Jumatatu, 10 Februari 2020

CANADA YATOA ZAIDI YA BILIONI 90 KWA AJILI YA KUBORESHA ELIMU YA UALIMU

Serikali ya Canada imetoa zaidi ya bilioni 90 kwa Tanzania zitakazotumika kuboresha elimu ya ualimu nchini.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo  wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kupitia na kutathmini utekelezaji wa Mradi wa Kuendeleza Elimu nchini (TESP) ambapo amesema mradi huo pia umewezesha kuinua kiwango cha ubora wa elimu katika shule za msingi na sekondari kwa kuzalisha rasilimali watu yenye ubora.
.
Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza na wadau wa Elimu ya Ualimu (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kupitia na kutathimini Mradi wa Kuendeleza Elimu ya Ualimu (TESP) Jijini Arusha
Dkt. Akwilapo amesema Canada kupitia TESP imetoa fedha hizo ambazo zimetumika katika kuvijenga upya baadhi ya vyuo vya ualimu, kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia  pamoja na kutoa mafunzo kazini kwa  walimu.

Kansela Mkuu, Ushirikiano na Maendeleo kutoka Canada Gwen Walmsely akizungumza na wadau wa Elimu ya Ualimu jijini Arusha
Kiongozi huyo amesema kuwa Ushirikiano wa Tanzania na Canada unalenga kuongeza uwezo wa vyuo vya ualimu kufundisha walimu waliobobea watakaofundisha vizuri katika shule mbalimbali.

“Tunatoa shukrani nyingi sana kwa serikali ya Canada na Kitengo chao cha Global Affairs ambacho kinasimamia mradi huu, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia mradi huu na matokeo yameshaanza kuonekana," amesisitiza Katibu Mkuu Akwilapo.

Dkt. Akwilapo amesema mafanikio  ya mradi huo yameanza kuonekana ambapo walimu wameongeza uwezo katika ufundishaji na matumizi ya TEHAMA katika kufundisha.

Kansela Mkuu, Ushirikiano na Maendeleo ​kutoka Canada Gwen Walmsley amesema kuwa Canada itaendelea kutoa fedha zaidi katika kuboresha sekta ya elimu nchini na mradi huo ni moja kati ya juhudi wanazozifanya katika kuunga mkono serikali ya Tanzania katika jitihada za  kuboresha elimu.

Gwen ameipongeza Tanzania kwa kufanya Sekta ya Elimu kipaumbele ili  kuhakikisha watoto wote wanapata elimu, suala ambalo limewezesha zaidi ya watoto milioni 10.6 kujiunga na elimu ya msingi na sekondari

Mratibu wa Mradi wa kuendeleza Elimu​ ya Ualimu TESP kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Ignas Chonya amesema kuwa mradi huo umewawezesha walimu kuboresha mbinu za ufundishaji kupitia Tehama ambapo vyuo 35 vya ualimu vimeanganishwa na mfumo huo na wanatarajia kuunganishwa na mkongo wa Taifa.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.