Chuo cha Ufundi Arusha chatakiwa
kukamilisha ukarabati ili kuwezesha vifaa vilivyonunuliwa kutumika.
Naibu
waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amekitaka chuo cha
Ufundi cha Arusha kukamilisha ukarabati na upanuzi wa karakana zake ili
kuwezesha vifaa vya kisasa vilivyonunuliwa vianze kutumika.
Naibu
waziri Ole Nasha ametoa agizo hilo alipofanya ziara katika Chuo hicho kilichopo
mkoani Arusha ili kujionea utendaji kazi, ambapo amesisitiza kuwa serikali ya
awamu ya tano imejielekeza katika kuboresha elimu ya ufundi ili kufikia malengo
ya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Ole
Nasha amesema kutokana na umuhimu huo serikali nimeamua kuwekeza katika
uboreshaji wa vyuo vinavyotoa Elimu ya ufundi kwa kununua vifaa vya
kisasa na kukarabati miundombinu ya vyuo hivyo ili viweze kuzalisha raslimali
watu watakaowezesha nchi kujenga uchumi wa viwanda.
Naibu
waziri amesema chuo hicho kimepata vifaa vya kufundishia na kujifunzia vya
kisasa vilivyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 14 kutoka nchini Australia
ikiwa ni sehemu ya jitihadi zinazofanywa na serikali ya kuboresha namna
ya utoaji wa elimu ya Ufundi kwa lengo kusaidia kuzalisha vijana wengi wenye taaluma
ya kisasa katika ufundi.
Ole
Nasha amevitaka vyuo vyote vya ufundi kutambua kuwa vina jukumu kubwa la
kuwatengeneza vijana watakaokuwa na weledi na umahiri katika kuchangamkia fursa
za kazi zitakazokuwa zikipatikana katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Kwa
upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo Dkt. Erick Mgaya amesema vifaa vya kisasa
vilivyonunuliwa vitawezesha kurahisisha zoezi zima la ujifundishaji na
ujifunzaji kutokana na kuongezeka kwa udahili.