Jumatatu, 8 Oktoba 2018

OLE NASHA ATOA AGIZO KALI KWA VIONGOZI NA WAZAZI MKOANI MANYARA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha amewataka viongozi kuanzia ngazi ya mkoa hadi vijiji nchini kote kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza darasa la saba hawaondoki katika maeneo yao  kwenda kufanya kazi za ndani wakati wakisubiri matokeo ya kuhitimu darasa la saba, kwani  kufanya hivyo  kunawaondolea fursa  ya kuendelea na masomo pindi wanapofaulu.

Ole Nasha ametoa agizo hilo mkoani Manyara wakati akizungumza na viongozi hao kuhusu hali ya Elimu mkoani humo ambapo amewataka kusimamia kwa ukaribu suala hilo ili kutokatisha ndoto za watoto hao na kwamba wale wanaofanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

"Hakikisheni watoto wanaposubiri matokeo hawasafirishwi kwenda kwenye maeneo mengine kwa ajili ya kufanya kazi za ndani, kumekuwa na tabia za kuwarubuni watoto hata wanapofaulu na kutakiwa kurejea kwa ajili ya masomo hawarejei, Katika hili pia wazazi msiwe sehemu ya kuchangia watoto wenu kwenda mjini kwa kuwa tu wanawatumia fedha kwa ajili ya matumizi bali hakikisheni mnawasimamia vyema na kuwapeleka shule pindi matokeo yanapotoka na kuonekana wamefaulu," alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokelewa na Watendaji wa Mkoa wa Manyara wakati alipowasili mkoani hapo kwa ajili ya kupata taarifa ya Elimu ya Mkoa huo. Naibu waziri huyo yuko Mkoani Manyara kwa ziara ya siku tatu ikiwa ni muendelezo wa ziara zake ambazo amekuwa akizifanya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na kuangalia hali ya Elimu katika mkoa husika.

Kiongozi huyo ameendelea kuwasisitiza wazazi kuwa fursa za Elimu katika nchi yetu ni kubwa, ikizingatiwa kuwa Elimu msingi ni bure hivyo hakuna kisingizio tena kuwa mtoto hawezi kusoma.

Amewataka viongozi hao kutumia sheria kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule wanaandikishwa  ili kutokuwa na wimbi kubwa la watoto wa mitaani wasiokwenda shule.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akitoa maelekezo kwa Viongozi na watendaji wa VETA Manyara wakati wa kukagua karakana inayotumika na wanafunzi wanaosoma kozi ya ufundi wa zana za kilimo (Agro Mechanics). 

Awali Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara Arnold Msuya alimweleza Naibu waziri huyo kuwa mkoa kwa sasa una mwamko mdogo wa Elimu hasa katika jamii ya wafugaji hali inayopelekea wazazi kutowaandikisha shule watoto wenye umri wa kuanza shule.

Naibu waziri Ole Nasha pia ametembelea Chuo cha Ufundi  na Mafunzo ya Ufundi stadi cha Mkoa  Manyara na kuwataka kuboresha  Mitaala yao ili mafunzo wanayoyatoa yaendane na wakati ikiwa ni pamoja na kukidhi  mahitaji ya soko la ajira ili kuongeza fursa ya vijana kujiajiri pindi wanapomaliza masomo yao.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua maendeleo ya ujenzi wa karakana itakayotumiwa na wanafunzi wanaosoma kozi ya ufundi uwashi katika Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Manyara. 

Jumamosi, 6 Oktoba 2018

SERIKALI YAWATAKA WALIMU KUACHA KUFANYA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI


Serikali imewataka walimu wote nchini kuacha kufanya vitendo vya udanganyifu wakati wa mitihani huku ikiwataka wanafunzi kuhakikisha wanatoa  taarifa kuhusu vitendo vya udanganyifu vinapokuwa vinatokea.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani Shinyanga.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof. Joyce Ndalichako akiangalia maonesho ya picha na maandishi mbalimbali kuhusu mwanzilishi wa Shule ya Sekondari ya Don Bosco ambayo ilianzishwa mwaka 1993-2018 na kuwa sasa  imetimiza miaka 25.

Waziri Ndalichako amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na Mashirika ya kidini katika kuwaandaa vijana kitaaluma na kinidhamu na ndiyo maana hakuna vitendo vya udanganyifu katika mitihani kwenye shule hizo kwa kuwa wanafunzi wanaandaliwa vya kutosha pia wana maadili.

“Nichukue fursa hii kuwasihi sana walimu nchini kote kuacha kufanya vitendo vya udanyifu wakati wa mitihani kwa sababu tunawaharibu watoto  na tunatengeneza vijana ambao hawana uwezo kitaaluma, kama tunawafanyia mitihani wakija kupata kazi pia tutawafanyia kazi?

“Nimependa Moto wa shule hii ya Don Bosco Didia kuwa ni kulea, kuwafunza nidhamu watoto kwa lengo la kutimiza ndoto zao naunga mkono juhudi zinazofanywa na viongozi wa shule hii sasa pia ni vyema na shule nyingine zikaiga,” alisisitiza Waziri Ndalichako.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea picha ya mfano wake ambayo imechorwa na mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Don Bosco mkoani Shinyanga wakati wa kuadhimisha miaka 25 tangu shule hiyo ianzishwe.

Waziri Ndalichako ameihakikishia Shule ya Sekondari ya Don Bosco kuwa Serikali iko  pamoja kushirikiana na shule hiyo kwa kuwa mambo wanayoyafanya wanaunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Tano.

Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Zainab Telack ameisifu shule hiyo ya Don Bosco kwa kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha nne na kuwa mkoa unajivunia sana kuwepo kwa shule hiyo ambapo amewasisitiza wanafunzi kuhakikisha wanaendelea kushirikiana ikiwa ni pamoja na kusoma kwa makundi pamoja na kuwasaidia wale ambao uwezo wao ni mdogo.
Waziri Ndalichako akizungumza wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule ya sekondari Don Bosco Didia iliyopo mkoani shinyanga.

Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo mwaka 1993 Baba Vicent alisimikwa rasmi kuwa Baba wa kiroho kwa ajili ya shule hiyo ya Sekondari.

Ijumaa, 5 Oktoba 2018

NDALICHAKO AAGIZA KUONDOLEWA KWA MKUU WA CHUO CHA UALIMU SHINYANGA KWENYE NAFASI YAKE, ASEMA CHUO HICHO KINA HARUFU YA RUSHWA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kumuondoa mara moja Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Shinyanga Paschal Highmagway kwenye nafasi yake kwa kushindwa kusimamia kazi za ujenzi lakini pia kumtetea Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd ili hali Mkandarasi huyo ameshindwa kukamilisha kazi yake katika muda uliopangwa.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu chuoni hapo unaotekelezwa na wakandarasi wawili tofauti ambapo Mkandarasi mmoja ni Masasi Construction Company Ltd amekamisha kazi yake kwa asilimia 98 huku Affrique Enginearing and Construction Company Ltd ikishindwa kukamilisha kazi katika muda uliopangwa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua ujenzi wa miundombinu katika Chuo cha Ualimu Shinyanga, ambapo hajaridhishwa kabisa na kasi  ya ujenzi anayokwenda nayo Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd

Kufuatia hali hiyo Waziri Ndalichako amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Diwani Athumani kuanza kuchunguza miradi inayotekelezwa katika chuo hicho pamoja na maafisa manunuzi wa Wizara ya Elimu kwa kuwa katika Chuo hicho kuna dalili za rushwa.

Waziri pia amemwelekeza Mkandarasi Afrique Enginearing and Construction Company Ltd kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kazi hiyo inakamilika ndani ya mwezi mmoja na kuwa  tayari mkandarasi huyo  ameshalipwa kiasi cha bilioni 2 na milioni 700. 

“Haipendezi viongozi wa umma kila siku kukemea watendaji, kutumbuana kila tunapokutana kwenye majukumu, tunatakiwa tunapokutana tuwe tunakaa na kufurahi lakini kwa mtindo huu wa kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati serikali haitamvumilia mtu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Mkandarasi wa Affrique Enginearing and Construction Company Ltd wakati wakikagua ukumbi wa mihadhara chuoni hapo na kuwa ujenzi wa ukumbi huo haujakamilika.

Profesa Ndalichako amesema kuwa fedha inayotolewa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule ya vyuo ni sumu na endapo itatumika vibaya waliohusika wataitapika fedha hiyo. 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko amemhakikishia Waziri kuwa Uongozi wa Wilaya utasimamia kwa karibu kuhakikisha maelekezo aliyoyatoa yanatekelezwa lakini pia amewataka wakandarasi wababaishaji wabadilike na wasipobadilika basi uongozi wa Wilaya utawabadilisha.
Mwanafunzi Skauti katika Chuo cha Ualimu Shinyanga akimvalisha skafu mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako mara baada ya kupokelewa katika Chuo cha Ualimu Shinyanga.

CHUO CHA MUST CHAPONGEZWA KWA KUSIMAMIA UKARABATI CHUO CHA UALIMU TANDALA VIZURI


Serikali imekipongeza Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) kwa kusimamia kwa ufanisi ukarabati wa Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati akikagua ukarabati wa miundombinu ya Chuoni hapo mradi ambao unafadhiliwa na Wizara hiyo.

 “Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya wamekuwa wakifanya kazi nzuri za kuridhisha katika miradi yao yote waliokabidhiwa na Wizara na hivi ndivyo inavyotakiwa, Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya kurejesha hadhi ya miundombinu ya shule, vyuo na miundombinu mingine zilenge kukamilisha kazi hizo na sio kutanguliza maslahi binafsi na kuingiza Serikali kwenye hasara,” alisema Naibu Waziri Ole Nasha
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiangalia katika picha muonekano wa zamani kabla ya ukarabati na baada ya ukarabati wa miundombinu ya Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe wakati alipotembelea Chuoni hapo kukagua ukarabati uliofanyika.

Naibu Waziri huyo amezitaka Taasisi nyingine za Serikali kuwa waadilifu katika matumizi ya fedha pindi Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia huku akiwataka wanafunzi wa chuo hicho kusoma kwa bidii na kufaulu kwa kiwango cha juu.

Kiongozi huyo ameeleza kuwa Serikali ilisitisha kutoa ajira kwa wingi kwa lengo la kupitia mifumo ya ajira upya kwani iliyokuwepo ilizalisha wafanyakazi hewa na wenye vyeti feki hivyo ilikuwa ni lazima kufanya hivyo ili kuiepusha Serikali kuingia kwenye hasara.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu ya Chuo cha Ualimu Tandala kilichopo Wilaya ya Makete Mkoani Njombe  baada ya ukarabati.

Nae Mkuu wa Chuo cha Ualimu Tandala Philip Khamisi alisema mpaka sasa Chuo hicho kina wanachuo 225 huku wakitegemea kupokea wanachuo 342 ambapo itafanya idadi ya kufika 567.

Wizara ilitoa zaidi ya shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya Chuo cha Tandala ambacho miundombinu yake ilikuwa imechakaa.
Muonekano wa sasa wa mabweni ya wavulana katika Chuo cha ualimu Tandala kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe.

Jumatano, 3 Oktoba 2018

WIZARA YA ELIMU YAVUNJA MKATABA NA MKANDARASI HERKIN BUILDERS LTD


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imevunja mkataba na mkandarasi Herkin Builders anayejenga Chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa kutokana na kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati hali iliyopelekea kuchelewesha utoaji huduma na kuitia Serikali hasara.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametangaza kuvunjwa kwa mkataba huo leo alipofanya ziara katika eneo la mradi na kukuta hakuna kazi inayoendelea zaidi ya kuchimba msingi. 

"Mkandarasi huyu amekabidhiwa kazi Novemba 15, 2016 na alitakiwa akabidhi kazi hiyo Septemba 10, 2017 hajakabidhi Serikali ikamuongezea muda mara mbili lakini hata muda ulioongezwa hakuna atakachofanya, hali halisi inaonekana tunavunja mkataba huu leo,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akipokea taarifa ya Mradi wa ujenzi wa Chuo cha ufundi stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa kutoka kwa Msimamizi wa Mradi Mhandisi Peter Sizya kutoka VETA Makao Makuu.

Ole Nasha amesema hatambui tathmini ya Mradi iliyofanywa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) na kumtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo ndani ya wiki moja kuunda timu ya wataalamu watakaofanya tathmini ya mradi huo.

"Ninyi VETA ndio mmeendelea kusisitiza kupewa kandarasi kwa kampuni hii pamoja na kuonyesha udhaifu katika kazi kadhaa ambazo amewahi kufanya na kuharibu bado ninyi mnafanya tathmini ya mradi hadi ilipofikia jambo hili halikubaliki na kampuni hii haifai kupewa kazi” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.  
 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa kinachojengwa na Mkandarasi Herkins Builders Limited

Awali Mhandisi wa mradi kutoka VETA makao makuu Peter Sizya alimweleza Naibu Waziri tathmini iliyofanyika inaonesha kazi imetekelezwa kwa asilimia 6 ambapo zaidi ya milioni 590 zimetumika kumlipa mkandarasi.


Gharama za ujenzi wa mradi wa chuo hicho ni zaidi ya shilingi bilioni 9 na unagharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa kutumia fedha za mkopo kutoka benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na fedha za ndani.
Muonekano wa sasa wa hatua ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi cha mkoa wa Njombe kilichopo eneo la Shaurimoyo wilaya ya Ludewa.

Jumanne, 2 Oktoba 2018

OLE NASHA AAGIZA KUFANYIKA KIKAO NA TBA KUHUSU UCHELEWESHWAJI WA MIRADI YA WIZARA ELIMU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ametoa wiki moja kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kuitisha kikao cha pamoja na Wakala wa Majengo ya Serikali nchini (TBA) ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu changamoto za utekelezaji wa miradi ya Wizara hiyo inayotekelezwa na TBA.

Naibu waziri ametoa agizo hilo akiwa Mkoani Ruvuma wakati wa kukagua miundombinu katika shule ya Sekondari wasichana Songea ambapo amesema Wizara hairidhishwi na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo hivyo kikao kitakachoitishwa kijielekeze kuona namna bora ya kukamilisha miradi hiyo au ikiwezekana kuvunja mkataba na wakala huyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akikagua miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Wasichana  Songea iliyoko wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

Ole Nasha amesisitiza  kuwa kuchelewa kwa miradi hiyo kunaiongezea gharama zaidi Serikali lakini pia hakutatui changamoto iliyokuwa imekusudiwa.

"Wanafunzi wanapata tabu ya kusongamana wakati tayari Serikali imeliona hilo na kutoa  fedha kwa ajili ya kuboresha  miundombinu hiyo ili waweze kusoma  ninyi leo mnaichelewesha sio sahihi,” alisisitiza Naibu waziri Ole Nasha.

TBA walikabidhiwa mradi wa kukarabati Miundombinu ya shule ya sekondari ya wasichana  Songea Machi 2017  na ulitakiwa kukamilika Septemba 2017  ambapo mpaka leo mradi huo haujakamilika na tayari Wizara imekwishawalipa    TBA shilingi milioni 580 kwa ajili  ya kazi hiyo.  

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na walimu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea mara baada ya kukagua miundombinu ya shule hiyo iliyofanyiwa ukarabati na Wizara. Amewataka walimu kutekeleza majukumu yao kwa weledi lakini pia kuunga mkono juhudi za Serikali inazozifanya katika kuboresha miundombinu ya Shule. 
Kwa upande wake mwakilishi wa TBA mkoani Ruvuma mhandisi Matapuli Juma amekiri kuwapo kwa ucheleweshwaji wa kukamilisha kazi hizo na  kuwa kwa sasa wamejipanga kuhakikisha kazi hiyo inakamilika mapema. 

Naibu Waziri Ole Nasha amekamilisha ziara yake leo mkoani Ruvuma ambapo pia ametembelea Chuo cha Ualimu Songea na kuongea na walimu pamoja na wanafunzi ambapo amewaeleza kuwa serikali inatambua changamoto zilizopo katika sekta ya Elimu na imekuwa ikizishughulikia kila siku ili kuhakikisha Elimu inatolewa katika mazingira mazuri.


Naibu Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiongea na wakufunzi wanaofundisha somo la Fizikia katika Maabara ya somo hilo wakati alipotembelea Chuo cha Ualimu Songea Kilichopo Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma 

KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AMEWATAKA WATENDAJI KUZINGATIA SHERIA KATIKA KUSIMAMIA MIRADI YA SERIKALI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amewataka washiriki wa mafunzo ya Force Akaunti kuhakikisha wanazingatia Kanuni, taratibu na Sheria wakati wa usimamiaji wa ujenzi na ukarabati  wa miradi ya serikali.

Dkt. Akwilapo ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya matumizi ya Force Akaunti yanayofanyika mkoani Morogoro ambayo yameshirikisha  watumishi wa Serikali wakiwemo Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakurugenzi wa kanda VETA, Maafisa Kutoka  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Maafisa kutoka VETA.



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amefunga mafunzo ya Force Akaunti ambapo pia amewataka watendaji kuzingatia taratibu,kanuni na sheria za Fedha.
Katibu Mkuu huyo amewaeleza washiriki hao kuwa utaratibu wa Force Akaunti upo kisheria, hivyo amewasisitiza washiriki kuhakikisha wanakuwa na utunzaji wa kumbukumbu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa risiti za kielektroniki (EFD).



Dkt. Akwilapo  amesema kuwa Force Akaunti ikisimamiwa vizuri inaonyesha thamani ya Fedha, mradi unakamilika na kuwa yote hayo yanawezekana enadapo  ushirikiahwaji na uwazi miongoni mwa Jamii utakuwepo katika eneo ambalo mradi unatekelezwa.


Washiriki wakifuatilia mafunzo ya Force Akaunti yenye lengo la kuwajengea uwezo washiriki namna bora ya kusimamia miradi ya ujenzi na ukarabati yanayofanyika Mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanaratibiwa na mradi wa kukuza Maarifa, Stadi na ujuzi (ESPJ) yamehusisha Wakurugenzi wa halmashauri za Kasulu,Ngorongoro,Kongwa,Nyasa, Wakurugenzi wa  Kanda VETA, Wakurugenzi wasaidizi kutoka Makao Makuu VETA na Maafisa kutoka VETA.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akisindikizwa  na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi Dkt. Noel Mbonde pamoja na mratibu wa mafunzo ya kukuza maarifa, stadi na Ujuzi (ESPJ), Dkt. Keneth Hosea baada ya kufunga mafunzo ya Force Akaunti yaliyofanyika mkoani Morogoro.