Ijumaa, 14 Desemba 2018

UINGEREZA NA CANADA KUENDELEA KUSAIDIA SEKTA YA ELIMU


Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia zimekubalina kuendelea kuimarisha programu za  Mpango wa Elimu kwa walioikosa (MEMKWA) na Mpango wa Elimu Jumuishi baada ya Kumaliza elimu msingi (IPPE), ili kuwezesha wanafunzi wanaokatisha masomo kabla ya kumaliza shule waweze kuendelea na masomo yao.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Afrika Mashariki na Kusini kutoka nchini Canada Mars Andre Fredette aliyeambatana na Balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O Donnell ambao wote kwa pamoja wamejadili masuala mbalimbali pamoja na nchi hiyo kuendelea kuisaidia Tanzania katika  Sekta ya Elimu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mkuu wa DFID Tanzania Beth Arthy aliyefika kwenye ofisi za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zilizopo jijini  Dar es Salaam kujadili masuala mbalimbali kuhusu sekta ya  Elimu
Waziri Ndalichako amesema nia ya serikali ni kuona kila mtoto wa kitanzania anayepaswa kupata elimu anaandikishwa na kubaki shule mpaka anapomaliza masomo yake ingawa kumekuwepo na Changamoto ya baadhi wa wanafunzi kukatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali.

 “Ukitembea barabarani unakutana na watoto wadogo wakifanya biashara ndogondogo unapoongea nao wanakwambia wameacha shule ili kusaidia wazazi kufanya biashara hizo, wengine utawakuta wapo mashambani wanawasaidia wazazi kulima hivyo changamoto ya watoto kukatisha masomo ni kubwa, na ndiyo maana serikali inaona namna bora ya kuhakikisha wale wote wanaokatisha masomo wanajiendeleza”alisisitiza waziri Ndalichako

Waziri Ndalichako amesema programu ya MEMKWA inamwezesha mtoto ambaye hakwenda shule kabisa kusoma na kisha kufanya mtihani wa darasa la nne na baadaye anapofaulu huandikishwa katika  mfumo rasmi na kuendelea na masomo kama wanafunzi wengine wakati mfumo wa IPPF ni kwa ajili ya wanafunzi wanaokatisha masomo ya sekondari  unawawezesha kumaliza masomo hayo na kuendelea na elimu juu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akijadiliana na Mkurugenzi Mkuu wa Afrika Mashariki na Kusini kutoka Canada Mars Andre Fredette aliyeambatana na Balozi wa Canada nchini Tanzania Pamela O Donnell ambao kwa pamoja wamejadiliana namna bora ya kuboresha elimu nchini Tanzania.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Afrika Mashariki na Kusini kutoka Canada Mars Andre Fredett amesema Canada inajivunia uhusiano wa muda mrefu uliopo katika ya Tanzania na Canada ambao umewezesha nchi kupata misaada mbalimbali ya kuendeleza sekta ya elimu ambayo imewezesha watoto wa kike na kiume kupata elimu bora pamoja na kutoa mafunzo kwa walimu.

Waziri wa Elimu pia amefanya mazungumzo na Balozi wa Finlanda nchi Pekka Hukka na Mkuu wa Dfid Tanzania Beth Arthy ambao wamezungumzia masuala mbalimbali ya namna bora ya kuboresha elimu nchini ikiwepo masuala ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu bora kwa kila mtoto wa kitanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni