Makubaliano hayo yamefanyika
mkoani Dodoma ambapo kwa upande wa Tanzania Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako ndiye aliyetia saini makubaliano hayo huku
nchi ya Sudan Kusini ikiwakilishwa na Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Deng Deng
Hoc Yai.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako (Tanzania) na Waziri wa Elimu Deng Deng Hoc (Sudan Kusini)
wakitiliana saini makubaliano ya kushirikiana katika masuala mbalimbali
yahusuyo Elimu katika nchi hizi mbili.
Waziri Ndalichako amesema
makubaliano yanalenga kufungua fursa katika nchi hizo mbili, na kuwa Tanzania
iko tayari kuhakikisha inaisaidia nchi ya Sudan Kusini kufikia malengo waliyojiwekea.
“Tukio hili ni muhimu,
ambapo nchi ya Sudan Kusini wameomba ushirikiano katika sekta ya Elimu na kuwa
Tanzania tunaihakikishia nchi hiyo
ushirikiano kwa kuchapisha vitabu vya somo la Kiswahili, Tanzania pia iko
tayari kwa walimu wa Kiswahili kwenda
Sudan kufundisha somo hilo pia nchi hizo mbili zitaweza kubadilishana uzoefu
katika eneo la mafunzo ya ufundi stadi," alisema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako (Tanzania) na Waziri wa Elimu (Sudan Kusini) Deng Deng
Hoc wakionesha mkataba wa makubaliano unaohusu ushirikiano katika sekta ya
elimu ambapo wote kwa pamoja wamekubaliana kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano
kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake Waziri wa
Elimu wa Sudan Kusini Deng Deng Hoc Yai ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa
kuendelea kudumisha umoja na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili huku akisisitiza
kuwa Tanzania ni nyumbani.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa
hafla ya utilianaji saini wa makubaliano ya mashirikiano katika masuala
mbalimbali yahusuyo elimu. Amesema makubaliano hayo yanalenga kufungua fursa
kwenye sekta ya elimu katika nchi hizo mbili ikiwa ni pamoja na kubadilishana
uzoefu na ujuzi.
Waziri Deng Deng amesema kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha zinazoweza kushindanishwa na lugha nyingine za kimataifa kama vile Kingereza na Kiarabu hivyo nchi hiyo imeona umuhimu kwa shule zao kuanza kufundisha lugha ya kiswahili shuleni.
Waziri
wa Elimu Tanzania na Waziri wa Elimu Sudan Kusini wakifurahia jambo baada
ya kutiliana saini makubaliano ya
ushirikiano katika masuala mbalimbali
kwenye sekta ya elimu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.