Jumatatu, 18 Agosti 2014

Serikali yaipongeza VETA kwa Mafanikio


Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini (VETA)  kutokana na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu kati ya mwaka 2011 na  2014. Mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka kwa wanafunzi waliojiunga na mafunzo ya ufundi stadi kutoka 102, 700 mwaka 2011 hadi 159, 345 mwaka 2014, kuongezeka kwa ushirikishwaji wanawake katika nafasi mbalimbali  katika elimu ya ufundi stadi kutoka asilimia 35 mwaka 2011 hadi asilimia 42 mwaka 2014 na kuongezeka kwa udahili kwa walimu wa mafunzo ya ufundi stadi ngazi ya cheti kutoka  276 mwaka 2011 hadi  939 mwaka  2014 na ngazi ya stashahada kutoka walimu 34 mwaka 2011 hadi  89 mwaka 2014.


Waziri Kawambwa alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es Salaam ya kuwaaga Wajumbe wa Bodi ya Ufundi Stadi ya Taifa iliyomaliza muda wake ambapo aliyataja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kukamilika na kuanza kutekelezwa  kwa Mpango  Mkakati wa Miaka Mitano (2012/13 -2016/17) wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi na kuimarika kwa mifumo mbalimbali ya Uongozi na Usimamiaji wa Fedha. Aidha, Dkt. Kawambwa alisema VETA katika kipindi hicho imeweza kujenga vyuo vipya vya Mikoa vya Manyara, Lindi, na Pwani.  Pia, kukamilisha ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi - Kipawa ICT na Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya cha Makete na  Chuo cha Hoteli na Utalii cha Arusha (VHTTI).

VETA pia imekamilisha maandalizi ya msingi katika maeneo patakapojengwa  vyuo vipya vya Mkoa vya Simiyu, Geita, Njombe na Rukwa.

Mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kukamilika na kuanza kutekelezwa kwa sera na miongozo mbalimbali ya kuwezesha kutolewa elimu na Mafunzo ya ya ufundi stadi yaliyo bora, kuanzishwa kwa viwango 53 vya stadi za kazi      na kuhuishwa kwa mitaala mbalimbali na kuanzishwa kwa mahusiano na makubaliano mbalimbali kitaifa na kimataifa katika kuendeleza na kuimarisha elimu na mafunzo ya ufundi stadi. 

Pamoja na kutoa pongezi kwa Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa mafanikio yote yaliyopatikana wakati ikiwa chini ya usimamizi wa Bodi iliyomaliza muda wake, Waziri Kawambwa aliwaasa kuongeza bidii zaidi ili kupata mafanikio makubwa zaidi ya yale waliyofikia. 
“Naiasa Menejimenti ya VETA  kuipa ushirikiano mkubwa Bodi mpya nitakayoiteua muda si mrefu ili kuelekeza nguvu zao kutatua changamoto zilizopo,” alisema Dkt. Kawambwa. 

“Aidha, bado ufumbuzi unatakiwa wa jinsi ya kuwapata wakufunzi wenye umahiri wanaotakiwa kutoa mafunzo katika vyuo vyetu kulingana na hali ya sasa ya mabadiliko ya mara kwa mara ya Sayansi na teknolojia.  Hali ya sasa ya kutegemea walimu wenye "trade test" au ngazi ya aina moja kufundisha ngazi ile ile inabidi iepukwe. Lazima mikakati maalumu iandaliwe ya kupata wakufunzi walio mahiri kutoka vyanzo mbalimbali,” alisema Waziri Kawambwa. 
Bodi ya Ufundi Stadi ya Taifa iliyomaliza muda wake ilikuwa inaongozwa na Profesa Idrisa Bilal Mshoro na iliingia madarakani tarehe 1 Agosti, 2011 ilipoanza kazi rasmi.
 

  

Alhamisi, 7 Agosti 2014

MRADI WA KUKUZA STADI KUANZISHWA

Wizara  ya  Elimu na Mafunzo  ya  Ufundi  kwa kushirikiana  na Asasi  za vyuo na  taasisi za Canada wataanzisha Mpango wa kutekeleza mradi  wa  Mafunzo  ya kukuza  stadi kwa ajili ya uajiri (Improving Skills Training for Employment Programme - ISTEP ). Mpango huu utajenga uwezo wa asasi za Mafunzo ya ufundi nchini kufundisha kwa umahiri stadi zinazoitajika katika sekta za uchimbaji wa madini, mafuta, gesi na sekta ya utalii.

Kaimu  Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Thomas   Katebalirwe  alieleza hayo jijini Dar es Salaam katika warsha   ya makubaliano  na wadau  iliyokuwa  ikijijadili hatua  mbalimbali  katika kujenga  ushirikiano wa jinsi wanafunzi  na tasnia zitakavyofaidika na mpango huu.

Alisema  Mradi  huu  utajikita  katika sekta   za madini, gesi  na utalii, kwamba  utajenga uwezo wa asasi za kitanzania za Mafunzo ya ufundi kufundisha kwa umahiri stadi zinazohitajika katika sekta zote za uchimbaji wa madini, mafuta na gesi na sekta ya utalii, na hivyo kuwapatia vijana takribian 1,200 stadi mwafaka zitakazowawezesha  kujiajiriwa kwenye sekta ya uchimbaji na utalii ama kujiajiri.

“Tayari wataalanu wamefanya   upembuzi   katka  maeneo  mbalimbali  , ili  kupata    mahitaji  ya utekelezaji  wa mradi huo wa miaka  mitano, ambao utagharamia Dola za Canada million  13   na utawanufainisha  watanzania   12,000 hasa  katika  masuala  ya gesi .” alisema Katabalirwe.

Aidha,    alisema  taasisi  11  zitashirikiana katika kukuza uelewa  kwa vijana   kwa kuwa  gesi  ni kitu kipya  kinachohitaji nguvu  kazi  ya kutosha na yenye Mafunzo maalum. Vijana hao watatoka katika taasisi za utalii, Madini na Gesi ambao watapatiwa Mafunzo ya uchimbaji wa madini na uchomeleaji wa mabomba ya gesi.  
Mwenyekiti  kutoka shirikisho  la wachimbaji na watafutaji  wa Madini Tanzania , Nyanda  Shuli  alisema  mpango huo  ni muhimu  katika  kuendeleza  Sekta  ya  Madini    na Nishati  kwa kuwa inahitaji   nguvu kazi  ya kutosha  kukuza  sekta  hiyo.

Alisema   kila mwaka shirikisho  huandaa Mafunzo  kwa kuangalia  mahitaji ya  Sekta  ya  Madini. Alisisitiza kuwa vyuo vilivyosajiliwa   vitanufaika  kutumia  fursa  hiyo  kwani ni  ya kipekee, sekta hiyo inahitaji kufikia lengo la kuchangia pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025, kwa kuwa miaka iliyopita ni asilimia 3 pekee iliyotoka katika sekta hiyo.
Jumatano, 6 Agosti 2014

KAMPASI YA HISABATI KUANZISHWA NCHINI

Serikali ya Tanzania  na Taasisi ya  African  Institute for  Mathematical  Sciences - Next Einstein Initiative (AIMS-NEI) wamesaini Mkataba wa Makubaliano kuanzishwa kwa kampasi ya taasisi hiyo  nchini  itakayofundisha na kuendeleza masomo ya  Hisabati na Sayansi.

Mkataba huo umesainiwa   jana na Katibu Mkuu wa   Wizara ya Elimu na Mafunzo  ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome kwa upande wa Serikali na  Bwana Thierry Zomahoun, Mkurugenzi Mtendaji wa AIMS-NEI  jijini  Dar es Salaam.


Profesa Mchome amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni  jitihada za Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kuhakikisha kuwa Taifa linakuwa na wataalam wa kutosha katika Nyanja za Hisabati na Sayansi. Mheshimiwa Rais alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa taasisi hiyo alipokuwa ziarani nchini Canada mwishoni mwa mwaka jana.

Akizungumzia mkataba huo, Profesa Mchome alisema “Hii ni nafasi ya pekee maana huwezi kupata Mainjinia bila kujua hesabu, wala Madaktari na Wanasheria bila kuwa na ufahamu wa hesabu, na hesabu ndiyo kila kitu,”.

Taasisi ya African Institute for Mathematical Science-Next Einstein Initiative (AIMS-NEI), wameshafungua kampasi zake  katika  nchi za Afrika Kusini, Senegal, Ghana na Cameroon, na kwa hapa Tanzania tayari wamepata eneo wilayani Bagamoyo katika majengo ya Boma ambayo yatakarabatiwa. Kwa kuanzia masomo hayo yatatolewa katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo Arusha ambapo wanafunzi 40 wa awali wameshadahiliwa tayari kwa kuanza masomo hayo mwezi Septemba mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa African Institute for Mathematical Sciences-Next Einstein Initiative (AIMS-NEI), Thierry Zomahoun, alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi bora kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki, ili ijijenge katika misingi ya uchumi imara zaidi, haina budi kuwekeza katika masuala ya hesabu na sayansi ili kupata watalaamu  watakaolisaidia taifa kusonga mbele kimaendeleo.

Aidha, Bwana Zomahoun alimpongeza Mheshimiwa Rais Kikwete kwa  kukubali kuanzishwa kwa kampasi ya taasisi hiyo hapa nchini ili kukuza na kuendeleza masomo ya hisabati na sayansi na kuzalisha wataalamu wa kutosha watakaokidhi mahitaji ya nchi katika nyanja mbalimbali.