Jumamosi, 8 Februari 2020

MKUTANO WA WATUMISHI WA WIZARA WALIOKO MAKAO MAKUU


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo amesema utumishi wa umma una sheria, kanuni, taratibu, maadili na miiko ya kiutendaji ambayo kila mtumishi anapaswa kuielewa na kuzingatia katika utendaji kazi.
 
Katibu Mkuu Akwilapo amesema hayo wakati wa Mkutano  wa Wafanyakazi wa kutathmini utendaji wa Wizara katika kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2019 ambapo amesema ni vizuri kila mtumishi akazingatia taratibu hizo ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Amesema pamoja na kuzingatia sheria hizo ni vizuri tukafanya kazi kwa kushirikiana na kuelekezana ili kupata matokeo chanya katika utekelezaji wa majukumu.

Kiongozi huyo amepongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili kufikia malengo makubwa ya Wizara ambayo ni kutoa Elimu bora nchini.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. AveMaria Semakafu amesema ni vizuri watumishi wakaendeleza kasi liyopo sasa ya utendaji huku wakizingatia utendaji wenye viwango ili sekta ya Elimu iendelee kufanya vizuri.

Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Wizara Bwana Nicholaus Moshi ameupongeza Uongozi wa Wizara kwa namna unavyoweka mazingira wezeshi ya utoaji Elimu kwa  kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu, kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kuhakikisha uwepo wa vitendea kazi pamoja na ujenzi wa ofisi zikiwemo za Wathibiti Ubora wa shule na ukarabati na upanuzi wa  Vyuo  ya Ualimu.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni