Jumamosi, 14 Septemba 2019

WAZIRI NDALICHAKO AITAKA BENKI YA BIASHARA YA MWALIMU KUBUNI MBINU ZA KUWAVUTIA WATEJA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ameutaka Uongozi wa Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB BANK) kuboresha huduma za kifedha ikiwemo kuweka vivutio na masharti rafiki ambayo yatawawezesha walimu nchini kukopa fedha ili kukuza vipato vyao.

Prof. Ndalichako ametoa wito huo wakati akifunga Kongamano la Walimu wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusisitiza kuwa matarajio ya serikali ni kuona benki hiyo inakuwa rafiki kwa walimu nchini kwa kuondoa adha na vikwazo ambavyo kwa muda mrefu walimu wamekuwa wakikabiliana navyo katika taasisi mbalimbali  za kifedha.

"Benki ya Biashara ya Mwalimu iwe na ahueni kwa mwalimu anapokuwa ni mteja katika kufanya hivyo walimu wengi watahamasika kujiunga na benki hii, kupitishia mishahara pamoja na hata kuchukua mikopo"
 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa kufunga Kongamano la Walimu lililoandaliwa na Benki ya Biashara ya Mwalimu Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma.


Aidha  ameutaka Uongozi  wa benki hiyo  kusimamia vizuri fedha iliyokwisha wekezwa na walimu ili kuwavutia walimu wengine ambao bado hawajajiunga na kusisitiza kuwepo na kasi ya uanzishwaji wa ofisi za benki hiyo katika mikoa yote nchini iongezeke ili kuwavutia wateja.

"Nafahamu kwamba tayari  mnatoa huduma kidijitali na mnashirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma katika maeneo ambayo hamna ofisi, lakini ni muhimu mkaharakisha uanzishwaji wa ofisi zenu kila mkoa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma," amesema Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amewaasa walimu nchini kuwa na utamaduni wa kujiwekea akiba pindi wanapopata mishahara yao ili iwasaidie kuanzisha miradi mingine ya kiuchumi ambayo itakuwa mkombozi wa maisha yao pindi wanapostaafu.

"Walimu tambueni akiba ni kile kitu unachokiweka kwanza kabla ya kuanza matumizi, lakini watu wengi wanadhani akiba ni bakaa baada ya matumizi kwa utaratibu huo kamwe hakutakuwa na kitu kinachobaki," amesema Ndalichako.


Baadhi ya Walimu wa mkoa wa Kigoma walioshiriki Kongamano wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako. Kongamano limeandaliwa na Benki ya Biashara ya walimu ili kutoa elimu ya kifedha kwao.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya Mwalimu, Richard Makungwa amesema benki hiyo imeendelea kujiimarisha katika kusogeza  huduma kwa wateja wake na kwamba  tayari imeanzisha ofisi zake katika baadhi ya mikoa nchini  ikiwemo Mbeya, Morogoro na Mwanza huku ikishirikiana na Benki ya Posta kutoa huduma kwa wateja ambao bado mikoa yao haijafikiwa.

Amesema katika benki hiyo mwalimu mmoja anamiliki hisa takribani asilimia 35.28 huku chama cha walimu na kampuni yao wakimiliki takribani asilimia 16.17.

"Ukiangalia utakubaliana nami kuwa chombo hiki ni cha walimu na madhumuni yake ni kuwaletea maendeleo wao wenyewe ndiyo maana tukasema lazima tuwafikie walimu popote walipo," amesema Mkurugenzi huyo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiteta jambo na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara ya Mwalimu Richard Makungwa wakati wa hafla ya kufunga Kongamano la Walimu lililoandaliwa na Benki hiyo Kasulu Mkoani Kigoma.

Naye Mkuu wa wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange amesema mara nyingi watumishi wanakosa nidhamu ya fedha na kutumia zaidi ya kile anachopata na kusisitiza kuwa ni vizuri walimu wakawa na utaratibu wa kujiwekea akiba ili pindi wanapostaafu waweze kuishi maisha ambayo wameishi wakiwa kazini.

Mwalimu mstaafu aliyeshiriki kongamano hilo, Kalist Tarimo ameishukuru Benki ya Biashara ya Mwalimu kwa kufanya Kongamano hilo ili kutoa elimu kwao lakini pia ameishauri benki hiyo kuwa na ofisi katika kila Wilaya ili walimu waweze kutumia huduma za benki hiyo.

Kongamano hilo limeandaliwa na Benki ya Biashara ya Mwalimu na limeshirikisha walimu kutoka mkoa wa Kigoma.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Benki ya Biashara ya Mwalimu pamoja na baadhi ya walimu wa mkoa wa Kigoma walioshiriki Kongamano hilo lililofanyika Kasulu Mkoani Kigoma.

Jumatatu, 9 Septemba 2019

SERIKALI YATANGAZA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA MAFUNZO YA UALIMU VYUO VYA SERIKALI


Katibu Mkuu wa Wizara  ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani). Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Avemaria Semakafu.
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza sehemu ya pili ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya ualimu katika vyuo 35 vya serikali.

Akitoa taarifa hiyo jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema jumla ya wanafunzi 2,834 wamechaguliwa kujiungana mafunzo ya ualimu ambapo kati yao 1,013 ni wa Astashahada na 1,821 ni wa Stashahada.

Dkt. Akwilapo ameongeza kuwa hadi sasa jumla ya wanafunzi 11,028 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu vya serikali ambapo kati yao wanafunzi 8,194 walichaguliwa awali na TAMISEMI na 2,834 wamechaguliwa na NACTE.

Aidha, Dkt. Akwilapo amewataka wanafunzi hao waliochaguliwa kuripoti katika vyuo walivyopangiwa kuanzia tarehe 20 Septemba mwaka huu na kwamba mwisho wa kuripoti ni tarehe 6 Oktoba mwaka huu.  Amesisitiza wahakikishe wanaripoti ndani ya muda huo kwani baada ya hapo hawatapokelewa na nafasi zao zitajazwa na wengine wenye sifa ambao walikosa nafasi.

“Wanafunzi wote waliochaguliwa wanatakiwa waripoti katika vyuo vyao kuanzia tarehe 20 mwezi huu hadi 6 Oktoba mwaka huu.  Watakaoripoti baada ya hapo hawatapokelewa na nafasi zao zitajazwa na wanafunzi wengine walioomba ambao wana sifa ila walikosa nafasi,” amesisitiza Dkt. Akwilapo.

Aidha, Dkt. Akwilapo amesema serikali inatambua kuwepo kwa wanafunzi wengi waliokosa nafasi za kujiunga na masomo katika kozi mbalimbali na hivyo ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kufungua dirisha dogo la udahili kwa siku 14 kuanzia tarehe 7 Septemba ili wanafunzi waliokosa nafasi za masomo katika kada mbalimbali waweze kutumia fursa hiyo.


“Wizara inatambua kuwepo kwa idadi kubwa ya waombaji waliokosa nafasi katika awamu hii kutokana aidha na ushindani au kutofanya uchaguzi sahihi wa kozi hivyo wizara inaiagiza NACTE kufungua dirisha dogo la udahili kuanzia leo tarehe 7 hadi 21 Septemba ili kuwapa nafasi waombaji waliokosa nafasi katika programu mbalimbali waweze kufanya uchaguzi upya,” amesema Dkt. Akwilapo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo (katikati) akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma. Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Avemaria Semakafu (kushoto) na Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa Baraza la Taifa la Ufundi (NACTE), Twaha Twaha.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Avemaria Semakafu akiongea katika mkutano huo amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakichagua kozi ambazo hawana sifa zinazohitajika.  Amewaasa waombaju kuzingatia sifa za kozi ili kuepuka kuenguliwa kwani masharti yanayowekwa kuhusu sifa hayabadilishwi.

“Utakuta kwa mfano mtu ana ufaulu mzuri wa alama A hadi C katika masomo ya lugha, badala ya kuchagua kozi zinazotaka ufaulu wa lugha yeye atachagua kozi za masomo ya sayansi ambayo kapata alama D, matokeo yake anajikuta hachaguliwi katika kozi alizoomba,” amesema Dkt. Semakafu.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa NACTE, Twaha Twaha amewatahadharisha waombaji hasa wa kozi za afya kuhakikisha kuwa wamefaulu vizuri katika masomo ya sayansi kwani ndio sifa ya msingi katika udahili wa kozi hizo.


“Katika kozi za afya vigezo vinaangalia masomo, mfano mwanafunzi anayetaka kusoma clinical medicine au nursing, anatakiwa awe na ufaulu wa alama D katika masomo ya Physics, Chemistry na Biology.  Sifa zote hizi zipo katika kitabu cha Mwongozo wa Udahili ambacho kinapatikana kwenye tovuti ya NACTE ambayo ni www.nacte.go.tz,” amesema Twaha.