Jumanne, 30 Oktoba 2018

PROF NDALICHAKO: TATUENI CHANGAMOTO ZENU KIMIFUMO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amewashauri watumishi wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kuhakikisha kuwa wanatatua changamoto za mikopo ya Wanafunzi kwa njia ya mifumo.
Waziri Ndalichako amesema hayo jijini Dar Es Salaam alipotembelea ofisi ya HESLB lengo la kujiridhisha na hali ya mwenendo wa utoaji mikopo kwa Wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wale wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/2019.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (mwenye koti la samawati) akiongea na wateja waliofika Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es Salaam kurejesha madeni yao ya mikopo ya Elimu ya juu.
Katika ziara hiyo licha ya kukutana na Menejimenti ya HESLB, Prof. Ndalichako pia aliongea na Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) Profesa Charles Kihampa kuhusu hali ya udahili wa Wanafunzi wa Elimu ya juu ambapo Kihampa alitumia nafasi hiyo pia kukabidhi orodha ya Wanafunzi 2,600 ambao udahili wao umethibitishwa.
Awali katika taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Abdul-Razaq Badru ilisema kiasi cha shilingi bilioni 98.12 mpaka sasa kimetolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 27,929 kati ya wanafunzi 40,485 wa mwaka wa kwanza waliotarajiwa kupatiwa mikopo kwa mwaka wa masomo 2018/2019.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Katikati) akitambulishwa kwa Maafisa Mikopo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo Abdul-Razaq Badru.
Badru alisema kuwa idadi ya wanafunzi waliobaki wapatao 12,556 watapangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 42 katika awamu inayofuata ili kukamilisha idadi iliyokusudiwa.

Aliongeza kuwa idadi ya wanafunzi 27,929 waliokwishapangiwa mikopo na ambao wamedahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu vinavyotambulika ni asilimia 69 ya wanafunzi 40,485 wanaotarajiwa kunufaika na mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2018/2019.

Orodha ya majina ya wanafunzi hao  27,929 (Awamu ya kwanza 25,532 na awamu ya pili 2,397) waliokwishapangiwa mikopo inapatikana kwenye tovuti ya HESLB www.heslb.go.tz  na itatumwa kwenye vyuo husika kwa ajili ya hatua zaidi za kukamilisha malipo ya mikopo hiyo.

Jumamosi, 27 Oktoba 2018

DHAMIRA YA SERIKALI YA KUWA NA CHUO KIKUU CHA KILIMO BUTIAMA IKO PALEPALE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema dhamira ya Serikali ya kumuenzi baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere kwa kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia, (MJUNAT) iko palepale.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo akiwa Wilayani Butiama mkoani Mara mara baada ya kutembelea Chuo hicho kwa lengo la kukagua miundombinu yake, pamoja na kuzungumza na watumishi wanaofanya kazi chuoni hapo.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakitoka nje mara baada ya kukagua  bwalo la chakula katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere.

Akizungumza na Watumishi wa Chuo hicho pamoja na viongozi wa Mkoa na wale wa Wilaya ya Musoma na Butiama amesema hivi sasa Serikali iko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya miundombinu hiyo kutoka kwa aliyekuwa mmiliki wa majengo hayo Nimrod Mkono.


Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Moshi Kabengwe na Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia CPA (T) Rose Waniha wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha Waziri kwenye Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani BUTIAMA mkoani Mara.

Waziri Ndalichako amesema lengo la kuwa na Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia ni kumuenzi baba wa Taifa kwa kutambua mchango wake katika suala la kilimo na kuwa suala hili pia limeanzishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi.


“Mchakato huu ulianza mwaka 2016 na kuwa hapo awali majengo haya yalikuwa yanamilikiwa na Nimrod Mkono, hivyo Serikali haiwezi kujenga au kuboresha bila kuwa na maandishi ya kisheria ya umiliki halali. Napenda kueleza kuwa makabidhiano yako katika hatua za mwisho ili Serikali iweze kuendelea na taratibu nyingine” alisema Ndalichako.
Waziri Wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokelewa na Watumishi katika Chuo Kikuu cha Kilimo, Sayansi na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere, kilichopo Butiama, Mkoani Mara.

Ijumaa, 26 Oktoba 2018

SERIKALI YAAHIDI KUTOA MILIONI 700 KUBORESHA SHULE ALIYOSOMA BABA WA TAIFA MWALIMU NYERERE


Serikali imeahidi kutoa kiasi cha Shilingi Milioni 700 kwa ajili ya kujenga na kukarabati Miundombinu mbalimbali katika shule ya msingi Mwisenge aliyosoma Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere iliyopo manispaa ya Musoma mkoani Mara.

Ahadi hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako mara baada ya kutii maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli ya kuitembelea shule hiyo na kufanya tathmini kwa lengo la kuikarabati ili iendane na hadhi ya Baba wa Taifa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima wakiwa wamekaa kwenye dawati alilokuwa anatumia Baba wa Taifa Mwalimu Jullius Nyerere wakati akisoma katika shule ya Msingi Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma, Mkoani Mara.


Waziri Ndalichako amesema, kipaumbele cha Serikali ya awamu ya Tano ni Elimu, hivyo amemwelekeza Mkuu wa mkoa huo Adam Malima kuhakikisha kuwa fedha ambazo zitaelekezwa katika shule hiyo basi zisimamiwe ili zifanye kazi iliyokusiduwa na si kutumika vinginevyo.

“Rais John Magufuli akiwa katika ziara zake alifika na kuona kuwa shule hii inahitaji kuboreshwa hivyo alinielekeza nifike na kufanya tathmini kwa lengo la kuboresha Miundombinu ya Shule hii, sasa Mkuu wa mkoa mimi na wewe tuhakikishe uboreshaji unafanyika tena kwa kiwango kitakachoendana na hadhi ya Baba wa Taifa letu,” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri wa Elimu  na Mkuu wa mkoa wa Mara wakiwa nje ya bweni alilokuwa analala Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere katika shule ya msingi aliyokuwa anasoma ya Mwisenge iliyopo manispaa ya Musoma.


Waziri Ndalichako amesema fedha hizo zitatumika kujenga mabweni mawili mapya, vyumba vitano vya madarasa, kukarabati Nyumba za walimu na kuboresha Miundombinu ya maji.

Kwa upande wake Mkuu wa mkoa huo Adam Malima ameahidi kusimamia fedha zitakazotolewa kwa ajili ya kuboresha Miundombinu katika shule hiyo na kuwa shule hiyo itakuwa mfano na pia kumbukumbu nzuri kwa Taifa.

Waziri Ndalichako pamoja na viongozi mbalimbali wa mkoa huo pia wametembelea Shule ya sekondari ya Ufundi Musoma, Shule ya sekondari Mara na Chuo Kikuu Cha kilimo na Teknolojia cha Mwalimu Nyerere kilichopo Wilayani Butiama kwa lengo la kukagua hali ya Miundombinu katika Taasisi hizo.
Darasa ambalo Baba wa Taifa Mwalimu Jullius K. Nyerere alilitumia kwa ajili ya kusoma kuanzia mwaka 1934 - 1936, shule hiyo ipo kwenye manispaa ya Musoma mkoani Mara.


Alhamisi, 25 Oktoba 2018

SERIKALI YAAHIDI KUENDELEA KUBORESHA MAZINGIRA YA WATU WENYE ULEMAVU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatenga asilimia 2 ya bajeti zao kwa ajili ya kuhudumia watu wenye ulemavu na kuwa suala hilo lipo kisheria.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo Kitaifa hapa nchini yamefanyikia Mkoani Mwanza.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Mkurugenzi Msaidizi wa idara ya           Elimu Maalumu wa Wizara hiyo Adamson Shimbatano aliyeshika Fimbo Nyeupe wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe duniani ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani Mwanza.

Ndalichako amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais John Magufuli imeendelea  kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kutoa ajira na kuwa katika ajira za mwaka jana  walimu 70 wasioona waliajiriwa.

“Niwahakikishie Watanzania kuwa Rais John Magufuli ni kiongozi anaejali sana watu wenye ulemavu ndiyo maana wapo viongozi wenye ulemavu aliowateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika Serikali yake wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi, Mabalozi, na wengine ili wamsaidie katika kutekeleza majukumu ya kuliletea Taifa Maendeleo,” alisema Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amewataka Wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wasioona na badala yake wahakikishe watoto wote waliofika umri wa kwenda Shule wanaandikishwa kwa kuwa hivi sasa Elimu msingi inatolewa bila malipo na kuwa ulemavu siyo kikwazo cha Maendeleo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea msaada wa Fimbo Nyeupe kutoka kwa mmoja Wafanyabiashara mkoani Mwanza, ili fimbo hizo zigaiwe kwa watu wasioona walioshiriki maadhimisho hayo mkoani Mwanza.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Shirikisho la watu wenye ulemavu nchini Tanzania Benedict Louis amempongeza na kumshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa kutambua jitihada na uwezo wa watu wenye ulemavu na hivyo kuwateua wenye ulemavu kushika nafasi mbalimbali.

Louis ameeleza kuwa Siku ya Fimbo Nyeupe ni muhimu kwa kuwa inatoa fursa kwa wasioona kutathmini jitihada zinazofanywa na serikali katika kuleta ustawi kwa watu wenye ulemavu na kuwa Fimbo hiyo ni nyenzo muhimu ambayo inamsaidia asiyeona kutambua vikwazo vilivyo mbele yake.

Kauli mbiu  ya mwaka huu katika maadhimisho hayo ni “ Mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni nyenzo Shirikishi ya uchumi wa Viwanda.”
Watu wasioona wakicheza mziki pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa maadhimisho ya siku ya Fimbo Nyeupe ambayo kitaifa yamefanyikia mkoani Mwanza na kauli mbiu katika maadhimisho hayo ni mafunzo ya TEHAMA kwa wasioona ni nyenzo shirikishi ya uchumi wa Viwanda.


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA


MAJINA YA WATANZANIA WALIOPATA UFADHILI WA MASOMO JAMHURI YA ALGERIA MWAKA WA MASOMO 2018 – 2019
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inawapongeza wanafunzi wote waliopata fursa za ufadhili wa masomo kutoka Serikali ya Jamhuri ya Algeria kwa mwaka wa masomo 2018/2019.  Wanufaika wote mnatakiwa kuzingatia maelekezo muhimu ili kufanikisha safari yenu ya kwenda masomoni.
Maelekezo Muhimu
Wanafunzi wote wanatakiwa kukamilisha maandalizi ya safari kwenda masomoni nchini Algeria kwa kufanya mambo yafuatayo:
(i)                 Kila mwanafunzi anatakiwa kuwasilisha “passport” yaani hati ya kusafiria ubalozi wa Algeria kwa ajili ya VISA.
(ii)              Kulipa USD 50 kwa ajili ya VISA.  Ada ya VISA italipwa ubalozi wa Algeria.
(iii)            Awe na picha passport size 3 zenye kivuli cheupe.
(iv)            Tarehe ya safari ni kati ya tarehe 5 – 11/11/2018.
NB: Iwapo mnufaika atakuwa na changamoto awasiliane na Mratibu Bwana L. Malili Na. ya simu ni 0715 150047.

NA
NAMBA YA USAJILI
JINA LA
MWANAFUNZI
JINA LA CHUO
PROGRAMMU
1
8TZA4703
Kassim Adila Ally
University of Science and Technology in Oran
Science and Technology
2
8TZA4701
Oscar Gomba
University of Constantine 1
Natural Science and life
3
8TZA4626
Mkumbo Nakembetwa John
University of Setf 1
Natural Science and Life
4
8TZA4375
Faru Suhayrnan R George
University of Science and Technology in Blida 1
Science and Technology Science
5
8TZA4126
Masige Goodluck Stephano
University of Constantine 1
English
6
8TZA4118
Ngwenya Alfonce Simon
University Sidi Bel Abbes
English
7
8TZA4132
Malekela Yonathani Frank
University of Constantine 1
Veterinary Science
8
8TZA4175
Mohamed Ali Mlenge
University of Tlemcen
Science and Technology
9
8TZA4182
Mwakikuti Ezra George
University of Blida 1
Veterinary Science
10
8TZA4165
Malemo Francisca Masatu
University of Science and Technology in Oran
Hydraulic
11
8TZA4172
Kabyazi Edibily Egbert
University of Bejaia
Economic Science Management and Trade
12
8TZA4039
Hussein Mariam Ismail
University of Constantine 1
English
13
8TZA4122
Meza Ismail Omary
University of Oran 2
English

Imetolewa na:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
25/10/2018



Jumanne, 23 Oktoba 2018

UFAFANUZI WATOLEWA KUHUSU WANAFUNZI KUJIUNGA UDSM


ALIYOYAZUNGUMZA NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM PROF. BONAVENTURE RUTINWA KATIKA KIPINDI CHA JAMBO TANZANIA LEO TBC.

1. Wale wote waliiomba Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wakafutiwa udahili kwa sababu ya kuwa wengi zaidi (over capacity) wamerudishwa wote bila masharti yoyote.

2. Prof. Rutinwa ameeleza kuwa wale walioko Dar es Salaam waendelee kuchukua barua zao za udahili (admission letter) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wale walioko mbali na Dar es Salaam watazipokea barua zao kuanzia tarehe 27/10/2018 watakapofika kwa usaili. 

3. Wataalamu wa mifumo ya kompyuta wanaandaa utaratibu ili waliodahiliwa wapokee barua zao kwenye akaunti zao za udahili.

4. Wanafunzi ambao wamekosa code au wameshindwa kuingiza codes UDSM au vyuo vingine watapewa utaratibu wa kwenda chuo wanachokitaka.

5. Kutakua na dirisha la wale waliokosa nafasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ya Program hizo kujaa wapate nafasi ya kuomba tena.

6.Serikali imeendelea kuboresha Miundombinu katika Chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa na maabara kwa hali ya juu na ya viwango kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi ambao chuo hicho inataka kuwadahili.


7. Serikali pia inaendelea kukiwezesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuongeza idadi ya Wahadhiri wabobevu ili kukidhi uhitaji.

8. Leo ilikuwa ni siku ya mwisho kufunga udahili lakini mara baada ya kufanya kikao na Mhe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alielekeza kuongezwa kwa siku hizo ili kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi.


9. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinamshukuru sana Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa kusaidia kutatua changamoto iliyokuwepo katika udahili kwa UDSM.