Ijumaa, 15 Februari 2019

SERIKALI YABAINISHA MIKAKATI YA KUZUIA MIMBA NA NDOA ZA UTOTONI

Serikali imesema inaendelea na mkakati wa kujenga mabweni katika shule mbalimbali za Sekondari hapa nchini ambazo ni za kutwa ili kuepusha watoto wa kike kupata mimba pamoja na kuzuia ndoa za utotoni.

Kauli ya Serikali imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole Nasha wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Girls Inspire Tanzania wenye lengo la kuzuia ndoa za utotoni uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Wiliam Ole Nasha akizungumza na wadau wa Elimu (Hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Girls Inspire Tanzania wenye lengo la kuzuia ndoa za utotoni Jijini Dar es Salaam

Naibu Waziri huyo amesema tatizo la ndoa za utotoni ni kubwa katika nchi nyingi hali ambayo inasababisha watoto wa kike kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu na kusababisha Taifa  kukosa wataalamu.

“Ndoa za utotoni zinafanya mtoto wa kike asisonge mbele katika safari yake ya elimu  na ndio maana serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali   kuhakikisha tunazuia ndoa za utotoni na kuweka mazingira wezeshi ya kuwafanya watoto wa kike waendelee kubaki shuleni kupata elimu,” alisema Mhe. Ole Nasha.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi wa wadau wa elimu waliohudhuria mkutano wa mkutano wa kimataifa wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Girls Inspire Tanzania.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya na Wizara ya Elimu zinashirikiana kuhakikisha shule za msingi na sekondari zinakuwa na Walimu ambao watasaidia kutoa ushauri nasaha kwa wanafunzi kufahamu namna ya kujizuia kuingia katika  ndoa na mimba za utotoni.

Mradi wa Girls Inspire Tanzania una lenga kuzuia ndoa za utotoni unatekelezwa katika nchi za Tanzania, Msumbiji, Bangladesh, India na Pakistani na kufadhiliwa na na serikali za Canada na Australia ambapo kwa Tanzania umatekelezwa na Taasisi ya Elimu ya Watu wazima na Shirika lisolo la Serikali Kiota Women Health and Development, (KIHOWEDE).

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akiwa na  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, Balozi wa Canada O’Donnell na Mwenyekiti wa Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania Dkt. Naomi Katunzi wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wa katika mkutano wa kimataifa wa kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mradi wa Girls Inspire Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.