Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameigiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi VETA Kanda ya Kusini Magharibi kuhakikisha Chuo Cha Wilaya ya
Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kinaanza kutoa mafunzo ya
muda mfupi kuanzia mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri Ndalichako ametoa
agizo hilo akiwa ziarani mkoani Rukwa kwa ajili ya kukagua
miradi ya Elimu inayotekelezwa na wizara hiyo katika mkoa wa Rukwa ambapo
amesema majengo yaliyopo yanaweza kuendelea kutumika kutoa
mafunzo ya muda mfupi huku serikali ikiendelea na utaratibu wa
kufanya ukarabati katika majengo hayo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya Chuo Cha Wilaya
ya Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wapofanya ziara katika majengo ya
chuo hicho yaliyopo katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa. Waziri aliagiza
majengo hayo yaanze kutumika kwa kutoa kozi fupi.
Waziri Ndalichako amesema
majengo hayo ni imara pamoja na kwamba hayajatumika kwa zaidi ya miaka mitatu
lakini miundombinu ya majengo hayo bado ipo vizuri na inahitaji tu kupakwa
rangi na kurekebisha masuala ya umeme .
“Ukiangali unaona raslimali ya
serikali inapotea kuna majengo ambayo yangeweza kutumika kutoa mafunzo kwa
vijana wa Nkasi ili kuwapatia ujuzi lakini hayatumiki, bado
nasisitiza mtumie majengo haya kwa kuanzia yatumike kwa kutoa kozi za
muda mfupi,”alisisitiza Waziri Ndalichako
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya
Kusini Magharibi Justine Ruta (Mwenye suti ya Khaki) akitoa ufafanuzi
kuhusu Chuo cha VETA Nkasi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof
Joyce Ndalichako akijadiliana na Mkuu wa Wilaya hiyo Iddi Kamanta
Waziri Ndalichako amesema
dhamira ya serikali ni kufikia vijana wengi katika kuwapatia ujuzi na maarifa
na vijana wa Nkasi ni sehemu ya vijana hao wanahitaji kuwezeshwa kupata ujuzi
na maarifa ili kuziona fursa nyingi za kimaendeleo.
Akiwa mkoani Rukwa Waziri
Ndalichako pia ametembelea shule ya Sekondari ya Nkasi kwa
lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa
na wadau wa Elimu ambapo katika kuunga mkono juhudi hizo ametoa
mifuko 100 ya simenti itakayosaidia katika ujenzi wa miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya
ya Nkasi Iddi Kimanta amesema serikali ya wilaya ipo tayari
kushirikiana na VETA katika kuhakikisha Chuo hicho kinaanza mapema.