Ijumaa, 14 Desemba 2018

SKAUTI WATAKIWA KUJENGA NA KULEA MAADILI MEMA KWA VIJANA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania kuwajenga na kuwalea vijana katika maadili mema ya kitanzania .

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo wakati wa hafla ya kumkabidhi Balozi Nicholas Kuhanga tuzo ya Elephant Award aliyotunukiwa na Chama cha Skauti Kanda ya Afrika iliyofanyika jiji Dar es Salaam ambapo amesema tuzo hiyo inatolewa ili Kutambua huduma iliyotukuka na mchango wa balozi huyo  katika maendeleo ya shughuli za Skauti barani Afrika.

“Ninawapongeza Viongozi wote wa Chama kwa kujenga na kulea maadili mema, na kwa juhudi zenu katika kupambana na mmomonyoko wa maadili ili kujenga taifa lenye wazalendo watakao iletea nchi maendeleo ya kweli” alisisitiza Waziri Ndalichako
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimvisha nishani ya tuzo ya Elephant Award Balozi Nicholas Kuhanga aliyotunukiwa na Chama cha Skauti Kanda ya Afrika katika hafla ya kumkabidhi iliyofanyika jiji Dar es Salaam.

Waziri Ndalichako amesema Balozi Kuhanga ameiweka nchi katika kumbukumbu ya kihistoria katika ngazi ya Skauti Kanda ya Afrika kwa kuwa  tuzo aliyopata ina hadhi ya juu kuliko zote ndani ya Skauti Kanda ya Afrika, hivyo mchango wa Balozi Kuhanga ni wa kujivunia na ni mfano wa kuigwa, hasa kwa vijana ambao ni viongozi wa baadae.

Akizungumza katika hafla hiyo Kamishna Mtendaji wa chama hicho Eline Kitaly amesema Balozi Kuhanga amekuwa kiongozi wa mstari wa mbele katika shughuli za skauti, na hata alipostaafu kazi serikalini ameendelea kuwa kiongozi wa Skauti anayefundisha maadili mema kwa skauti pamoja na Viongozi waSkauti Tanzania.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimpatia zawadi Balozi Nicholas Kuhanga iliyotolewa na Chama cha Skauti Tanzania wakati wakuadhimisha miaka 100 ya skauti nchi, zawadi hizo zimekabidhiwa leo jijini Dar es Salaam. 

Kwa upande wake Balozi Nicholas Kuhanga ameishukuru Serikali ya Tanzania  kwa kumpatia elimu iliiyomwezesha  kufanya kazi zake kwa umakini na pia aliwashukuru watumishi wa skauti kwa ushirikiano waliompa mpaka kufikia hatua ya kupata tuzo hiyo.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni