Jumatano, 5 Desemba 2018

WAZIRI MKUU MAJALIWA ASISITIZA MATUMIZI YA TEHAMA KATIKA SEKTA YA ELIMU


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) ikitumika vizuri katika sekta ya elimu itasaidia kujenga mazingira mazuri na kuwezesha kuwepo kwa mbinu bora katika ufundishaji na ujifunzaji.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa kauli hiyo jijini Dar Es Salaam katika halfa ya utoaji wa tuzo  kwa washindi wa mashindano ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa mwaka 2018 yaliyoandaliwa na Taasisi ya Huawei Tanzania, na kusisitiza kuwa  kutumia TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji Mwalimu  mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi waliosehemu tofauti.


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa mashindano ya TEHAMA yaliyoandaliwa na Huawei Tanzania Emannuel Chaula kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mhe. Majaliwa amewataka wanafunzi kutumia fursa ya mashindano hayo kuendelea kujifunza TEHAMA ili wewe na  uwezo wa kumiliki mifumo  ambayo itasaidia nchi katika kurahisisha utendaji wa shughuli zake kupitia sayansi na Teknolojia

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inaendelea kuunganisha mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya serikali ya kurahisisha utendaji kazi.

Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Elimu, Sayansi naTeknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka vijana walioshiriki katika mashindano hayo kuendelea kujifunza zaidi kwani nchi bado inahitaji Maendeleo katika kipindi ambacho serikali imekusudia kujenga uchumi wa viwanda.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi mmoja wa washindi wa mashindano ya TEHAMA tuzo katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa washindi wa mashindano ya TEHAMA iliyofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amewataka vijana walioshiriki katika mashindano hayo kuendelea kujifunza zaidi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou amesema kabla ya vijana hao kuingia katika mashindano hayo walipatiwa mafunzo ili kuwawezesha kuzitambua Teknolojia za kisasa kwa kuwa Teknolojia  inakua kila siku.

Mashindano hayo ya TEHAMA yalianza na  vijana  500 lakini mpaka mwishoni vijana 10  tu ndio wamefanikiwa kushinda ambapo washindi watatu wa juu wanatarajiwa kwenda katika nchi za Afrika Kusini na China kwa lengo la kujifunza zaidi masuala ya TEHAMA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa China na Viongozi wa Taasisi ya Huawei Tanzania wakati wa hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa mashindano ya TEHAMA 2018 iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni