Jumanne, 10 Oktoba 2017

Mradi wa TEHAMA wazinduliwa Mkoani Pwani


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo amezindua mradi wenye thamani ya  zaidi ya shilingi bilioni 4 wa ujifunzaji na ufundiashaji wa TEHAMA kwa shule za Sekondari.
Akizindua mradi huo mkoani Pwani hii leo Dkt. Akwilapo amsema Serikali inahitaji kuona mradi huu unakuwa  endelevu na usiishie katika mkoa wa Pwani pekee bali usambae kwa nchi nzima.
Pia amewataka waratibu wa mradi huo - gesci -  kuhakikisha mpango huu unafanikiwa kwa kushirikisha  wadau wote wa Elimu ili mradi  ufanikiwe.
Dkt. Akwilapo amesema TEHAMA ni nyenzo muhimu katika ulimwengu wa mawasiliano, na kwa sasa ndiyo nyenzo kuu ya utoaji na usambazaji wa taarifa kwa umma.
Katibu Mkuu Akwilapo amewataka wale wote wenye miradi au mipango ya namna hiyo wawasiliane na wizara ili miradi yao iweze kuratibiwa na  kutekelezwa kwa taratibu za Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mradi huo unatekelezwa katika baadhi ya nchi za Afrika ikiwemo Tanzania, Kenya, na Cotedvoire





Jumatatu, 9 Oktoba 2017

VIONGOZI WA WIZARA YA ELIMU,SAYANSI NA TEKNOLOJIA WAAHIDI KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema kuwa kitendo cha Rais  John Magufuli kumbakisha kwenye Wizara hiyo ni sawa na kumchagua upya,  hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii.

Waziri Ndalichako amesema hayo wakati akimkaribisha Naibu waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ambaye ameapishwa leo kuitumikia Wizara  hiyo.
 
Wakati akizungunza na Watumishi wa Wizara hiyo Naibu Waziri  Ole Nasha amesema  katika utumishi wake anaamini katika mambo manne ambayo ni uadilifu na uaminifu,  kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na ushirikiano ili kutimiza malengo ya Kitaifa.

 Ole Nasha amesema hayo muda mfupi baada ya kupokelwa na watumishi wa Wizara hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano katika kuendeleza Sekta ya Elimu.




Alhamisi, 5 Oktoba 2017

Waziri Ndalichako azindua Bodi ya Wakurugenzi HESLB na Baraza la TET

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknnolojia Prof. Joyce Ndalichako amelitaka  Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania na Bodi ya wakurugenzi ya Bodi ya mikopo ya Wanafunzi  wa elimu ya juu kufanya kazi kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu za kazi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa bodi hizo ambapo amezitaka pia kuhakiksha zinarudisha hadhi ya Taasisi  za serikali wanazozisimamia katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuweka miongozo ya utendaji kazi na kuhakikisha wanaisimamia miongozo hiyo ili kuleta ufanisi katika kazi.

Ndalichako amezitaka bodi hizo kuhakikisha zinatembea katika ahadi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli za kuhakikisha zinawasaidia wanyonge kupata Elimu bora.

Waziri Ndalichacho amelitaka Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania kuhakikisha vitabu vyote vyenye makosa vinarekebishwa na kwamba bodi ijiridhishe na mfumo na utaratibu utakaotumika katika kuvirekebisha vitabu hivyo.

Baraza hili ambalo litahudumu kwa miaka mine (4) kuanzaia septemba 2017 hadi septemba 2021 limetakiwa pia kusimamia Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma vizuri kwa sababu kumekuwa na upotoshaji kuhusiana na Taasisi lakini pia amewataka kuhakikisha kunakuwa na vipindi vya kuelimisha namna Taasisi inavyotekeleza majukumu yake. 


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Elimu Tanzania Profesa Bernadetta Kilian amesema atahakikisha Taasisi inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwamba maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi ili kukidhi matarajio ya watanzania. 




Jumanne, 26 Septemba 2017

MBINU ZA KUFUNDISHIA ZIMEPUNGUZA UTORO - KKK MKOANI SINGIDA

Walimu wanaofundisha darasa la awali hadi la tatu katika shule ya msingi Nyerere, Mughanga na shule ya wanafunzi wenye mahitaji Maalumu Ikungi zote zilizopo mkoani Singida wameeleza kuwa  mbinu za kuimba, kucheza, kujifunza kwa kushirikisha wanafunzi zinawasaidia wanafunzi kuelewa kwa haraka pamoja na kuwa na umahiri wa  kusoma na kuandika na kuhesabu.

Akizungumza na timu ya wanahabari walio katika ziara ya kufuatilia hali ya ufundishaji na ujifunzaji wa KKK na kuangalia hali ya uboreshaji wa miundombinu mkoani humo Mwalimu Salome Kyomo amepongeza jitihada za serikali za kuwapatia walimu mafunzo ya KKK kwa kuwa mbinu na zana za kufundishia zimeboreshwa.


Kwa upande wake mratibu wa taaluma wa  shule ya msingi Nyerere Lisu Mnyambi amesema shule hiyo ilipokea kiasi cha shilingi Milioni 192 kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Programu ya Lipa kulingana na matokeo. ambazo zimetumika kujenga vyumba vya madarasa 8, ujenzi wa matundu ya vyoo na hivyo kupunguza  msongamano wa wanafunzi madarasani.

Walimu wa shule ya Msingi Mughanga mkoani Singida  wakiwa kwenye moja ya darasa la Pili ambalo mbinu mbalimbali za kujifunzia na kufundishia , (KKK) zipo katika darasa hilo.


Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nyerere iliyopo mkoani Singida ambayo imejengwa na fedha zilizotolewa na  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Program ya lipa kulingana na Matokeo, (P4R)


Mwanafunzi wa darasa la Pili katika Shule ya Endeberg iliyopo Manyara vijijini akisoma kile kilichoandaliwa na Mwalimu wake huku wanafunzi wengine wakimsikiliza. Lengo la Mwalimu hapo ni kujua wanafunzi wake wanaelewa kile alichowafundisha.

KKK NA UBORESHAJI MIUNDOMBINU GEITA

Mkuu wa mkoa wa Geita Meja Jenerali Ezekiel Kyunga amesema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu unaotekelezwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia  programu ya Lipa kulingana na Matokeo ( P4R ) umepunguza changamoto ya uhaba wa madarasa uliokuwa unaukabili mkoa huo kutokana na kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa wazazi wa kuandikisha watoto kujiunga na darasa la kwanza.

Kyunga amesema mkoa huo ulipatiwa kiasi cha shilingi milioni 194 kutoka Programu ya P4R ambazo zimejenga madarasa Nane, kuweka umeme shuleni hapo na uchimbaji wa  kisimana hivyo kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji.


Shule za msingi zilizotembelewa ni pamoja na Nguzombili,   Kalangalala ambazo zina madarasa ya awali mpk darasa la tatu, (madarasa yanayoongea)pamoja na kituo cha wanafunzi wenye mahitaji maalumu  kilichopo kwenye shule ya Mbugani.

Mwanafunzi wa  darasa la kwanza wa Shule ya msingi kalangalala iliyopo mkoani Geita akisoma ubaoni mbele ya wanafunzi wenzako pale alipotakiwa kufanya hivyo na Mwalimu wake. Hii ni kufuatia ziara ya Maafisa wa kitengo cha mawasiliano Wizarani pamoja na wanahabari ambao wanafuatilia ujifunzaji na ufundishaji wa KKK.


Programu ya Lipa kulingana na matokeo imesaidia kupunguza changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nguzo mbili, iliyopo mkoani Geita pia shule hiyo umeweza kuweka umeme na kuchimba kusoma na hivyo kutatua changamoto ya maji shuleni hapo


Moja ya darasa linaloongea lililopo kalangalala, mkoani Geita ambalo hutumiwa na wanafunzi wa awali shuleni hapo. Kuanzishwa kw mtaala wa KKK kumewafanya wanafunzi kupenda shule, imesaidia kupunguza utoro kwa wanafunzi na pia imechangia ufaulu wa wanafunzi.

TATHMINI YA MWAKA 2016, P4R

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na OR - TAMISEMI kwa kushirikiana na Washirika  wa maendeleo leo wamekutana mjini Dodoma kufanya Tathmini  ya utekelezaji wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo ( EP4R)  kwa mwaka 2016/17 ili kuona mafanikio yaliyopatikana, changamoto na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zilizopo katika suala la utoaji wa Elimu bora Nchini.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Mratibu wa Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo  Gerald Mweli kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema programu hiyo inafanya tathmini ili kujua hali halisi ya utekelezaji wa majukumu, kwa kiasi gani mradi umefanikiwa lakini pia kuona changamoto na namna ambavyo serikali kwa kushirikiana na washirika wa watakavyozitatua.

Mweli ametaja  mafanikio yaliyopatikana kupitia mradi huo,kuwa ni pamoja na  kujenga na kukarabati  miundombinu chakavu ya shule za Msingi na Sekondari zipatazo 361 kutoka katika Halmashauri 129, vyumba vya mdarasa 1,435, mabweni 261, majengo ya utawala 11, mabwalo 4, vyoo 2,832, nyumba za walimu 12, maktaba 4, na uwekaji wa maji katika shule nne (4).

Kwa upande wa vyuo vya ualimu programu imefanikiwa kukarabati  vyuo 10 vya ualimu ikiwa ni pamoja na kununua  compyuta 260 zitakazowawezesha walimu  kutekeleza  majukumu yao kwa urahisi, magodoro 6,730 yatakayotumiwa na wanafunzi pamoja na viti 1976 kwa ajili ya wanachuo.


Aidha, programu imenunua vifaa vya maabara 1,696 kwa ajili ya shule za sekondari ambavyo zitasaidia katika ufundishaji wa masomo ya sayansi na kuongeza uelewa kwa wanafunzi.