Ijumaa, 6 Julai 2018

DK. SEMAKAFU ASEMA HAKUNA ATAKAESALIMIKA MATUMIZI YA FORCE AKAUNTI


Serikali imesema haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakayekiuka utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika kutekeleza shughuli za ujenzi na ukarabati kwenye Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDC’S).

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Dk. Avemaria Semakafu  mjini Morogoro wakati wa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wakuu wa vyuo, maboharia na wahasibu kuhusu utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika shughuli za ujenzi na ukarabati katika vyuo vya FDCs.
kuwa upo kisheria na kwa yeyote atakaepindisha utaratibu huo atawajibika kwa hilo. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo ya matumizi ya utaratibu wa Force Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kuhakikisha wanafuata utaratibu huo.
Alisema utaratibu huo uko kisheria na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha kupata taaluma ya kutumia utaratibu huo  ambapo amewataka washiriki hao kwenda kutumia taaluma hiyo kama nyenzo kuleta mabadiliko wakati wa kutekeleza miradi katika maeneo yao.


 “Ni muhimu kwa Wakuu wa Vyuo na wote mtakaohusika katika shughuli za ujenzi na ukarabati kuhakikisha mnafuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa kuwa hakuna atakaesalimika kwa kuvunja sheria hizi,” alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo  Dk Semakafu.


Wajumbe wa Kikao wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu wakati wa kufunga mafunzo ya matumizi ya Force Account kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na Wahasibu yaliyofanyika mjini Morogoro.
Amesema Vyuo vya maendeleo ya Wananchi vilianzishwa kwa malengo mahususi ikiwa ni pamoja na kutoa stadi na mafunzo kwa wananchi hivyo miradi hiyo ikikamilika kwa wakati vyuo vitaweza kutimiza malengo yake lakini pia thamani halisi ya matumizi ya fedha (Value for Money) za ujenzi na ukarabati zitaonekana.

Mafunzo hayo ya utaratibu wa kutumia Force Akaunti yameshirikisha wajumbe kutoka Vyuo vya maenedeleo ya wananchi 11 na yameendeshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya  mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Ajira (ESPJ).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya namna ya kutumia force Akaunti yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jumatano, 4 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AIELEKEZA COSTECH KUPELEKEA MIONGOZO YA KUSAIDIA WABUNIFU KWENYE HALMASHAURI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce NDALICHAKO ameitaka Tume ya Taifa ya Sayansi naTeknolojia, COSTECH -kuhakikisha miongozo yote ya namna yakuwasaidia wabunifu inapelekwa  katika ngazi ya Halmashauri ili kuwezesha kupatikana kwa bunifu zitakazosaidia nchi kufikia uchumi wa viwanda.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo katika kongamano la  sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na ubunifu linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wanasayansi na wavunifu katika kongamano la sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika jijini Dar es Salaam.

Ndalichako amesema miongozo ikipelekwa kwenye halmashauri itasaidia  kupatikana kwa wabunifu watakaoendeleza  Teknolojia  na kufanya kazi katika viwanda.

Waziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia Elimu, Sayansi na Teknlojia amesema uchumi wa viwanda unategemea Sayansi  na wataalamu wenye ujuzi wakutengeneza na kubuni bidhaa mbalimbali zitakazotumika   viwandani lakini pia kuiletea jamii Maendeleo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka kwa Mwanafunzi wa Shule ya St Jude Erick Laizer kuhusu ubunifu wa mtambo wa ulinzi dhidi ya moto na wizi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa COSTECH  Dkt. Amos Nungu, amesema Kongamano hilo la siku tatu Lina lengo la  kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi, ikiwa ni pamoja  na kuanzisha na kuendeleza viwanda.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Abubakari Amani mtaalam aliyetengeza mashine ya kupurura ama kupura maharage katika   kongamano la sita la  Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linaloendelea jijini Dar es Salaam.

SERIKALI YAANZA KUKARABATI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI.


·         PROFESA MDOE ASISITIZA MATUMIZI YA FORCE AKAUNTI

Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wakuu wa Vyuo vya maendeleo ya Jamii nchini na Maboharia kutumia kikamilifu utaalamu watakaoupata katika mafunzo ya namna ya kutumia Force Account na kuhakikisha wanasimamia kikamilifu shughuli za ujenzi na ukarabati katika vyuo hivyo.

Profesa Mdoe ametoa kauli hiyo Mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa washiriki hao na kusisitiza kuwa   Serikali kwa sasa inakarabati vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, hivyo mafunzo watakayoyapata yakawe chachu ya kusimamia kazi hiyo kwa umakini na uadilifu ili thamani ya matumizi ya fedha iweze kuonekana.

“Ni vizuri mkashiriki mafunzo haya kikamilifu kwa kuwa matokeo ya mafunzo haya yataonekana katika utekelezaji wa miradi na kila mtu atawajibika kwa nafasi yake, thamani ya Fedha lazima iende ikaonekana katika utekelezaji wa uboreshaji wa vyuo hivi vya FDCs,” alisisitiza Profesa Mdoe.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya matumizi ya Force Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kutumia utaalamu watakaoupata katika kusimamia ujenzi na ukarabati katika vyuo vyao.

Profesa Mdoe amesema matumizi ya utaratibu wa Force Akaunti ni mzuri kwa kuwa gharama zinazotumika katika ujenzi na ukarabati ni ndogo na hii inatokana na kutumia wataalam na vifaa vya vinavyonunuliwa na kusimamiwa Taasisi husika.

Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Ajira umeanzishwa kwa lengo la kutekeleza vipaumbele vya Serikali vilivyoainishwa katika mkakati wa Serikali wa kufikia Tanzania ya Viwanda ifikapo 2025, lakini pia kuwezesha vijana kupata ujuzi kwa vitendo kuliko nadharia pamoja na kujengea uwezo vyuo vya kati.
Wajumbe wa Kikao wakifuatilia hotuba ya Kaimu Katibu Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Profesa James Mdoe wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya Force Account kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na Wahasibu yaliyofanyika mjini Morogoro.

Mafunzo hayo ya siku tatu yanahusisha Wakuu wa vyuo vya FDCs 11, Wahasibu na maboharia na yanatarajiwa kukamilika kesho kutwa.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Profesa James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya Washiriki wa mafunzo ya namna ya kutumia force Account yaliyofanyika Mjini Morogoro.

Jumanne, 3 Julai 2018

SERIKALI IMEKABIDHI PIKIPIKI ZAIDI YA 2500 KUBORESHA ELIMU NCHINI


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leo imekabidhi Pikipiki zaidi ya 2500 kwa  Waratibu Elimu Kata ili ziwasidie katika kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuimarisha Elimu hapa nchini.

Pikipiki hizo zinakabidhiwa Leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa  Joyce Ndalichako ambapo amesema Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES)  umenunua Pikipiki hizo 2894 kwa zaidi ya shilingi bilioni  Nane.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakikata utepe kuashiria makabidhiano ya Pikipiki zilizotolewa na Wizara ya Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) wanaoshuhudia tukio hilo ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda 

Waziri Ndalichako amesema pikipiki hizo zitasambazwa nchi nzima kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI.
"Rais alipoingia madarakani alihaidi kuimarisha ubora wa Elimu, sasa moja ya mikakati ya kutekelez hilo ndiyo maana hii Leo tunashuhudia vitendea Kazi hivi ambavyo vitasambazwa nchi nzima, lengo hapa ni kuhakikisha Elimu  inayotolewa inakuwa bora na kuhakikisha  nchi inakuwa na matokeo chanya kiuchumi” amesema Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amewataka waratibu elimu Kata hao kuhakikisha pikipiki hizo zinatumika kwa ajili yakusimamia elimu katika maeneo yao na kupandisha ufaulu na si vinginevyo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo wakizijaribu Pikipiki zilizotolewa kwa Waratibu Elimu Kata nchini Kata ili ziwasidie katika kutekeleza majukumu yao wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda

Kwa upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amewataka waratibu elimu kata kuhakikisha wanasimamia taaluma katika maeneo yao.

Aidha, Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Mikoa, Halmashauri, Manispaa na Majiji kuweka utaratibu wa kuzihudumia pikipiki hizo katika maeneo yao.


Mmoja wa Waratibu Elimu Kata akijaribu kuendesha Pikipiki iliyokabidhiwa kwake kwa ajili ya kumsaidia kusimamia elimu katika kata yake huku akishuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha

NAIBU WAZIRI OLE NASHA: VYUO VYA UFUNDI VINAMUANDAA KIJANA KUJIAJIRI NA KUAJIRIWA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mheshimiwa William Ole Nasha amewataka vijana kuachana na dhana ya kuwa ili kufanikiwa katika maisha lazima uwe umesoma hadi chuo Kikuu lakini ukweli ni kuwa vyuo vya ufundi  vinamuandaa kijana kuwa na uwezo wa kujiajiri na pia kuajiriwa ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo wakati alipotembelea Baadhi ya Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo ambazo zinashiriki maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mheshimiwa William Ole Nasha akisikiliza maelezo ya jinsi mtambo wa kusaidia kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka kwa mmoja wa mwanafunzi wa VETA Moshi alipotembelea Baadhi ya Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo ambazo zinashiriki maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.


Mheshimiwa Ole Nasha amewahakikishia Watanzania kuwa Elimu inayotolewa hapa nchini ina viwango vya ubora unaokubalija na ndiyo maana  vijana wengi wanaajiriwa nje ya nchi  kutokana na kile wanachokuwa wamekisomea.

Naibu Waziri ameleza kuwa serikali ya awamu ya Tano imeboresha Mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vya Ufundi kwa kununua mitambo na vifaa vya kisasa ili kuimarisha mafunzo yanayotolewa na vyuo hivyo.

“ Uwekezaji huu mkubwa unalenga kuhakikisha vijana wanaohitimu katika vyuo vya Ufundi nchini wanakidhi soko la ajira la ndani na nje y nchi,”amesema Mheshimiwa Ole Nasha.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mheshimiwa William Ole Nasha akiwa katika banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati alipotembelea maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Taasisi zinazoshiriki Mamlaka ya Ufundi stadi- VETA, CHUO Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Cha Mzumbe, Taasisi ya Teknolojia-DIT, Baraza la Ufundi la Taifa-NACTE, Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi MUHAS  na Tume ya nguvu za Atomiki.

Jumatatu, 2 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AMEWATAKA WATAFITI KUTAFSIRI MATOKEO YA TAFITI KUWA BIDHAA NA HUDUMA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka watafiti wa afya nchini kupanga mipango ya utafiti kuzingatia matakwa ya wateja wanaowahudunia na kutafsiri matokeo ya tafiti hizo kuwa bidhaa na huduma.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa kongamano la sita la kisayansi jijini Dar es Salaam na kusisitiza  kuwa utafiti unapotafsiriwa unaweza kubadilisha na kuboresha huduma zinavyotolewa pamoja na kusaidia taifa kufikia uchumi wa viwanda.  


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia Pfro . Joyce Ndalichako akizungumza wajumbe (hawapo Pichani) wa kongoamano la sita la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) ambapo aliwasisitiza kupanga mipango ya utafiti kuzingatia matakwa ya wateja wanaowahudunia na kutafsiri matokeo ya tafiti hizo kuwa bidhaa na huduma

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Andrea Pembe amesema tafiti zitakazowasiliwashwa ni pamoja na masuala ya Afya ya Uzazi, Magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, na magonjwa yanayoambukiza, Sera ya Afya, Madawa ya jadi na mbadala na Sayansi ya madawa.

Kauli mbiu ya Kongamano hilo ni “Uimarishaji wa Uchumi wa Viwanda kupitia Tafiti za Afya kwenye nchi zenye kipato cha chini”.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia Pfro . Joyce Ndalichako akipata maelezo kuhusu dawa mbalimbali za usafi zilizotengenezwa na wadau wa afya wakati wa  kongoamano la sita la Kisayansi lililofanyika Jijini Dar es Salaam

Lengo la Kauli Mbiu hiyo ni kusisitiza umuhimu wa matumizi ya matokeo ya tafiti za Kisayansi za afya katika kuchangia uimarishaji wa uchumi wa viwanda.
Kongamano hilo la kisayansi limeandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na limeshirikisha jumla ya washiriki na wajumbe zaidi ya 400 kutoka nchini na nchi za Rwanda, Uingreza, Japan, Uturuki, Italy, Marekani na wenyeji Tanzania.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolijia Pfro . Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kongoamano la sita la Kisayansi lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS)

Alhamisi, 21 Juni 2018

PROFESA MDOE APONGEZA UBUNIFU NA KUWATAKA WANAFUNZI WABUNIFU KUJITOKEZA KWA WINGI


Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wanafunzi ambao wanakipaji cha ubunifu kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi ili waweze kuonyesha vipaji vyao, kwa kuwa bunifu zao zinatakiwa zitatue changamoto mbalimbali hapa nchini.

Profesa Mdoe ameyasema hayo leo mkoani Dodoma wakati akifunga jukwaa la Maonesho ya ubunifu kwa vijana wenye umri kuanzia miaka 13 hadi 21 yanayosimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia chini ya Mradi wa kukuza Ujuzi, na stadi za kazi, ESPJ.
Kaimu Katibu Mkuu huyo amesema vijana wabunifu wakiendelezwa vyema watapata fursa ya kuchangia uchumi wa Taifa kupitia bunifu zao mbalimbali.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akizungumza na wadau mbalimbali wa masuala ya ubunifu wakati akifunga maonesho ya ubunifu yaliyohusisha wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari kutoka Tanzania bara na Visiwani, yaliyofanyika mkoani Dodoma.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu akizungumza katika maonesho hayo ametambua mchango wa kijana Keton Mbwiro ambaye amehitimu Elimu yake ya Msingi na ameweza kubuni kijiko maalumu cha gari ambacho hutumika kuchimba na kuchota mchanga. Pia amebuni gari la kubeba vifaa vya ujenzi hivyo ameahidi kuwa kijana huyo atapelekwa shule ya ufundi ili aweze kujiendeleza.

“Keton Mbwiro ni kijana mdogo lakini ameweza kubuni kitu ambacho miaka ya nyuma tulizoea kuona vitu vya namna hii vinafanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu, hivyo uwezo wake lazima tuuendeleze kwa kuhakikisha anakwenda shule ya Ufundi, pia ni vyema watanzania tukaachana na dhana ya kuwa vyuo vya ufundi ni vya useremala pekee bali ni zaidi ya hapo.” anasema Dk. Semakafu.
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiwa na baadhi ya watendaji wa Wizara hiyo wakiangalia moja ya ubunifu uliohusisha mashine ya kusafishia/kuondoa uchafu kwenye mazulia. Maonesho hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, Mjini Dodoma. 

Mradi wa kukuza Ujuzi na Stadi za kazi, ESPJ ni mradi wa miaka miatano ambao unatekelezwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Benki ya Dunia, lengo likiwa ni kuhakikisha mkakati wa Serikali wa Tanzania kuwa
nchi ya Uchumi wa viwanda mpaka 2025 inatimia.
Prof. James Mdoe ambae ni Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akiwa ameshika chupa yenye dizeli iliyotokana na kuyeyushwa kwa chupa za plastiki ambazo zimekwisha matumizi yake.