja, matundu ya vyoo 10, bwalo pamoja na ukarabati wa maabara.

Ndalichako amesema  kazi iliyofanyika haiendani na fedha iliyotolewa kutokana na miundombinu hiyo kujengwa chini ya Kiwango.

“Milango ya madarasa na hata ya mabweni mmetengeneza kwa mbao laini tofauti na BOQ pamoja na kuwa laini ina uwazi hii nataka itolewe, tazama sakafu imeshaharibika hapa hata mwaka haujaisha mabweni mliambiwa ya watu themanini mmejenga ya watu sitini"
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia mlango wa darasa ambao umetengenezwa kwa mbao laini kinyume cha taratibu katika shule ya sekondari Kasangezi

Kufuatia hali hiyo ndalichako ameagiza kuwa ujenzi wa mabweni urudiwe kwa kuzingatia BoQ na ameaguza ujenzi huo uwe umekamilika ifikapo desemba.

"Nitakuja mwenyewe mwezi wa kwanza kukagua kama hayo yatakuwa hayajatekelezwa mengine yatafuata,” amesema waziri Ndalichako.

Aidha waziri Ndalichako amemuagiza  Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kasulu Mhandisi  Godfrey Kasekenya  kumuondoa  mara moja shuleni hapo mkuu wa shule hiyo kwa kushindwa kusimamia  vizuri kazi hiyo na hivyo kuisababishia hasara serikali.

“Kwanza ujenzi wa mara ya kwanza hata matofali hukununua ulichukua kwenye benki ya wananchi na tayari nilikuwa nimeleta fedha sasa kwanini hukujiongeza hata ukarekebisha ofisi ya Mkuu wa Shule ambayo iko katika hali isiyoridhisha vitu vingine ni kudhalilisha Serikali, Mkurugenzi muahamishe huyu katika shule hii,” alisema waziri Ndalichako.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako akikagua maendeleo ya  ujenzi wa moja ya bweni katika shule ya sekondari Kasangezi iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri Ndalichako pia ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na  Rushwa (TAKUKURU) wilayani Kasulu   kufuatilia muenendo wa upatikanaji wa madawati miamoja themanini yaliyonunuliwa katika mradi huo kama yametimia na yamenunuliwa kwa kufuata utaratibu.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange amekiri kuwepo uzembe katika kusimamia miradi hiyo na kumuhakikishia waziri Ndalichako kuwa ofisi yake itafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa katika ziara hiyo.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolijia Prof. Joyce Ndalichako yupo mkoani Kigoma Kwa ziara ya Kikazi akikagua miradi ya elimu inatekelezwa kupitia fedha za Programu ya lipa kwa matokeo EP4R.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mlago wa darasa ambao umetumia mbao laini tofauti na maelekezo katika shule ya sekondari Kasangezi.

Jumatano, 16 Oktoba 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATOA SIKU 15 KWA MSHAURI ELEKEZI BICO KUFANYA TATHMINI YA GHARAMA ZA UJENZI CHUO CHA UALIMU KABANGA


Wakati Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga kilichopo Wilayani Kasulu  mkoani Kigoma ukiendelea kwa kusuasua Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku 15 kwa Mshauri Elekezi BICO  kupitia upya gharama za ujenzi wa mradi huo ambazo ni  zaidi ya shilingi bilioni kumi  ili kujiridhisha kama fedha hiyo inaendana na ukubwa wa mradi.

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi huo ambapo pamoja na kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi ametilia shaka gharama ya  ujenzi ambayo ni zaidi ya shilingi bilioni kumi kutumika ndivyo sivyo kutokana na aina ya majengo yanayojengwa katika chuo hicho kuwa ya thamani ndogo.

"Hivi ni vighorofa mtoto na narudia ni vighorofa mtoto huwezi kuniambia kwamba majengo haya ambayo kwanza ni machache, pili siyo ghorofa zile kubwa kama tulizojenga katika miradi mingine tena kwa gharama ndogo ya shilingi bilioni sita zinazidiwa na vighorofa hivi hapa kuna kitu hakipo sawa nataka ndani ya siku kumi na tano gharama za mradi zipitiwe upya kwa kila jengo na nipewe taarifa vinginevyo mratibu wa miradi hii utafute kazi nyingine," alisema Prof. Ndalichako.
Injinia wa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga akimuonesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako namna chuo cha Ualimu Kabanga kitakavyoonekana baada ya ujenzi kukamilika

Kuhusu kusuasua kwa Mradi Waziri Ndalichako amemtaka Mkandarasi huyo ambaye ni Kampuni ya SUMA JKT kuongeza kasi ya kufanya kazi akisisitiza ziletwe mashine za kisasa ambazo zitarahisisha kazi pamoja na kuongeza vibarua kwenye eneo la kazi.

"Huwezi kutekeleza mradi wa zaidi ya shilingi bilioni kumi kama nyumba yako unayojenga, yaani una kamashine kamoja tena kakusukuma,vibarua wenyewe inaonekana umewaleta leo baada ya kusikia nakuja kukagua, hii haikubaliki tunataka kazi ifanyike usiku na mchana kwa sababu pesa zipo lazima mradi ukamilike haraka," alisema Waziri  Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ualimu, Kabanga unaojengwa na Wizara kupitia Mradi wa TESP wilayani Kasulu mkoani Kigoma

Mapema akitoa  taarifa  ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Ujenzi SUMA JKT, Luteni Kanali Onesmo Njau amesema mpaka sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia thelathini na kudai kukabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo  usumbufu wa kupata vifaa vya ujenzi kama saruji na mchanga.

"Mheshimiwa Waziri tulikuwa tukitegemea kupata saruji kwa kampuni ya Dangote lakini kwa sasa inabidi tufuate wenyewe Dodoma na hivyo kutumia muda mwingi kusubiri vifaa vifike kwenye eneo la mradi," alisema Kanali Njau.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa Chuo cha Ualimu Kabanga Kasulu Mkoani Kigoma

Naye mshauri elekezi wa mradi huo kutoka BICO, Fred Munishi amekiri kuwa kazi inasuasua na kusema kuwa tayari ametoa maelekezo kwa Mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi taarifa ambayo hata hivyo imeonekana kukinzana na taarifa ya Mkandarasi na hivyo kutakiwa kufanya kazi kwa karibu na Mkandarasi.

"Inaonekana hapa hakuna maelewano mazuri baina ya Mkandarasi na mshauri elekezi, sitaki mivutano kazini kaeni pamoja fanyeni kazi ya serikali na mkiendelea hivi tutawaondoa," alisema Waziri Ndalichako.

Akiwa katika Halmashauri ya wilaya ya Kasulu, Waziri Ndalichako pia amekagua miradi mingine minne ya elimu katika shule za sekondari na msingi za Kigodya, Ruhita, Nyantare  na Kasyenene na kueleza kuridhishwa na kazi huku akisisitiza kuwa serikali inatoa fedha ili kuona matokeo.

Katika ziara hiyo Waziri Ndalichako aliambatana pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Dkt. AveMaria Semakafu pamoja na Mratibu wa Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo pamoja na ule wa TESP.
Muonekano wa sasa wa hatua ya ujenzi wa baadhi ya majengo katika eneo la mradi wa Chuo cha Ualimu Kabanga wilani Kasulu Mkoani Kigoma

UKARABATI CHUO CHA MZUMBE NA MIAKA 20 BILA MWALIMU NYERERE

USIMAMIZI MBOVU WA MIRADI YA ELIMU BUHIGWE WAMKERA WAZIRI NDALICHAKO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameonesha kukerwa na usimamizi mbovu wa miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara anayoisimamia, Dkt. Leonard Akwilapo kuleta wataalamu watakaofanya ukaguzi maalum wa utekelezaji wa miradi ya elimu katika wilaya hiyo.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo  Wilayani Buhigwe mkoani Kigoma mara baada ya kukagua baadhi ya  miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)na kubaini uwepo wa kasoro kadhaa ikiwemo matumizi ya vifaa vya ujenzi vilivyo chini ya Kiwango na  majengo ya shule ya Msingi ya mfano Bwega  kutofautiana na ramani iliyopendekezwa na wizara.

"Kwa ujumla usimamizi wa Miradi katika wilaya ya Buhigwe  siyo mzuri, maafisa elimu hawawajibiki katika kuangalia kazi zao, unakuta kazi zimefanyika hovyo, watu hawafuatilii," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia akikagua moja ya nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Kasumo iliyoko wilayani Buhigwe mkoani Kigoma

Waziri Ndalichako amesema Mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe hatimizi wajibu wake ipasavyo kwa kuwa ameshindwa kusimamia miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa na kuruhusu matumizi ya vifaa vya ujenzi visivyo na ubora lakini pia ameshindwa kufuata ramani  katika ujenzi wa majengo ya shule ya msingi ya mfano inayojengwa wilayani humo.

Kiongozi huyo amesema tayari  amewasiliana na Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt. Leonard Akwilapo ili ufanyike ukaguzi wa kina katika miradi ya elimu  Wilaya ya Buhigwe lengo likiwa ni kubaini mapungufu na iwapo kuna mtu kafanya uzembe kwa manufaa yake awajibike.

"Inabidi kabla ya kuleta fedha nyingine za miradi ya elimu wilayani Buhigwe ije timu ya watalaamu mainjinia wachunguze walinganishe BoQ na kilichofanyika, haiwezekani turuhusu uzembe kama huu kuendelea kwenye miradi inayotumia fedha ya wananchi wanyonge," aliongeza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akionesha dosari kwenye jengo la maabara la shule ya sekondari Janda wakati akikagua miradi ya elimu inayotekelezwa katika shule hiyo na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R)

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayanalina amemshukuru Waziri Ndalichako kwa ziara yake wilayani humo na kusema kuwa  mapungufu yote yaliyobainika tayari  Kamati yake imeyatolea maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na kwamba zoezi linaloendelea ni kuwachukulia hatua wahusika.

"Kamati ya Usalama ya wilaya ilibaini mapungufu katika miradi mbalimbali na tulitoa maelekezo kupitia kwa  Mkurugenzi na vyombo vyetu vilishaagizwa kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki," amesema Mkuu wa Wilaya hiyo, Ngayalina.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa maabara unaoendelea katika shule ya sekondari Janda iliyoko Buhigwe Mkoani Kigoma

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Anosta Nyamoga amesema ofisi yake tayari imemfukuza kazi fundi aliyekuwa na mkataba wa kufanya ukarabati na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Sekondari Janda kutokana na kufanya kazi hiyo chini ya viwango na kuahidi kuzifanyia kazi kasoro zote ambazo zimebainishwa na Waziri Ndalichako.

Akiwa wilayani Buhigwe Waziri Ndalichako amekagua miradi ya elimu katika shule ya msingi Bwega, shule ya sekondari Janda,  shule ya sekondari Muyama na shule ya msingi Kasumo ambayo kwa pamoja inatarajia kugharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

Waziri Ndalichako yuko Mkoani Kigoma kwa ziara ya kikazi kukagua miradi ya Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe na Halmashauri ya Mji Kasulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua moja ya dawati lililoko katika Shule ya Sekondari Muyama mara baada ya kukagua ujenzi wa darasa hilo