Jumatano, 8 Novemba 2017

Katibu Mkuu ataka fedha za tafiti zitumike kama zilivyopangwa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leornard Akwilapo amesema Serikali itahakikisha fedha zilizotolewa  na Serikali ya Sweden kupitia Shirika la Kimataifa la misaada la nchi hiyo (SIDA) zinatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya masuala ya tafiti na kuhakikisha matokeo tarajiwa yanapatikana kikamilifu.

Dkt. Akwilapo ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya miaka 40 ya ushirikiano katika tafiti kati ya Tanzania na Sweden yanayofanyika jijini Dar es Salaam ambapo nchi ya Sweden imetoa zaidi ya bilioni 78 kwa ajili ya kuendeleza masuala ya tafiti kwa kipindi cha 2015 hadi 2020.

Dkt Akwilapo amezitaja taasisi zilizonufaika na zinazoendelea kunufaika na ushirikiano huo kuwa ni Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Chuo Kikuu Ardhi (ARU), Chuo Kikuu cha tiba na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambao wamekuwa wakifanya tafiti katika masuala mbalimbali ya kitaaluma na kijamii. 


Ushirikiano kati ya Tanzania na Sweden umewezesha Tanzania kupata wataalam 455 katika ngazi ya uzamili na 82 katika ngazi ya uzamivu kwa mwaka 1998 hadi 2009 na mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 200 wanaendelea na masomo ya katika ngazi uzamili na wengine 80 katika ngazi uzamivu kutokana na ushirikiano Kati ya nchi hizo mbili.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni