Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu Sayansi na
Teknolojia Dk.Leonard Akwilapo amewataka Wakuu wa Vyuo vya Ualimu, Maboharia na
Wahasibu wa Wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia taratibu za manunuzi wakati
wote wa ukarabati na ujenzi wa Miundombinu ya vyuo 8 vya Ualimu
unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Dk.Akwilapo amesema hayo leo
mkoani Dodoma wakati wa semina Elekezi kwa watendaji hao juu ya namna bora ya
kutumia Force Akaunti wakati wa ujenzi kwa kutumia wataalamu na vifaa vyake au
kwa kukodi na kutumia mafundi wengine.
Dk. Akwilapo amewasisitiza wakuu
hao wa vyuo vya Ualimu kuhakikisha wanatunza vyema kumbukumbu za matumizi ya
fedha, ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ambazo zitasimamia manunuzi, upokeaji
wa vifaa na matumizi bora ya vifaa hivyo.
Awamu hii ya pili inahusisha Chuo
cha Ualimu Patandi, Tarime, Nachingwea, Murutunguru, Mangaka, Tandala, Ilonga
na Kinampanda ambapo tayari Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia
Programu ya Lipa kulingana na Matokeo imeshatuma fedha za awali
kiasi cha shilingi bilioni 6 kwa ajili kazi hiyo.
Awamu ya kwanza ya ukarabati
ilihusisha Vyuo vya Ualimu 10 ambavyo ni chuo cha Butimba, Mpwapwa,
kleruu, Songea, Kasulu, Tukuyu, Korogwe, Marangu, Morogoro na Chuo cha
Tabora ambapo Wizara ilitumia shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa
Vyuo hivyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.