Jumatano, 6 Machi 2019

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ASEMA SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UBUNIFU VINACHANGIA UKUAJI WA UCHUMI



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nashaa mesema Sayansi, Teknolojia na ubunifu ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema hayo leo wakati wa kufungua mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na ubunifu yanayofanyika mkoani Dodoma na kusisitiza kuwa ubunifu na ugunduzi una fursa ya kuchagiza katika kuongeza tija kwenye viwanda vikubwa, hivyo uhamasishaji wa pamoja unahitajika.
Naibu Waziri Mhe. William Ole Nasha akizungumza wakati akifungua mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu ambayo kitaifa yanafanyika mkoani Dodoma.
“Hulka ya ubunifu ni mtu anazaliwa nayo, na kwa jinsi nilivyotembelea mabanda mbalimbali ya maonesho haya tayari mimi naona wote hapa ni washindi, sasa niishauri Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia - COSTECH ione namna ya kuwaendeleza wabunifu wote na isiwe ni kwa wabunifu wachache,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha.

Mhe. Ole Nasha amesema kutokana na umuhimu wa wabunifu na wagunduzi nchini ni vyema wananchi wakaendelea kuhamasishwa ikiwa ni pamoja na mashindano hayo yakawa yanafanyika kila mwaka.
Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Ilboru, Maximillian akimuelezea Naibu Waziri Ole Nasha na Viongozi wengine namna anavyotekeleza ubunifu wake.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Kaimu Katibu Mkuu Profesa James Mdoe amesema lengo la mashindano hayo ni kukuza hamasa za ubunifu na kuchochea ugunduzi utakaohamasisha Mapinduzi ya Viwanda.
Mwanafunzi wa Chuo Cha Usafirishaji - NIT akimuendesha Naibu Waziri kwenye gari ambalo linatumia mfumo wa umeme kufanya kazi, na kuwa gari hilo halina injini.
Baada ya mashindano hayo kutangazwa Wabunifu zaidi ya 400 walijitokeza kushiriki na kati yao wabunifu 60 walichaguliwa kiushindani na ndiyo ambao wameshiriki mashindano ambayo yanafanyika kitaifa mkoani Dodoma.

Kaulimbiu ya mashindano hayo ni, kukuza ujuzi na ubunifu kwa uchumi wa viwanda.
Bustani ya mbogamboga ambayo haitumii udongo ikiwa imeoteshwa mboga mbalimbali za majani.

SERIKALI YATOA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI MOJA KUJENGA NA KUKAMILISHA MIUNDOMBINU YA SHULE WILAYANI BUHIGWE-KIGOMA


Serikali imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga na kukamilisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ulioanzishwa kwa nguvu za wananchi katika shule ya sekondari Janda iliyopo katika kata ya Janda wilayani Buhigwe.
Waziri waElimu, SayansinaTeknolojiaProfesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya nyumba za walimu ambazo katika shule ya Sekondari Janda iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe Mkoani Kigoma.
Waziri Ndalichako pamoja na kupongeza hatua hiyo ya wananchi amesema tayari Wizara kupitia Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo(EP4R) imeingiza fedha zaidi ya shilingi milioni Mia Tisa   kwenye akaunti ya Halmashauri ya Buhigwe ambazo zitatumika kuanza ujenzi wa shule mpya ya msingi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 945 na kundeleza ujenzi wa miradi mingine ya shule ambayo haijakamilika.

 “Kwanza niwapongeze wananchi wa Buhigwe kwa hatua hii, hapa  kwenye Halmashauri ya Buhigwe bado kuna kazi kubwa ya kufanya, ukiangalia idadi ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na idadi ya sekondari zilizopo, bado wanafunzi wengi  wanabaki hivyo nawasihi wananchi endeleeni kuchangia ujenzi wa miundombinu ya shule na serikali itaunga mkono juhudi hizo”, alisema Waziri Ndalichako.
Waziri waElimu, SayansinaTeknolojiaProfesa Joyce Ndalichako akiongea na wanafunzi wa shule ya Sekondari Janda iliyoko Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma. Amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu na kufikia malengo yao.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameeleza kusikitishwa na ufaulu duni wa wanafunzi wa kike katika mkoa wa kigoma na hasa  shule ya sekondari  Janda na kuwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.

“Nimeangalia  katika matokeo yenu miaka miwili iliyopita hakuna anaepata daraja la kwanza, mnaanzia daraja la tatu hadi sifuri kwa nini hamjitahidi, serikali inalipa ada  ili ninyi msome nahitaji mabadiliko ongezeni juhudi katika masomo,” aliongeza waziri Ndalichako.
Muonekano wa Hatua ya ujenzi wa nyumba za walimu katika shule ya Sekondari Janda iliyopo katika Halmashauri ya wilaya ya Kilosa Mkoani Kigoma.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Luteni Kanali Michael Ngayalina alimweleza Waziri kuwa Halmashauri hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya madarasa 25, na kusema kuwa tayari ameagiza kila kijiji kujenga darasa moja katika shule ya kata.

Jumapili, 3 Machi 2019

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WATOTO WA KIKE KUSHIRIKI MICHEZO ILI KUEPUKA VISHAWISHI


Wanafunzi wa kike nchini wametakiwa kushiriki kikamilifu katika michezo ili kuimarisha afya ya akili katika masomo na kuepuka vishawishi vinavyoweza kuharibu ndoto zao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako  wakati wa bonanza la mpira wa miguu maarufu kama MIRIAM CUP lililoshirikisha wanafunzi wa kike kutoka shule za msingi, secondari, vyuo vya ualimu na vile vya Maendeleo ya wananchi lililofanyika wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikabidhi kombe wa wanachuo wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma baada ya kuibuka kidedea katika mechi zilizoshindanisha wanafunzi wa kike kutoka shule za Msingi, Sekondari, Vyuo vya Ualimu na vile vya Maendeleo ya wananchi vilivyopo katika Halmashauri ya Kasulu.

Waziri Ndalichako amesema  lengo la bonanza hilo ni kutoa hamasa kwa watoto wa kike kujiepusha na mimba za utotoni  na kuwa michezo ikitumika vizuri ina nafasi kubwa ya kumkomboa mtoto wa kike kielimu.

'' Michezo inachangamsha akili, michezo inajenga afya iliyobora lakini pia michezo ni ajira na inaondoa vishawishi,” alisisitiza Waziri Ndalichako.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akisalimiana na wanafunzi wa kike ambao wameshiriki bonanza la mpira wa miguu almaarufu MIRIAM CUP lililoandaliwa na mdau wa Elimu Miriam Ntakisivya kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi wa kike kukataa mimba za utotoni na kuendelea na masomo.

 Waziri Ndalichako amempongeza muandaaji wa bonanza hilo ambaye ni Mdau wa Elimu Miriam Ntakisivya na kusema kuwa bonanza hilo liwe endelevu ili kuleta hamasa kwa wanafunzi wa kike mkoani Kigoma kufanya vizuri katika masomo na kupunguza mimba za utotoni.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Simon Anange amesema wilaya hiyo kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2016 kumekuwa na ufaulu mdogo kwa wanafunzi wa kike wanaomaliza kidato cha nne, hivyo bonanza hilo limewaleta pamoja wazazi, walimu na jumuiya nzima ya Kasulukwa lengo la kukumbushana umuhimu wa kuwapa nafasi watotowa kike kwenye masomo.


Wanafunzi wa kike walioshiriki bonanza la mpira wa miguu wakicheza mpira katika kiwanja cha mpira kilichopo Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Naye muandaaji wa Bonanza hilo Miriam Ntakisivya amesema ameamua kuanzisha bonanza hilo baada ya kuona watoto wa kike mkoani humo  wanashawishiwa na vitu vidogo na kuacha shule wakiwa na umri mdogo na hivyo kuamua kuwaleta pamoja kukataa vitendo hivyo kupitia michezo.

Bonanza hilo limeshirikisha timu za wasichana nane kutoka wilaya ya Kasulu na mechi kubwa iliyohusisha  timu za watani wa jadi Kasulu United FC na Bodaboda FC.



Muandaaji wa Bonanza la mpira wa miguu kwa wanafunzi wa kike katika wilaya ya Kasulu Miriam Ntakisivya akimpa cheti cha shukrani Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako

Jumamosi, 2 Machi 2019

WAZIRI NDALICHAKO ATAKA WANAWAKE KUSHIKAMANA NA KUSAIDIA MAKUNDI YA WATU WASIOJIWEZA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi ya watu wasiojiweza hasa watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Prof Ndalichako ametoa wito huo mkoani Kigoma wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maombi ya dunia ya umoja wa wanawake  wa kikristo  Tanzania  CCT na kusema kuwa wanawake  wakiamua wana uwezo mkubwa wa kubadili maisha katika jamii.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya maombi ya dunia kwa wanawake mkoani Kigoma. Amewataka wanawake kuwa mstari wa mbele kuyasaidia makundi ya watu wasiojiweza na hasa watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili wapate haki zao za msingi hususan elimu.

Amesema wanawake ndio walezi wa watoto kuanzia ngazi za familia akiwafananisha na walimu kwani wao wana jukumu la kulea na kufundisha watoto wote.

“Wanawake wenzangu tukumbushane msemo ambao Mama Salma Kikwete ambae ni mke wa Rais Mstaafu wa awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewahi kusema kuwa mtoto wa mwenzio ni wa kwako hivyo tuwasaidie watoto yatima, wa mitaani na wale wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kutimiza ndoto zao hasa za  kupata elimu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako (aliyepo katikati) akicheza na moja ya kwaya iliyotumbuiza wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya maombi ya dunia kwa wanawake katika Kanisa la Anglikan lililopo mkoani Kigoma.

Pia, Waziri Ndalichako amewataka wanawake nchini kudumisha mshikamano miongoni mwao na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa vitendo kwa kuhakikisha wanafanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali kwa lengo la kujipatia kipato.

Akiwa mkoani humo waziri Ndalichako pia aliwatembelea wagonjwa ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya  Kigoma Maweni na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa hao.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwajulia hali baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Kigoma Maweni. 

Ijumaa, 1 Machi 2019

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUBORESHA IDARA YA UTHIBITI UBORA WA SHULE

Serikali imesema idara ya uthibiti ubora wa shule ndiyo jicho kwa maendeleo ya Elimu ya nchi yetu na ndiyo maana idara hiyo imeendelea kuboreshewa mazingira ya kazi ikiwa ni pamoja na kupatiwa magari 45 kwa lengo la kuongeza ufanisi utendaji kazi.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati akifungua kikao kazi kinacholenga kuwakumbusha wathibiti ubora wa shule wajibu wa utekelezaji wa majukumu yao.





Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wathibiti Ubora wa Shule wakati akifungua kikao kazi hicho mkoani Morogoro


Waziri Ndalichako pia amesema katika kuboresha mazingira Wizara imejipanga kujenga ofisi 100 za wathibiti ubora wa shule, na kuwa fedha kwa ajili ya shughuli hiyo zipo tayari.



Wathibiti Ubora wa Shule wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wakati wa ufunguzi kikao kazi Cha siku nne kinachofanyikia mkoani Morogoro.


“Wathibiti ubora wa shule ni wadau muhimu kwa Maendeleo ya elimu ya nchi yetu, na kuwa nyingi ndiyo jicho la Serikali na ndiyo maana serikali imeendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuleta ufanisi,” alisema Waziri Ndalichako.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya uthibiti ubora wa shule Euphrasia Buchuma amesema kikao kazi hicho  cha siku nne, kina lenga kuwajengea uwezo wa kiutendaji watumishi wa Idara hiyo, kubadilishana uzoefu miongoni mwao, pamoja na kukumbushana matumizi sahihi ya fedha za Umma.


Wathibiti Wakuu Ubora wa Shule Wa Kanda na Wilaya wakifuatilia majadiliano wakati wa kikao kazi cha kukumbusha wajibu wa utekelezaji wa majukumu.

Kikao kazi hicho kimeshirikisha wathibiti wakuu ubora wa shule wa kanda na Wilaya zote 11.



Viongozi na baadhi ya ya Wathibiti Wakuu Ubora Wa Shule wakiwa katika picha ya pamoja .