Serikali ya awamu ya Tano
imesema miongoni mwa vipaumbele vyake ni pamoja na kuimarisha na kuboresha Elimu
nchini na ndiyo maana sekta hiyo imetengewa fedha nyingi katika bajeti ya Taifa.
Kauli hiyo ya serikali
imetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. William Ole
Nasha mkoani Morogoro wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wanaosimamia Elimu
katika mkoa huo na kueleza kuwa kwa sasa Tanzania ni nchi inayosifiwa kwa kuongeza
bajeti ya Elimu kwa asilimia 21.4 ya bajeti ya jumla ya Taifa.
“Ninachoweza kusema kwa sasa
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka inapokea bajeti yake ambayo ni
sh trilioni 1.4 na kwenye fedha za Maendeleo zinapatikana zote kwa asilimia 100
kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Elimu bila kuchelewa yote haya ni kwa sababu
Sekta ya Elimu ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano,” aliongeza Naibu
Waziri Ole Nasha
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akiongea na viongozi
wa elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mara baada ya kuwasili katika
Halmashauri hiyo kukagua miradi ya Elimu.
Amesema katika miaka mitatu ya uongozi wa
Serikali ya Awamu ya Tano kumefanyika uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Elimu
kuliko wakati wowote na kuwataka watendaji wa sekta hiyo kusimamia fedha zinazotolewa
kwa ajili ya miradi ya Maendeleo ya Elimu kwa umakini ili kuweza kubadilisha
mazingira ya watoto ya kujifunzia.
“Wote ni mashahidi kuhusu ujenzi wa
miundombinu ya Elimu inayoendelea nchini, Juzi mmeona Mhe. Rais John Magufuli akifungua maktaba kubwa
kuliko maktaba zote Afrika Mashariki na Kati, maktaba yenye uwezo wa kuchukua
vitabu laki nane na wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja lakini pia kwenye vyuo vya
ufundi na shule pia kuna uwekezaji mkubwa ambao umefanyika wa kuboresha
miundombinu ya kufundishia na kujifunzia vyote hivyo ni kwa sababu sekta ya
Elimu ni kipaumbele,” alisisitiza Ole Nasha
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akikagua mradi wa
ujenzi ya sekondari ya Kumbukumbu ya Sokoine inayojengwa katika Halmashauri ya
Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro. Yanayoonekana hapo ni madarasa ambayo
yatakuwa katika mfumo wa ghorofa.
Naibu Waziri Ole Nasha yuko mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku
tatu na kuwa ziara hiyo inatarajiwa kuhitimishwa leo.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William ole Nasha akikagua majengo ya
Chuo cha Ualimu Ilongo kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa ambayo miundombinu
yake imefanyiwa ukarabati na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia
Programu ya EP4R.