Alhamisi, 12 Julai 2018
Jumatano, 11 Julai 2018
WAZIRI NDALICHAKO AMTAKA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU KUWACHUKULIA HATUA WALIOHUSIKA NA SAKATA LA VIFAA VYA MAABARA CHUO CHA UALIMU KASULU
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo
kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uagizaji na upokeaji wa vifaa vya
maabara katika Chuo cha Ualimu Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako ametoa
kauli hiyo Wilayani Kasulu alipofanya ziara katika Chuo hicho na kukuta idadi
kubwa ya kemikali za maabara zisizohitajika lakini pia vifaa vya maabara
kutokuwa na ubora huku chuo kikiomba kununuliwa tena vifaa vya maabara na
kemikali.
“Haiwezekani kwa sasa
manasema mna upungufu wa vifaa pamoja na kemikali wakati mmevijaza hapa chuoni
tena kwa utaratibu usiofaa, huku mkisema vitaharibika kwa kuwa havihitajiki, ni
nani aliviagiza na ni kwanini mliviagiza bila ya kuwa na uhitaji, kwa hili sio
la kufumbia macho ni lazima hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika katika
suala hili”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipokelewa na Mwenyekiti wa
Bodi pamoja na Watumishi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Mkoani Kigoma
wakati alipowasili chuoni hapo.
Waziri Ndalichako pia
ameitaka Idara ya Elimu ya Ualimu katika Wizara hiyo pamoja na Chuo cha Ualimu
Kasulu kutoa taarifa ya kina ya uagizaji na upokeaji wa vifaa hivyo kwa kuwa
kumekuwepo na kutokuelewana baina yao ni nani alitoa mahitaji halisi ya vifaa
hivyo hali iliyoisababishia Serikali hasara ya kununua vifaa visivyohitajika
wakati zipo shule za Sekondari zingeweza kupata vifaa hivyo.
“Bahati mbaya bodi yenu
haina taarifa ya manunuzi haya, wakuu wa vyuo muache tabia ya kuficha mambo
yanayoendelea chuoni hapa nachukua hatua na bodi iangalie hatua za kuchukua
hatuwezi kuruhusu mtu anayefanya uhalifu huu akabaki salama,” alisema Profesa
Ndalichako.
Wzairi wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua kemikali za Maabara
katika Chuo cha Ualimu Kasulu
Awali Mkuu wa Chuo cha
Ualimu Kasulu Josephat Mwangamila katika hotuba yake alisema Chuo hicho kina
deni la takribani shilingi milioni 64 kwa ajili ya ununuzi wa Kemikali na Vifaa kwa
ajili ya matumizi ya ofisi (stationary) kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha
sita waliofanya mitihani.
Mkuu wa Chuo alisema
walifikia uamuzi wa kununua kemikali hizo kwa kuwa hawakuwa nazo chuoni hapo
lakini pia zilizokuwepo hazihitajiki kwa matumizi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya majengo
ya Chuo Cha Ualimu Kabanga Mkoani Kigoma. Akiwa Chuoni hapo Profesa Ndalichako
amezungumza na wakufunzi pamoja na watumishi wa chuo na kuahidi kujenga upya
Chuo hicho kwa kuwa miundombinu yake imechakaa.
Serikali imenunua vifaa vya
maabara vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Moja ambavyo vimesambazwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini ikiwa ni
juhudi za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ili wakaweze kufundisha
kwa umahiri pindi wanapomaliza masomo yao.
Waziri wa Elimu pia
ametembelea Chuo cha Ualimu Kabanga ambapo ameahidi kujenga upya chuo hicho
katika mwaka wa fedha ulioanza 2018/19 kwa kuwa majengo yake ni chakavu na
kuvitaka vyuo ambavyo vimekarabatiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kutunza
miundombinu ya vyuo.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ngazi za
mabweni ambayo imechakaa katika Chuo Cha Ualimu Kasulu, Wilayani Kasulu Mkoani
Kigoma
Ijumaa, 6 Julai 2018
DK. SEMAKAFU ASEMA HAKUNA ATAKAESALIMIKA MATUMIZI YA FORCE AKAUNTI
Serikali
imesema haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa mtu yeyote atakayekiuka
utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika kutekeleza shughuli za ujenzi na
ukarabati kwenye Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDC’S).
Kauli
hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Dk.
Avemaria Semakafu mjini Morogoro wakati
wa akifunga mafunzo ya siku tatu kwa wakuu wa vyuo, maboharia na wahasibu
kuhusu utaratibu wa kutumia Force Akaunti katika shughuli za ujenzi na
ukarabati katika vyuo vya FDCs.
kuwa upo kisheria na kwa
yeyote atakaepindisha utaratibu huo atawajibika kwa hilo. Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akizungumza na
wajumbe (hawapo pichani) wakati akifunga mafunzo ya matumizi ya utaratibu wa
Force Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kuhakikisha wanafuata utaratibu
huo.
Alisema
utaratibu huo uko kisheria na kwamba mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha kupata
taaluma ya kutumia utaratibu huo ambapo
amewataka washiriki hao kwenda kutumia taaluma hiyo kama nyenzo kuleta
mabadiliko wakati wa kutekeleza miradi katika maeneo yao.
Wajumbe wa Kikao
wakifuatilia hotuba ya Naibu Katibu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk.
Avemaria Semakafu wakati wa kufunga mafunzo ya matumizi ya Force Account kwa
Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na Wahasibu yaliyofanyika
mjini Morogoro.
Amesema Vyuo vya maendeleo ya Wananchi
vilianzishwa kwa malengo mahususi ikiwa ni pamoja na kutoa stadi na mafunzo kwa
wananchi hivyo miradi hiyo ikikamilika kwa wakati vyuo vitaweza kutimiza
malengo yake lakini pia thamani halisi ya matumizi ya fedha (Value for Money)
za ujenzi na ukarabati zitaonekana.
Mafunzo
hayo ya utaratibu wa kutumia Force Akaunti yameshirikisha wajumbe kutoka Vyuo
vya maenedeleo ya wananchi 11 na yameendeshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia chini ya mradi wa Kukuza
Ujuzi na Stadi za Ajira (ESPJ).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Avemaria Semakafu akiwa katika picha ya
pamoja na baadhi ya Washiriki wa mafunzo
ya namna ya kutumia force Akaunti yaliyofanyika Mjini Morogoro.
Jumatano, 4 Julai 2018
WAZIRI NDALICHAKO AIELEKEZA COSTECH KUPELEKEA MIONGOZO YA KUSAIDIA WABUNIFU KWENYE HALMASHAURI
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Profesa Joyce NDALICHAKO ameitaka Tume ya Taifa ya Sayansi naTeknolojia,
COSTECH -kuhakikisha miongozo yote ya namna yakuwasaidia wabunifu
inapelekwa katika ngazi ya Halmashauri
ili kuwezesha kupatikana kwa bunifu zitakazosaidia nchi kufikia uchumi wa
viwanda.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo
katika kongamano la sita la Kitaifa la
Sayansi, Teknolojia na ubunifu linalofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na wanasayansi na wavunifu katika
kongamano la sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu linalofanyika
jijini Dar es Salaam.
Ndalichako amesema miongozo ikipelekwa
kwenye halmashauri itasaidia kupatikana
kwa wabunifu watakaoendeleza
Teknolojia na kufanya kazi katika
viwanda.
Waziri huyo mwenye dhamana ya kusimamia
Elimu, Sayansi na Teknlojia amesema uchumi wa viwanda unategemea Sayansi na wataalamu wenye ujuzi wakutengeneza na kubuni
bidhaa mbalimbali zitakazotumika
viwandani lakini pia kuiletea jamii Maendeleo.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka
kwa Mwanafunzi wa Shule ya St Jude Erick Laizer kuhusu ubunifu wa mtambo wa
ulinzi dhidi ya moto na wizi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa
COSTECH Dkt. Amos Nungu, amesema
Kongamano hilo la siku tatu Lina lengo la
kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuendeleza viwanda.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Abubakari
Amani mtaalam aliyetengeza mashine ya kupurura ama kupura maharage katika kongamano la sita la Kitaifa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu
linaloendelea jijini Dar es Salaam.
SERIKALI YAANZA KUKARABATI VYUO VYA MAENDELEO YA WANANCHI.
·
PROFESA MDOE ASISITIZA MATUMIZI YA FORCE
AKAUNTI
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya
Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe amewataka wakuu wa Vyuo vya
maendeleo ya Jamii nchini na Maboharia kutumia kikamilifu utaalamu watakaoupata
katika mafunzo ya namna ya kutumia Force Account na kuhakikisha wanasimamia
kikamilifu shughuli za ujenzi na ukarabati katika vyuo hivyo.
Profesa Mdoe ametoa kauli
hiyo Mjini Morogoro wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa washiriki hao na
kusisitiza kuwa Serikali kwa sasa
inakarabati vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, hivyo mafunzo watakayoyapata yakawe
chachu ya kusimamia kazi hiyo kwa umakini na uadilifu ili thamani ya matumizi
ya fedha iweze kuonekana.
“Ni vizuri mkashiriki
mafunzo haya kikamilifu kwa kuwa matokeo ya mafunzo haya yataonekana katika
utekelezaji wa miradi na kila mtu atawajibika kwa nafasi yake, thamani ya Fedha
lazima iende ikaonekana katika utekelezaji wa uboreshaji wa vyuo hivi vya
FDCs,” alisisitiza Profesa Mdoe.
Kaimu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa James Mdoe
akizungumza na wajumbe (hawapo pichani) wakati wa mafunzo ya matumizi ya Force
Account Mjini Morogoro. Amewataka wajumbe kutumia utaalamu watakaoupata katika
kusimamia ujenzi na ukarabati katika vyuo vyao.
Profesa Mdoe amesema matumizi ya utaratibu wa
Force Akaunti ni mzuri kwa kuwa gharama zinazotumika katika ujenzi na ukarabati
ni ndogo na hii inatokana na kutumia wataalam na vifaa vya vinavyonunuliwa na
kusimamiwa Taasisi husika.
Mradi wa Kukuza Ujuzi na Stadi za Ajira umeanzishwa kwa
lengo la kutekeleza vipaumbele vya Serikali vilivyoainishwa katika mkakati wa
Serikali wa kufikia Tanzania ya Viwanda ifikapo 2025, lakini pia kuwezesha
vijana kupata ujuzi kwa vitendo kuliko nadharia pamoja na kujengea uwezo vyuo
vya kati.
Wajumbe
wa Kikao wakifuatilia hotuba ya Kaimu Katibu Wizara ya Elimu, Saynsi na
Teknolojia Profesa James Mdoe wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya
Force Account kwa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi, Maboharia na
Wahasibu yaliyofanyika mjini Morogoro.
Mafunzo hayo ya siku tatu
yanahusisha Wakuu wa vyuo vya FDCs 11, Wahasibu na maboharia na yanatarajiwa kukamilika
kesho kutwa.
Kaimu
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Saynsi na Teknolojia Profesa James Mdoe akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya
Washiriki wa mafunzo ya namna ya kutumia force Account yaliyofanyika Mjini
Morogoro.
Jumanne, 3 Julai 2018
SERIKALI IMEKABIDHI PIKIPIKI ZAIDI YA 2500 KUBORESHA ELIMU NCHINI
Wizara
ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Leo imekabidhi Pikipiki zaidi ya 2500 kwa Waratibu Elimu Kata ili ziwasidie katika
kutekeleza majukumu yao kwa lengo la kuimarisha Elimu hapa nchini.
Pikipiki
hizo zinakabidhiwa Leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako
ambapo amesema Wizara ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma,
Kuandika na Kuhesabu (LANES) umenunua
Pikipiki hizo 2894 kwa zaidi ya shilingi bilioni Nane.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo
wakikata utepe kuashiria makabidhiano ya Pikipiki zilizotolewa na Wizara ya Wizara
ya Elimu kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (LANES) wanaoshuhudia
tukio hilo ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha,
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda
Waziri
Ndalichako amesema pikipiki hizo zitasambazwa nchi nzima kupitia Ofisi ya Rais
TAMISEMI.
"Rais
alipoingia madarakani alihaidi kuimarisha ubora wa Elimu, sasa moja ya mikakati
ya kutekelez hilo ndiyo maana hii Leo tunashuhudia vitendea Kazi hivi ambavyo
vitasambazwa nchi nzima, lengo hapa ni kuhakikisha Elimu inayotolewa inakuwa bora na kuhakikisha nchi inakuwa na matokeo chanya kiuchumi”
amesema Ndalichako.
Waziri
Ndalichako pia amewataka waratibu elimu Kata hao kuhakikisha pikipiki hizo
zinatumika kwa ajili yakusimamia elimu katika maeneo yao na kupandisha ufaulu
na si vinginevyo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.
Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo
wakizijaribu Pikipiki zilizotolewa kwa Waratibu Elimu Kata nchini Kata ili ziwasidie katika kutekeleza majukumu yao wengine katika picha
ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha, Kaimu Katibu
Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Pfor. James Mdoe na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda
Kwa
upande wake Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Selemani Jafo amewataka
waratibu elimu kata kuhakikisha wanasimamia taaluma katika maeneo yao.
Aidha,
Jafo amewaagiza Wakurugenzi wa Mikoa, Halmashauri, Manispaa na Majiji kuweka
utaratibu wa kuzihudumia pikipiki hizo katika maeneo yao.
Mmoja wa Waratibu Elimu Kata akijaribu
kuendesha Pikipiki iliyokabidhiwa kwake kwa ajili ya kumsaidia kusimamia elimu
katika kata yake huku akishuhudiwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI
Selemani Jafo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha
NAIBU WAZIRI OLE NASHA: VYUO VYA UFUNDI VINAMUANDAA KIJANA KUJIAJIRI NA KUAJIRIWA
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mheshimiwa
William Ole Nasha amewataka vijana kuachana na dhana ya kuwa ili kufanikiwa
katika maisha lazima uwe umesoma hadi chuo Kikuu lakini ukweli ni kuwa vyuo vya
ufundi vinamuandaa kijana kuwa na uwezo
wa kujiajiri na pia kuajiriwa ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo wakati
alipotembelea Baadhi ya Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo ambazo zinashiriki maonesho
ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia
Mheshimiwa William Ole Nasha akisikiliza maelezo ya jinsi mtambo wa kusaidia
kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi kutoka kwa mmoja wa mwanafunzi wa VETA
Moshi alipotembelea Baadhi ya Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo ambazo
zinashiriki maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Mheshimiwa Ole Nasha amewahakikishia Watanzania kuwa
Elimu inayotolewa hapa nchini ina viwango vya ubora unaokubalija na ndiyo
maana vijana wengi wanaajiriwa nje ya
nchi kutokana na kile wanachokuwa
wamekisomea.
Naibu Waziri ameleza kuwa serikali ya awamu ya Tano
imeboresha Mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika vyuo vya Ufundi kwa
kununua mitambo na vifaa vya kisasa ili kuimarisha mafunzo yanayotolewa na vyuo
hivyo.
“ Uwekezaji huu mkubwa unalenga kuhakikisha vijana
wanaohitimu katika vyuo vya Ufundi nchini wanakidhi soko la ajira la ndani na
nje y nchi,”amesema Mheshimiwa Ole Nasha.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknlojia Mheshimiwa William Ole Nasha akiwa katika
banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati alipotembelea maonesho ya sabasaba
yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Taasisi zinazoshiriki Mamlaka ya Ufundi stadi- VETA, CHUO
Kikuu Cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Cha Mzumbe, Taasisi ya Teknolojia-DIT,
Baraza la Ufundi la Taifa-NACTE, Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Chuo
Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi MUHAS na Tume ya nguvu za Atomiki.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)