JAMHURI YA
MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA
ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Anwani
ya Simu: “ELIMU”
DAR
ES SALAAM
Simu:
0262963533,
Tovuti:www.moe.go.tz
|
|
Chuo cha Masomo ya Biashara na Sheria,
Chuo Kikuu cha Dodoma
S. L. P. 10
40479 DODOMA
|
TAARIFA KWA UMMA
Ndugu
Wanahabari,
Kama
ambavyo wengi wenu wanafahamu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inaendelea
na programu yake ya ukarabati mkubwa wa shule kongwe za Sekondari nchini. Programu
ambayo itahusisha jumla ya shule kongwe 89. Katika awamu hii ya kwanza ambayo
imetekelezwa kwa miaka miwili sasa, yaani mwaka wa fedha 2016/17 na 2017/18,
jumla ya shule 46 kati ya 89 zipo kwenye mpango wa ukarabati huu. Taarifa ya
programu hii ya ukarabati ni kama ifuatavyo:
- Shule 10 za sekondari ambazo ni Mpwapwa, Musoma Ufundi, Mtwara Ufundi,
Ifakara, Kantalamba, Tanga Ufundi, Ifunda Ufundi, Moshi Ufundi, Bwiru Wavulana
na Kibiti zinaendelea kukarabatiwa kwa usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi
na Teknolojia cha Mbeya (MUST). MUST ni taasisi ya kielimu, kwa hiyo wamekuwa
makini sana na ratiba za shule. Shule zote hizi ziko katika hatua za mwisho za
ukarabati na wanafunzi wanaendelea na masomo kama kawaida;
- Shule za Sekondari za Iyunga, Chidya, Tambaza, Zanaki na Kisutu
zinakarabatiwa chini ya Uongozi wa Shule na Bodi za Shule kwa usimamizi wa
Halmashauri za Wilaya zao. Nazo pia ukarabati unaendelea vizuri sana.
- Shule ya sekondari ya Ndwika ambayo iko Wilaya ya Masasi, inajengwa upya chini ya Halmashauri
baada ya taarifa ya wahandisi kubaini kuwa majengo yake hayawezi kufanyiwa
ukarabati.
- Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo nazo pia zinajengwa upya kufuatia kuharibiwa vibaya na tetemeko la ardhi
lililotokea katika Mkoa wa Kagera mwezi Septemba, 2016. Na kwa upande wa Shule
ya Sekondari ya Rugambwa, hii inajengewa nyumba 8 za walimu ambazo zilibomoka
kutokana na tetemeko hilo;
- Vilevile
Wizara kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania inakarabati Shule za Sekondari 17
ambazo ni : Ilboru,
Same, Pugu, Mwenge, Nganza, Mzumbe, Kilakala, Tabora Wavulana, Tabora
Wasichana, Msalato, Dodoma, Ruvu, Korogwe, Bwiru Wasichana, Sengerema, Bihawana
na Kondoa Wasichana. Katika ya hizi mpaka sasa shule 10
zimeshakamilika na saba zitaanza kukarabatiwa hivi karibuni bila kuathiri
masomo.
- Shule za Sekondari 9 ambazo ni Jangwani, Azania, Kibaha, Kigoma,
Tosamaganga, Malangali, Milambo, Minaki na Nangwa zinaendelea kukarabatiwa
chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania – TBA ambazo zipo kwenye hatua
mbalimbali za ukarabati, ambapo shule ya Songea
Wasichana bado haijaanza
kukarabatiwa.
- Ndugu Wanahabari kama mnavyotambua shule zetu
zinafunguliwa kesho kutwa tarehe 8 Januari.
- Wizara baada ya kufanya tathmini ya kina imegundua
kuwa kwenye shule zinazokarabatiwa na TBA kumekuwa na tatizo la ukamilishwaji
wa miradi katika muda uliopangwa. Miradi yote iko nyuma ya ratiba. Na mbaya
zaidi ni kwamba baadhi ya shule haziko tayari kabisa kupokea wanafunzi na
wakaendelea na masomo yao kwa ukamilifu. Yaani mazingira ya ufundishaji na
ujifunzaji hayajakamilika.
- Hivyo basi baada ya mashauriano na wenzetu wa
Ofisi ya Rais TAMISEMI tumekubaliana kuhairisha kuanza kwa muhula wa kwanza kwa
shule za Milambo, Jangwani na Azania.
- Kwa shule hizi muhula wa kwanza utaanza
tarehe 22 Januari 2018.
- Ratiba za masomo katika shule hizi
itarekebishwa ili wiki hizi mbili ziweze kufidiwa. Utaratibu wa kawaida ni
kufidia muda huu wakati wa likizo fupi na likizo ndefu ya mwezi ya mwezi Julai.
Wizara
kwa kushirikiana na Serikali za Mikoa na Halmashauri husika itafanya usimamizi
wa karibu kuhakikisha kuwa shule hizi zinakamilika katika kipindi hiki cha wiki
mbili.
Tunaomba
radhi kwa usumbufu wowote utakaojitokeza kwa wazazi/walezi na wanafunzi
wanaosoma na waliochaguliwa kujiunga katika kidato cha kwanza katika shule hizi.
Natumaini mnatambua nia njema ya Serikali ya kutaka kuimarisha mazingira ya
shule hizi ambazo zilikuwa zimechakaa sana.
Nachukua
fursa hii pia kuwaagiza Wakala wa Majengo, TBA, kutekeleza majukumu yao
kulingana Mikataba tuliyoingia nao. Pamoja na shule hizi Kongwe pia tumewapa
kazi za ujenzi wa Kampasi ya MUHAS-Mloganzila. Matarajio yetu ni kwamba Kampasi
hii itachukua wanafunzi wa kwanza mwaka huu. Nawaagiza TBA kuongeza juhudi pale
Mloganzila ili lengo hili likamilike.
Maelekezo
ya Waziri wangu Mhe. Prof. Ndalichako ni kuhakikisha kuwa tunafanya usimamizi
wa karibu ili miradi yote ya TBA ianze kwenda kulingana na Mikataba. Tutafanya
hivyo wakati pia tunaangalia taratibu za kisheria ili kama kuna hatua zozote
muafaka ziweze kuchukuliwa ili malengo yakamilike kulingana na matarajio.
Ninawashukuru
sana.
Dkt. Leonard D. Akwilapo
KATIBU
MKUU
06 Januari 2018