Alhamisi, 19 Julai 2018

WIZARA YA ELIMU YAKABIDHI MAGARI 47 KWA WADHIBITI UBORA WA SHULE


Wathibiti Ubora wa Shule nchini wametakiwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa taaluma shuleni kwani matokeo bora ya ujifunzaji yanahitaji usimamizi na tathmini ya mara kwa mara.

Hayo yameelezwa leo mkoani Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya kukabidhi magari 45 kwa Wathibiti Ubora wa Shule wa Kanda na Wilaya na magari 2 kwa ajili ya Baraza la Mitihani Tanzania.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji magari kwa Wathibiti Ubora wa Shule Kanda na Wilaya, pamoja na Baraza la Mitihani la Tanzania. Amesisitiza matumizi bora ya magari hayo ili yaweze kutimiza lengo lililokusudiwa.

Waziri Ndalichako amesema lengo la Taifa ni kuwa na watu walioelimika,  mahiri na wabunifu katika  kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo 2025, hivyo ili kufikia malengo hayo  usimamizi wa karibu na tathmini ya mara kwa mara inahitajika.

Waziri Ndalichako amewasisitiza Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanafanya  ufuatiliaji wa karibu wa kitaaluma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  walimu wanafika  shuleni  kwa  wakati  wanaingia  kwenye  vipindi  na wanafundisha.

 “Nataka nione mnasimamia kwa karibu taaluma na nataka  kuona  mabadiliko makubwa katika shule zetu za   Serikali  kuanzia  upande  wa  nidhamu na  taaluma ili mabadiliko yaweze kujitokeza  kwenye Shule zetu,  na tuone shule zetu  zinafanya vizuri katika matokeo ya Taifa ya kidato  cha  Nne,’’ alisisitiza Prof. Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa magari ambayo ameyagawa kwa Wathibiti Ubora wa Shule ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


Profesa Ndalichako ametaka magari hayo kutotumika katika malengo yasiyokusudiwa badala yake yatumike tu kwa ufuatiliaji wa taaluma shuleni.

“Haya ni magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa Elimu, ninaagiza magari haya yasitumike kwa matumizi mengine yoyote tofauti na masuala ya Elimu, naomba hili likazingatiwe sana na yeyote atakayekikuka hatua za kinidhamu  zitachukuliwa,”alisisitiza Waziri Ndalichako.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua moja ya gari lililonunuliwa na Wizara kama nyenzo na kitendea kazi kwa Wathibiti Ubora wa  Shule.



Pia Waziri Ndalichako amewataka Wakuu   wa  Shule  kuendelea  kusimamia  nidhamu  na kutowaonea huruma  wanafunzi wanaokiuka taratibu za Shule  kwani Serikali haitakuwa  na huruma na watendaji pale mambo yatakapokuwa hayaendi vizuri. 

“Angalieni  Mkuu wa Shule ya Sekondari Jangwani ameng’oka  kwa  hiyo  Serikali haitakuwa na huruma nanyi  pale mtakapowalea wanafunzi wenye 
utovu wa nidhamu Shuleni, wanafunzi hawatakiwi kuwa na simu shuleni  lakini bado wanafunzi wameendelea kuwa na simu, hakikisheni mnasimamia maadili na nidhamu za wanafunzi kwa mujibu wa taratibu zinavyoelekeza.

Mapema mwanzoni mwa Mwezi Julai Wizara iligawa pikipiki 2,894  kwa  ajili ya Waratibu Elimu kata ikiwa ni muendelezo wa kutatua changamoto ya usafiri kwaWathibiti Ubora ili wazeze kufikia shule zote na kufuatilia  hali  ya ufundishaji shuleni.
Baadhi ya Magari ambayo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imenunua kwa ajili ya Wathibiti Ubora wa Shule Kanda na Wilaya pamoja na Baraza la Mitihani  Tanzania

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.