Ijumaa, 25 Julai 2014

AWAMU YA PILI KUCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA TANO

Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili kwa wanafunzi waliobaki kutokana na ufinyu wa nafasi za shule za kidato cha tano, baada ya kubaini uwepo wa nafasi hizo; na baadhi ya wanafunzi wenye sifa watachaguliwa kwenda kusomea ualimu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa  Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),  Bwana Jumanne Sagini alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari tarehe 22/07/2014  jijini Dar es salaam juu ya wanafunzi waliofaulu masomo ya sayansi.

Serikali kwa kutambua umuhimu wa masomo ya sayansi na mwitikio chanya uliopo sasa kwa wanafunzi kusoma masomo hayo, imeendelea kuimarisha miundombinu ya shule kwa kutoa fedha za ujenzi, ukamilishaji na ukarabati wa majengo ili wanafunzi wengi zaidi waweze kusoma masomo ya sayansi.

Bwana Sagini alisema wanafunzi ambao wamefaulu vizuri masomo ya sayansi na wanapenda kusoma masomo hayo wanayo fursa ya kubadilisha tahasusi (Combination) endapo zinapatikana kwenye shule walizopangwa kupitia kwa wakuu wao wa shule.  Iwapo tahasusi wanazozitaka hazifundishwi kwenye shule hizo wanaweza kuwasilisha maombi yao kwa Maafisa Elimu Mikoa ambayo shule hizo zipo kupitia kwa wakuu wa shule walizopangiwa ili waweze kubadilishiwa tahasusi za sayansi kwenye shule zilizopo kwenye Mikoa husika.

“Jamii inaweza kuwasiliana na watendaji wa wizara na Mikoa kwa simu ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya waziri Mkuu- TAMISEMI. Hivyo, naendelea kuwasisitiza watendaji wote wa Elimu hususani Wakuu wa Shule na Maafisa Elimu Mikoa kusimamia utekelezaji wa suala hili. Lengo la Serikali ni kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ili kuendana na Malengo ya Milenia na kutekeleza Mpango wa BRN.”alisema Katibu Mkuu.

Serikali inaendelea kusisitiza kila mwanafunzi kwenda kuripoti shule aliyopangiwa kuanzia tarehe 10-30 Julai, 2014, orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha Tano mwaka 2014 inapatikana katika tovuti za www.pmoralg.go.tz na www.moe.go.tz

Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa wataalamu katika fani za sayansi kwa kujiwekea mkakati wa kuhakikisha kuwa kila Mwanafunzi aliyefaulu masomo ya sayansi anapangiwa tahasusi ya masomo ya sayansi.

Katika matokeo ya mtihani kwa mwaka 2014, inaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 22,685 kati yao wasichana 7,859 na wavulana 14,826, wamechaguliwa kusoma tahasusi za sayansi ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi 18,746 kati yao wasichana 5,038 na wavulana 13,708 kwa mwaka 2013.

Uchaguzi wa wanafunzi kidato cha tano kwa mwaka 2014, ulifanyika mwezi mei, 2014 na matokeo yake kutangazwa kupitia tovuti ya OWM-TAMISEMI mwezi Juni 2014.Tofauti na miaka mingine iliyopita, Ufaulu wa watahiniwa wa shule kwa mwaka 2013 katika madaraja ya I-III umeongezeka kutoka watahiniwa 35,357 mwaka 2012 hadi 71,527 mwaka huu. Ufaulu huu ni zaidi ya asilimia mia moja ya watahiniwa waliokuwa na sifa za kuendelea na masomo ya kidato cha tano mwaka 2013.


Matokeo haya  yanakaribia sana malengo ambayo Serikali imejiwekea kupitia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (yaani Big Results Now-BRN) ambapo serikali ilijiwekea lengo la kuhakikisha wanafunzi wanafaulu kwa asilimia 60 mwaka 2013. Matokeo halisi yanaonyesha kuwa ufaulu umepanda kutoka asilimia 43 mwaka 2012 hadi asilimia 58.25 mwaka 2013.

Yapo manufaa mbalimbali ambayo yatapatikana kutokana na ufaulu huu wa wanafunzi kwa taifa na kwa wanafunzi husika. Kwa taifa ufaulu katika masomo ya sayansi utasaidia kupunguza uhaba wa wataalamu katika fani mbalimbali  za sayansi na pia unarahisisha kazi ya kuwapatia wanafunzi nafasi mbalimbali za kujiendeleza katika masomo ya ngazi ya juu.

Jumatatu, 21 Julai 2014

Kuweni Wabunifu Zaidi - Prof. Mchome

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome amewataka Watumishi wa Wizara hiyo kuwa wabunifu zaidi na kuhakikisha kuwa wanachokibuni kiwe kinatekelezwa na kuchukua hatua kwa wasiotekeleza maelekezo ya kisera pamoja na kuwazawadia wanaotekeleza kwa ufanisi maelekezo yanayotolewa.

“Watumishi wa Wizara hii tunatakiwa tujiulize tunafanya ubunifu gani ili kuhakisha wahitimu katika ngazi mbalimbali wanapata maarifa yanayotakiwa na wanaoweza kusaidia nchi katika kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali,” alisema Profesa Mchome.

Profesa Mchome alikuwa akizungumza na Watumishi wa  Makao Makuu na Taasisi zilizoko chini ya Wizara hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (Julius Nyerere International Convention Centre), Ijumaa 18 Julai, 2014 ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na watumishi hao na kujadiliana namna bora zaidi ya kuboresha utendaji kazi katika wizara.

Aidha, Profesa Mchome alizungumzia umuhimu wa kuboresha Muundo wa Wizara hiyo ili kuwezesha namna bora ya kutekeleza majukumu yake baada ya ugatuaji wa uendeshaji na usimamizi wa shule za Sekondari kwenda kwenye Halmashauri chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na kwa kufuata Hati Idhini iliyounda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi iliyotolewa na Mheshimiwa Rais, Desemba 2010.





Jumatano, 16 Julai 2014

Maadhimisho ya wiki ya Elimu (Video)

Jarida La Maadhimisho ya wiki ya Elimu

Waziri Mhagama akagua utekelezaji wa STHEP

Naibu  Waziri  wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi amefanya  ziara  ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu (Science, Technology and Higher Education Project - STHEP) katika  Chuo Kikuu  Huria  cha Tanzania (OUT) na Chuo  Kikuu Kishiriki cha  Elimu Dar es salaam (DUCE) ambapo amejionea mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa Mradi huo.

Mafanikio hayo ni pamoja na majengo mbalimbali yaliyojengwa, vifaa vya kufundishia na kujifunzia, magari yaliyonunuliwa na Wahadhiri waliosomeshwa katika ngazi ya Shahada ya Uzamili na Uzamivu kupitia mradi huo.

“Kutokana  na kukamilika  kwa Mradi huo  katika awamu ya kwanza, Watanzania  wategemee  mabadiliko  makubwa  katika  sekta ya  Elimu  na kutoa  ubora  wa  Elimu  na  sasa tunakamilisha taratibu za kuanza  kwa awamu ya  pili  ya mradi huo  ambapo pia  tutawasomesha  walimu,” alisema Mhe. Mhagama.





Jumanne, 15 Julai 2014

WIZARA YA ELIMU KUKAMILISHA SERA YA ELIMU NA MAFUNZO 2014

 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inakamilisha sera ya Elimu na Mafunzo 2014  kwa kuingiza maboresho  yaliyotolewa kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri mapema mwezi Juni 2014.

Viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao kazi cha kuingiza maboresho  katika Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo 2014 yaliyotolewa kwenye Kikao cha Baraza la Mawaziri mapema mwezi Juni 2014

Jumatano, 2 Julai 2014

MABORESHO YA UKUSANYAJI WA TAKWIMU ZA ELIMU

Wizara ya  Elimu na  Mafunzo ya  Ufundi  yakutana na Wadau  wa Elimu  kujadili  namna  ya kuboresha  ukusanyaji wa Takwimu  za kielimu katika  Sekta ya  Elimu.
Wadau waliokutana ni pamoja na  Ofisi ya Waziri Mkuu -TAMISEMI,  Wizara ya  Maendeleo  ya Jamii, Jinsia na Watoto, Wizara ya Fedha ,e-Government Agency, UNESCO,USAID,TENMET, SIDA, MOF, AGILE na Data Vision.