Alhamisi, 15 Machi 2018

Maafisa Habari wa Serikali watoa msaada kwa Shule ya Laibon


Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali Leo wamekabidhi msaada wa Vitabu, Madaftari, kalamu na Matanki mawili ya kuhifadhia maji katika Shule ya Msingi Laibon iliyopo mkoani ARUSHA.

Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa Chama Cha Maafisa hao- TAGCO, Pascal Shelutete amesema lengo ni kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali za kutoa Elimu bure.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Rashid Njarita ameshukuru kupokea msaada huo ambapo amesema matanki ya maji yataondoa changamoto ya maji iliyokuwepo shuleni hapo.

Msaada uliotolewa unathamani ya shilingi milioni mbili na laki tano.

Mwenyekiti wa Chama Cha Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano wa Serikali - TAGCO, Pascal Shelutete akimkabidhi Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Laibon Rashid Njarita Madaftari kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo.
Maafisa hao wa Mawasiliano wanashiriki kikao kazi ambacho kinalenga kujengeana uwezo wa namna bora ya kutangaza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.


Kikao hicho kimeanza Machi 12 na kitamaliza Machi 16, 2018 huku kauli mbiu ya mkutano huo inasema Je? Mawasiliano ya kimkakati yanachagiza Vipi Tanzania ya Viwanda.

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Dk. Hassan Abass akimkabidhi daftari mmoja wa wanafunzi wa shule ya Msingi Laibon iliyopo mkoani Arusha.



Ijumaa, 9 Machi 2018

Naibu Waziri Ole Nasha asisitiza uadilifu na utunzaji wa siri za ofisi.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha amewataka watumishi wapya wa Wizara hiyo kuwa waadilifu katika utendaji kazi pamoja na kutunza siri katika maeneo wanayofanyia kazi.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa rai hiyo mjini Dodoma wakati wa akifunga mafunzo kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo, mafunzo ambayo yamelenga kuwakumbusha taratibu, sheria na miongozo ya kazi inayotakiwa katika utumishi wa umma.

Naibu Waziri huyo amesema anaamini mafunzo yaliyotolewa yatawawezesha kuwa watumishi bora wa umma ambao wanafahamu vema mipaka ya kazi, taratibu za kiutumishi lakini pia haki na wajibu katika utendaji kazi.

Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, Mhe.William Ole Nasha akifunga mafunzo ya watumishi wapya wa Wizara hiyo ambapo amewataka kuzingatia maadili ya Utumishi wa Umma,ikiwa ni pamoja na kutunza Siri za ofisi.

Pamoja na mambo mengine Naibu Waziri Ole Nasha amemuagiza Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara hiyo Moshi Kabengwe kuandaa utaratibu wa mafunzo kwa watumishi wengine wa Wizara hiyo ili kuwakumbusha taratibu, kanuni na miongozo kwa lengo la kuepuka ukiukaji wa maadili na pia kuleta chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi miongoni mwa watumishi.


Nae mmoja wa watumishi aliyeshiriki mafunzo hayo Lazaro Julius kutoka Ofisi ya Kamishna wa Elimu wa Wizara hiyo amesema mafunzo hayo ni muongozo thabiti katika kutekeleza majukumu ya kazi za kila siku katika utumishi wa umma ambapo ameahidi kuzingatia na kutekeleza yote yaliyoelekezwa.

Mafunzo  kwa waajiriwa wapya wa Wizara hiyo yamefanyika kwa siku Nne kuanzia Machi 6, na yameshirikisha waajiriwa wapya kutoka wizara ya Elimu Makao Makuu na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo.

Watumishi wapya wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia wakifuatilia mafunzo Maalumu ya namna wanavyotakiwa kutekeleza majukumu yao katika Utumishi wa Umma ambayo yamefanyika mkoani Dodoma.


Ole Nasha apiga  marufuku Wanafunzi wa Shule kunyimwa vyeti kwa kutokamilisha michango
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amepiga Marufuku Wanafunzi kunyimwa vyeti pindi wanapomaliza shule kwa madai ya kutokamilisha michango pindi walipokuwa wanasoma.

 Naibu Waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Tabora alipokutana na Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kuzungumzia namna ambavyo wanapaswa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John PombeMagufuli la kukataza michango shuleni kwa kuwa Serikali inagharamia ElimuMsingi.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha akikagua Vifaa vyama Maabara katika Chuo cha UalimuTabora kilichopo Manispaa ya Tabora Mkoani humo.

Naibu Waziri huyo amesema Magufuli hajakataza uchangiaji wahiari isipokuwa amekataza michango holela ambayo ilikuwa ikichangishwa bila utaratibu na kumzuia Mwanafunzi kuendelea na masomo kwa madai kuwa hajachanga mchango wa aina fulani.

 ‘Waraka wa Elimu Namba 6 wa mwaka 2016 unaeleza wazi namna Elimu bila malipo itakavyotekelezwa na nijukumu la mzazi kwa mtoto wake hivyo ni marufuku Mwanafunzi kubakizwa nyumbani au kutopewa cheti chake anapomaliza Shule kwa madai kuwa hajakamilisha mchango fulani’.amesema Ole Nasha

Pia ametoa rai kwa walimu wote nchini kujielekeza kwenye jukumu lao la msingi la kufundisha badala ya kujihusisha na uchangishaji wa mchango wa aina yoyote na kwamba michango yote ya hiari itaratibiwa na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri husika kupitia watendaji wake.

Ndalichako awataka Wanawake kufanya kazi kwa bidii


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewataka Wanawake nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuonyesha Thamani ya Mwanamke katika jamii na Taifa kwa ujumla.

 Waziri Ndalichako amesema bidii pekee katika shughuli mbalimbali za kujiletea Maendeleo kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla ndiyo itaonyesha mchango wa Mwanamke na kumfanya athaminiwe na kumuwezesha kupata nafasi kubwa na nzuri zaidi za kutumikia Taifa ikiwa ni pamoja na kufuta dhana potofu ya kuwa Mwanamke hawezi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Jukwaa la Akademia katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani shughuli ambayo  imefanyika jijini Dar es salaam.

Waziri Ndalichako amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na  Taasisi ya Akademia ya Sayansi Tanzania walati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ili kujadili mchango wa Mwanamke katika kuleta Maendeleo Endelevu ambalo limeshirikisha Wanawake na Wadau wengine kutoka nchi mbalimbali.

Kwa upande wake Spika Mstaafu Anne Makinda amesema wanawake wanapaswa kuhakikisha wanapata Elimu ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuwa na uthubutu wa kufanya shughuli ambazo wanaamini watazifanya kwa umakini ili kuonyesha uwezo walionao katika jamii inayowazunguka.

Jumatano, 7 Machi 2018

Mloganzila yapokea msaada wa Dawa


Serikali ya Korea leo imeikabidhi  msaada wa dawa  zenye thamani ya Shilingi Milioni Mia Moja kwa Serikali ya Tanzania ikiwa ni ishara ya mahusiano mazuri kati ya nchi hizo mbili.
Msaada huo umekabidhiwa kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Profesa Joyce Ndalichako jijini Dar es Salaam ili zitumike katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi ya Tiba Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Mloganzila.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa pamoja na Wajumbe wa Kamati za Bunge la Jamhuri ya Watu wa Korea wakisalimiana  na Wagonjwa katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Mlongazila jijini Dar es Salaam mara baada ya Korea kutoa msaada wa  kwa ajili ya Hospitali hiyo.

Mara baada ya kupokea msaada huo Waziri Ndalichako ameishukuru Serikali ya Korea kwa msaada huo na kuwataka wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho kutumia vema miundombinu ya Chuo kwa  kujifunzia na kufundishia ili kujijenga kitaaluma kwalengo la  kumaliza tatizo la uhaba wa Madaktari na Wataalam wa Afya hapa nchini.
Kiongozi wa Ujumbe wa  Kamati za Bunge la Jamhuri ya Watu wa Korea  Jun Hey Sook akimkabidhi rasmi Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako  msaada wa dawa uliotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya Chuo cha Taaluma na Tiba cha MLOGANZILA kilichopo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya makabidhiano ya dawa hizo Kiongozi wa Ujumbe wa Korea  wa Kamati ya Afya na Huduma za Jamii ya Bunge la nchi hiyo, Jun Hey Sook amesema msaada huo wa dawa ni ushirikiano katika kuboresha sekta ya Afya.

Serikali imesema haitasita kuvunja mkataba na Kampuni ya Skywards Construction


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa  Wiliam Ole Nasha, amesema Serikali haitasita kuvunja Mkataba na Kampuni ya Skywards Construction inayopaswa kujenga miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji katika Chuo cha Ualimu Ndala kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.

Naibu Waziri ametoa Kauli hiyo baada ya Kampuni ya Skyward Construction  iliyopaswa kujenga Mabweni, Vyumba vya Madarasa, Ukumbi, Maktaba, Maabara na Matundu ya vyoo kutoonekana katika eneo la ujenzi tangu alipokabidhiwa kutekeleza mradi huo mapema mwezi Januari 27, 2018.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa  William Ole Nasha akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Jacob Mtalitinya juu ya changamato zinazoikabili Shule ya Sekondari Kampala katika kukamilisha ujenzi wa Miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji.

Akizungumza akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa Miradi inayotekelezwa na Wizara yake kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matoke- EP4R, Naibu Waziri  Ole Nasha amesema Kampuni hiyo tangu ikabidhiwe Mradi haijawahi kufika eneo la mradi kuanza ujenzi na bila taarifa yoyote hivyo kuacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
‘Kampuni hii ilipaswa kuanza kazi Februari 24, 2018 cha kushangaza hadi sasa haijaonekana eneo la Mradi bila taarifa yoyote. Kampuni hii ya Skyward Constuction inapaswa kujua imeingia mkataba na mikataba hii huwa ina taratibu zake, kama kuna jambo haliendi sawa ni bora akaeleza kwa kuwa Serikali haitasita kuvunja mkataba nae.’ Alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.

Naibu Waziri Ole Nasha amezitaka Kampuni mbalimbali za ujenzi  kuhakikisha zinazingatia Mikataba, kwani kuchelewa kukabidhi Mradi kwa wakati  kunaisababishia Serikali gharama zisizo za lazima kwa kuwa vifaa vya ujenzi vitapanda bei lakini pia Mradi kushindwa kukidhi kusudio la kuwepo kwa wakati huo.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Ndala Abinego Ndikumwe amesema pamoja na Serikali kukarabati na kujenga miundombinu ya ujifunzaji na ufundishaji bado Chuo hicho kina changamoto za upatikanaji wa Maji, ukosefu wa  usafiri kwa matumizi ya Chuo, Bwalo na ofisi za Wafanyakazi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akikagua ujenzi wa Miundombinu ya  Shule ya Sekondari Mwanzoli, iliyojengwa na Wizara hiyo kupitia Progamu ya Lipa kulingana na Matokeo, EP4R ambapo mara baada ya ukaguzi huo Naibu Waziri amekiri kuridhishwa na ukarabati huo na kuzitaka shule nyingine kuuga mfano huo.

Akiwa Wilayani Nzega Mhe. Ole Nasha ametemtembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzega na Mwanhala, Shule ya Sekondari Kampala na Shule ya Sekondari Mwanhala ambapo akiwa kwenye Shule ya Sekondari Mwanzoli na amekiri kurdhishwa na namna Shule hiyo ilivyotekeleza mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule, ambapo ameahidi Wizara yake itahakikisha inakamilisha ujenzi wa Maabara, na  Nyumba mbili za Walimu.

Jumatatu, 5 Machi 2018

Naibu Waziri Ole Nasha: Sijaridhishwa na ukarabati uliofanyika Butimba


Naibu Waziri wa  Wizara ya  Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ameitaka Wizara yake kufanya uchunguzi na kutoa ripoti ya namna ukarabati wa Miundombinu ulivyofanyika katika Chuo cha Ualimu Butimba ili kujiridhisha kama kweli ukarabati huo unaakisi kiasi cha fedha zilizotolewa.

Naibu Waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo Mjini Mwanza baada ya kufanya ziara katika chuo hicho hapo  ambapo amesema hajaridhishwa na ukarabati ulivyofanyika kwa kuwa Chuo hicho kilipatiwa kiasi cha takribani  Milioni Mia Nane Sitini na Tatu.    


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akikagua moja ya Bweni la Wanafunzi katika Chuo cha Ualimu Butimba lililofanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).

Ole Nasha  amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha Vyuo vya Ualimu vinakuwa na mazingira mazuri ya kuwaandaa Walimu wanaokwenda kufundisha katika shule mbalimbali  hapa nchini hivyo ni jukumu la  Wakuu wa Taasisi na Vyuo vya Elimu kuhakikisha wanasimaia Miradi mbalimbali ya Elimu kwa ukamilifu  na kuwa Serikali haitasita kuchua hatua kwa yeyote atakayeshindwa kusimamia Miradi hiyo kwa weledi.

“Chuo hiki kimepatiwa takribani Milioni Mia Nane Sitini na Tatu kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu kama hivi ndivyo ukarabati uliofanyika hauonyeshi thamani ya fedha iliyotolewa kwa ajili ya Chuo hiki cha Ualimu Butimba, kwa kweli Sijaridhishwa”alisisitiza Naibu Waziri huyo.

Akitoa maelezo Mkuu wa Chuo hicho John Ole Meiludie amejitetea kuwa kazi hiyo ya ukarabati imefanyika kwa umakini isipokuwa wanafunzi wenyewe  ndiyo wanachana nyavu za madirisha lakini pia hali ya mvua zinaponyesha huondoa  rangi ambayo  inakuwa imepakwa katika majengo ya Chuo hicho.


1.      Naibu Waziri wa Elimu akipokea maelezo katika maabara ya baiolojia Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole akipokea maelezo kutoka kwa Mkufunzi Ramadhani Wenge kuhusiana na maabara ya Bailojia iliyopo katika Chuo cha Ualimu Butimba Mkoani Mwanza.


Akiwa Mkoani Mwanza Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea Shule ya Sekondari Nyegezi iliyoko Wilaya ya Nyamagana na Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma VETA kilichopo wilaya ya Ilemela na kuridhishwa na namna walivyotekeleza miradi ya Elimu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha akiongea na Wanafunzi wa Shule ya sekondari Nyegezi Iliyopo Mkoani Mwanza alipofanya ziara shuleni hapo kukagua miradi inayotekelezwa na Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).