Jumatano, 24 Aprili 2019

BARAZA LA WAFANYAKAZI WIZARA YA ELIMU LAKUTANA KUJADILI MWELEKEO WA BAJETI KWA MWAKA 2019/20.


Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Filisi Nyimbi amesema serikali ya awamu ya tano imeweka misingi imara itakayowezesha kila mtanzania kupata elimu iliyo bora na yenye tija kwa Taifa ili kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025.

Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoojia unaofanyika mkoani Mwanza na kusisitiza kuwa Wizara hiyo imepewa jukumu la kutunga sera, kuandaa na kusimamia miongozo mbali mbali ya Elimu itakayowezesha Elimu inayotolewa nchini kuwa bora.

Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa wameshikana mikono wakati wa kiimba wimbo wa “SOLIDARIRY” kuashiria umoja, mshikamano na upendo katika utekelezaji wa majukumu yao
 


Dkt. Nyimbi amesisitiza kuwa ili kutimiza azma ya serikali ya awamu ya tano kila mtumishi ana wajibu wa kufanya kazi kwa bidii na kwa weledi wa hali ya juu.

Dkt. Nyimbi ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia katika Shule za Sekondari, Vyuo vya Ualimu, Elimu ya Juu, Vyuo vya Ufundi,  na Vyuo vya Maendeleo ya wananchi (FDCs) lengo likiwa ni kuweka mazingira bora ya kielimu katika kuandaa vijana wenye sifa katika kujenga uchumi wa nchi.



Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Dkt. Filisi Nyimbi Akizungumza na washiriki katika Mkutano wa  26 wa  Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo watumishi wametakiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria.


Pia ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuimarisha na kuboresha  idara ya Uthibiti Ubora wa shule kwa kununua magari ili idara hiyo iendelee kukagua shule na kutoa ushauri wa kitaalamu  na kitaaluma.

Akizungumza katika mkutano huo Naibu Katibu Mkuu Prof. James Mdoe amesema pamoja na mambo mengine kikao hicho kitapitia utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2018/19 na kujadili mwelekeo wa bajeti kwa mwaka 2019/20.



Mgeni rasmi Dkt. Filisi Nyimbi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi na  washiriki wa Mkutano wa 20 wa Baraza la Wafanyakazi wakiwa kwenye picha ya pamoja. Kikao kazi hicho kimefanyikia mkoani Mwanza.
 


“Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu yake kwa lengo la kuboresha sekta ya Elimu hapa nchini, hivyo niwaase watendaji wote kuendelea kufanya kazi kwa kufauta kanuni, taratibu na sheria zinazosimamia utendaji katika maeneo yenu ya kazi,”alisisitiza Prof. Mdoe.

Mkutano huu umehudhuriwa na wajumbe zaidi ya 120 kutoka Wizara ya Elimu na wajumbe kutoka Chama cha Walimu Tanzania ( CWT ) na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na  Afya (TUGHE).   Kauli mbiu ya Mkutano huo wa 26 wa baraza la wafanyakazi ni: “Elimu bora na Uwajibikaji wa pamoja ni Chachu ya Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda Tanzania”



Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa 26 wa Baraza la Wafanyakazi wakifuatilia hotuba ya  mgeni rasmi wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo unaofanyika Jijini Mwanza



Ijumaa, 19 Aprili 2019

NAIBU KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU AKAGUA MRADI WA UJENZI MABWENI YA WANAFUNZI MZUMBE


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe ametembelea Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe na kukagua mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi unaoendelea katika eneo la Maekani

Akizungumza mara baada ya kukugua mradi huo mjini Morogoro, Prof. Mdoe amemuagiza mkandarasi “National Service Corporation Sole” (SUMA JKT) kukamilisha 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akikagua mradi wa ujenzi wa wa mabweni ya wanafunzi unaoendelea katika eneo la Maekani mkoani Morogoro.

"Serikali haitavumilia kucheleweshwa kwa mradi huu ambao ni muhimu kwa chuo katika kuondoa tatizo la malazi kwa wanafunzi"amesisitiza Prof. Mdoe

 Prof. Modoe  amewaagiza SUMA JKT  kuongeza vibarua na wafanyakazi kwa ajili ya kufanya kazi hiyo kwenda kwa haraka zaidi ili ukabidhiwe kwa wakati, hivyo kawashauri kuwa na zamu ili kukamilisha mradi huo.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Ganka Nyamsogoro  amesema mabweni hayo ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi zaidi ya 1000 katika eneo la Maekani, Kampasi Kuu. umefadhiliwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe akiongea na viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa wa mabweni ya wanafunzi unaoendelea katika eneo la Maekani mkoani Morogoro.

Nyamsogoro amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika tarehe 19 April 2019 na gharama yake ni kiasi cha shilingi  billioni 6.5 fedha ambazo zimetolewa na serikali kupitia  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Kwa upande wake msimamizi wa  mradi huo kutoka Suma jkt Eng. Focus Odecho wamemhakikishia Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa ujenzi wa mabweni hayo  utakamilika ndani ya muda uliopangwa.


Alhamisi, 18 Aprili 2019

WAZIRI NDALICHAKO AZINDUA MACHAPISHO YA LUGHA YA KISWAHILI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako (Mb) amezindua machapisho ya kitaaluma yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Uzinduzi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amesema kwa muda mrefu machapisho ya kitaaluma yamekua yakiandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kupelekea watanzania wengi kutopata majibu ya tafiti zinazofanywa na wanataaluma hao.

Waziri Ndalichako amewapongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa hatua hiyo kubwa ya  matumizi ya  lugha ya Kiswahili katika kuhakikisha maarifa yanawafikia wananchi wote hasa katika kipindi hiki ambapo nchi inapoelekea uchumi wa kati kupitia viwanda.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizindua machapisho ya Kitaaluma yaiandikwa kwa lugha ya Kiswahili, uzinduzi huo umefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
Aidha, Waziri  Ndalichako ahimiza watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika lugha ya Kiswahili.

"Nawapongeza wanataaluma kwa kutoa machapisho ya tafiti zao  kwa kutumia Lugha Adhimu ya Kiswahili endeleeni kufanya tafiti zaidi kwa maendeleo ya nchi," amesema Ndalichako.

Akimkaribisha Waziri kuzindua machapisho hayo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. William Anangisye amempongeza Waziri kwa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia elimu nchini.

Prof. Anangisye amesisitiza kuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendeleza kazi yake muhimu ya utafiti kwa ubora wa hali ya juu na kutoa machapisho katika majarida ya kitaaluma yenye hadhi ya juu ya kimataifa na kitaifa.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akionyesha moja ya Chapisho mara baada ya kuzindua machapisho ya Kitaaluma yaiandikwa kwa lugha ya Kiswahili, uzinduzi huo umefanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jijini Dar es Salaam

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Victor Eliah ameipongeza serikali  chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa jitihada kubwa za kukikuza na kukitumia Kiswahili.

Akiongea kwa niaba ya waandishi wa machapisho mbalimbali ya tafiti Eliah amekishukuru Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kumuwezesha kuandika kitabu kinachohusu Matumizi ya Kiswahili katika Vyombo vya Habari ikiwa  ni juhudi za kuhakikisha jamii inapata kazi za waandishi wa habari katika umahiri wa hali ya juu.

Nae Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Bonaventure Rutinwa amewataka wananchi kununua na kusoma vitabu mbalimbali ili kujichotea maarifa na kujiendeleza katika lugha hasa ya Kiswahili kwa sababu ina fursa nyingi sana za ajira ndani na nje ya nchi.