Jumamosi, 20 Januari 2018

TBA yapewa wiki moja kuanza ujenzi kampasi ya Mloganzila

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameipa wiki moja  Wakala wa Majengo nchin- TBA- Kuhakikisha ujenzi wa majengo mbalimbali  unaanza mara moja ikiwa ni pamoja na kuongeza mafundi pamoja na kupeleka vifaa vya ujenzi katika Mradi wa  Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi Muhimbili Kampasi ya Mloganzila.

Prof.  Ndalichako ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa madarasa, hosteli, ofisi na bwalo la Chakula katika Chuo Kikuu hicho kilichopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ambapo amesema hajaridhishwa na kasi ujenzi huo.

Waziri Ndalichako amesema Wizara tayari ilishaipatia TBA kiasi cha shilingi bilioni 3.9 kama malipo ya awali lakini mpaka sasa hakuna jengo lolote ambalo limeshaanza kujengwa na wala hakuna vifaa vya ujenzi katika eneo hilo zaidi ya kuchimbwa misingi tu.

Waziri Ndalichako amesema hatavumilia kuona udahili wa  wanafunzi wa fani za Afya unachelewa katika kampasi hiyo kwa kuwa  lengo la serikali ni kuongeza idadi ya wanafunzi wa fani hizo nchini.


Naye Kaimu Meneja wa Mkoa kutoka TBA Manase Kalage amemwakikisha Waziri kuwa maagizo aliyoyatoa watayatekeleza ikiwa ni pamoja na kukamilisha mradi huo kwa wakati.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni