Jumanne, 2 Septemba 2014
NAIBU WAZIRI AWAAGIZA MAAFISA ELIMU KUWARUDISHA WANAFUNZI WATORO SHULENI
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Mhe.Jenista Mhagama amewaagiza Maafisa Elimu wote nchini kuhakikisha wanafunzi walioacha shule kwa sababu mbalimbali wanarudi shuleni ili kuendelea na masomo.
Naibu Waziri alitoa agizo hilo mwishoni mwa
wiki wakati wa ziara yake mkoani Pwani
kukagua miradi inayojengwa na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Elimu
ya Sekondari (MMES). Shule zilizotembelewa ni Nyamisati,
Mkamba na WAMA Nakayama zote zikiwa za sekondari na shule ya Msingi ya Mazoezi Vikindu, .
Aliwataka
Maafisa Elimu kufuatilia sababu za utoro unaojitokeza shuleni na kuandika
taarifa juu ya utoro huo na kutafuta njia za kupunguza utoro shuleni. Pia aliwataka
Wakaguzi wa Shule wa Kanda pamoja na kazi nzuri wanayoifanya ya kukagua
ufundishaji na vigezo, ukaguzi unaofanyika sasa ujikite katika kujibu hoja ya utoro wa wanafunzi
katika shule. Alimuagiza Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Shule kutoka Wizarani Bibi
Hidaya Mohamed kutopokea ripoti zisizotoa uelekeo wa namna ya kuwarudisha
watoto shuleni.
“Katika
kila shule ambapo kutakuwa na utoro mkubwa wa wanafunzi Wakaguzi msipokee
ripoti ya ukaguzi isiyotoa majibu kwanini wanafunzi katika shule zetu za msingi
na sekondari wanaendelea kutoroka na ripoti ionyeshe hatua zilizochukuliwa kuwarudisha
shuleni, mipango na mikakati ya kuhakikisha suala hili halijirudii ili kuwa na
ubora wa elimu.” Alisema Mhe. Mhagama
Kuhusiana na maslahi ya Walimu Mhe. Mhagama
alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkuranga kuanzisha dawati la malalamiko
litakalowawezesha walimu kupeleka
malalamiko yao na kuwataka yafanyiwe kazi
haraka iwezekanavyo. Alisema kuanzishwa kwa dawati hilo kutawapunguzia adha
walimu ya kupoteza muda kufuatilia madai yao na badala yake watatumia muda huo
kuwafundisha wanafunzi.
“Sitaki
walimu hawa tunaowaleta huku wapoteze muda mwingi katika majengo ya Halmashauri
kufuatilia madai yao kwani hawa ndio watumishi wengi kwenye Halmashauri
hakikisheni mnawatengea dawati maalumu la kushughulikia kero zao.”Alisema Mhe. Mhagama.
Jumatatu, 25 Agosti 2014
Waziri Kawambwa aiasa Jamii Kuchangia Elimu
Aipongeza Airtel kwa kutoa
vitabu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru
Kawambwa ameiasa jamii kuchangia kuboresha elimu nchini kwa kutoa misaada
mbalimbali itakayosaidia kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa katika ngazi
mbalimbali za elimu.
Waziri Kawambwa alikuwa akizungumza katika
hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Vitabu
Airtel Shule Yetu 2014 jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki ambapo wawakilishi
wa shule za Sekondari 30 walipatiwa msaada wa vitabu vya
Sayansi na Hisabati na Kampuni hiyo.
Waziri Kawambwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika
uzinduzi huo alisema
Mradi huu wa Vitabu Airtel
Shule Yetu utakuwa wa manufaa makubwa sana si kwa wanafunzi shuleni tu bali kwa sekta nzima ya Elimu
hapa nchini na kwa Taifa kwa ujumla.
“Sote tunatambua kwamba kitu pekee
kinachotofautisha nchi zilizoendelea na zinazoendelea siyo utajiri na mali walizonazo
bali ni elimu na ujuzi. Hii ni kwa sababu
utajiri na mali havijileti vyenyewe isipokuwa huchochewa na maendeleo mazuri yaliyo
jengwa katika msingi mzuri wa ELIMU. Kwa kadri kiwango cha elimu na ujuzi au
maarifa kinapokuwa juu katika nchi, ndipo na kiwango cha maendeleo ya nchi yanapozidi
kukua katika nchi hiyo,”alisema Dkt. Kawambwa.
Dhamira ya
Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 (Tanzania Development Vision 2025) ni kuifanya Tanzania
kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Lakini hilo litawezekana tu kwa kupitia elimu.
Yaani kuwa na Taifa lililoelimika; lenye
wasomi wanaoweza kubaini na kutatua matatizo ya maendeleo ya nchi yetu. Na katika wakati huu tulionao, Sayansi na Tekinolojia vina nafasi ya pekee
katika maendeleo ya nchi na ustawi wa jamii.
“Tunaishukuru
sana Airtel Tanzania kwa kutuunga mkono katika dhamira ya Serikali yetu ya kuwekeza
katika sekta ya elimu nchini. Airtel imekuwa
mstari wa mbele katika kuchangia vitabu pamoja na misaada mbalimbali kwa shule zetu
hapa nchini. Vitabu hivi vilivyochangiwa
na Airtel vitasaidia sana katika juhudi za Serikali za kuimarisha ubora wa
elimu inayotolewa,” alisema Waziri Kawambwa.
Hivi
sasa kuna uhaba wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati katika shule zetu za
Sekondari hapa nchini. Takwimu zinaonesha
kwamba hadi mwaka 2013/14 tulikuwa na upungufu wa walimu wa Sayansi na Hisabati
26,998. Lakini hata kule kwenye walimu wa masomo haya bado
kuna tatizo la uhaba wa vitabu. Lakini
kule ambako kuna uhaba wa walimu uwepo wa vitabu hivi utakuwa ni wa msaada sana
kwa wanafunzi kuweza hata kujisomea wenyewe.
Tukio hilo la Kampuni ya Airtel kukabidhi vitabu ni mwendelezo wa mambo mengi
ambayo yamekwishafanya katika kuisadia Sekta ya elimu nchini. Mradi huu ulianza miaka takriban kumi
iliyopita na katika kipindi chote hiki mradi umeweza kupeleka vitabu na vifaa
vya maabara katika shule mbalimbali na pia kufanya ujenzi na matengenezo katika
shule kadhaa hapa nchini.
“Napenda kutumia fursa hii kuwahimiza makampuni mengine na Taasisi mbalimbali nchini kuiga mfano huu
wa Airtel na kusaidia sekta ya elimu ili kujenga taifa lililo bora. Serikali iko tayari kushirikiana na Taasisi,
Makampuni na asasi mbalimbali katika kuendeleza Elimu ya watoto na vijana wetu,”
alisema Waziri Kawambwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Airtel
Tanzania Sunil Colaso alisema kampuni yake itaendelea kuisaidia sekta ya elimu
ili kuchangia katika juhudi za serikali za kuboresha elimu hapa nchini ambapo
hadi hivi sasa shule za sekondari 1,000 zimefaidika kwa kupewa vitabu na kampuni
hiyo.
Ijumaa, 22 Agosti 2014
JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TANGAZO
KWA UMMA
MKUTANO
KATI YA WIZARA NA WANAFUNZI WANAOSOMA MASHARIKI MWA UKRAINE HUSUSANI ENEO LA LUGANSK
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inawatangazia wanafunzi wote wa Tanzania wanaosoma katika vyuo vya Lugansk, Ukraine na maeneo mengine Chini ya Ufadhili wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambao hivi sasa wako likizo hapa nchini kuwa kutakuwepo na mkutano kujadili, pamoja na mambo mengine, hali ya usalama na hatua za kuchukua kabla ya kurudi Lugansk kuendelea na masomo, mwezi Septemba, 2014.
Mkutano huo utafanyika Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi, siku ya Jumatano, tarehe 3 Septemba, 2014 saa nane mchana. Aidha, wanafunzi wengine wanaosoma Lugansk kwa
udhamini binafsi wanaombwa kuhudhuria ili kushiriki katika mkutano huo.
Imetolewa na: Katibu Mkuu
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi
7 Mtaa wa Magogoni,
Post Code 11479,
S.L.P. 9121,
DAR ES SALAAM.
Jumatano, 20 Agosti 2014
WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI
TANGAZO
KWA UMMA
MAPENDEKEZO
YA MABORESHO YA MICHEPUO NA TAHASUSI ZA KIDATO CHA KWANZA MPAKA CHA NNE NA
KIDATO CHA TANO NA SITA
Elimu
ya sekondari katika ngazi ya Kidato cha Kwanza hadi cha Nne imekuwa ikiongozwa na michepuo ya ama ya Sanaa,
Sayansi, Ufundi na Biashara. Halika dhalika, masomo ya sekondari Kidato cha
Tano na Sita yamekuwa ya kifundishwa kwa kutumia Tahasusi mbalimbali kulinga na
mahitaji ya nchi ambazo kwa sasa ni PCM, PCB, PGM, CBG, EGM, CBA, CBG, CBN kwa Sayansi,
na HGL, HGK, HKL, KLF, ECA, HGE kwa Sanaa.
Mafanikio
mbalimbali yamepatikana kwa kutumia mfumo huu tangu ulipoanza hadi sasa. Hata hivyo,
kutokana na (a) nia ya nchi kupiga hatua zaidi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo
ya nchi kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, (b) mabadiliko ya mahitaji
ya ulimwengu wa ajira na kazi na (c) kuendelea kukua kwa ugunduzi na ubunifu pamoja
na matumizi ya Sayansi na Teknolojia katika maeneo mbalimbali, Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi imeona kuna umuhimu wa kupitia upya Michepuo na Tahasusi zilizopo
ili ufundishaji uweze kwenda na wakati. Michepuo na Tahasusi hizo mpya zinatarajiwa
kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2015/2016.
Ili
kufanikisha maboresho hayo, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inakaribisha wadau
wote wa Elimu na Mafunzo kutoa mapendekezo ya jinsi gani Michepuo na Tahasusi za
elimu ya sekondari ziundwe au kuanzishwa katika madarasa ya kidato cha Kwanza
hadi Nne na Tano hadi Sita. Mwisho wa kutuma mapendekezo ni tarehe 31/10/2014. Wadau wote mnahamasishwa kutoa
maoni yenu kupitia njia mbalimbali ikiwemo vikao ama kwa kuwasiliana moja kwa moja
na wizara. Majumuisho ya mapendekezo ya tawekwa kwenye magazeti na tovuti kwa maoni
na hatua za mwisho katika kukamilisha maboresho haya.
Mapendekezo
ya Michepuo naTahasusi mpya yatumwe kwa anuani ifuatayo:
Katibu
Mkuu,
Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
7
Mtaa wa Magogoni,
11479
DAR ES SALAAM.
Elimu
Bora Inawezekana; Timiza Wajibu Wako
KATIBU
MKUU
WIZARA
YA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUN DI
Benki ya Dunia Kusaidia Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa Katika Sekta ya Elimu
Serikali
ya Tanzania na Benki ya Dunia wamesaini makubaliano ya mkopo wa Shilingi
bilioni 203 za Kitanzania (Dola za Marekani milioni 122) kwa ajili ya kusaidia, kukuza na kuendeleza Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu wenye lengo la kuimarisha na
kuboresha elimu ya msingi na sekondari.
Makubaliano
hayo yalitiwa saini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Dkt. Servacius
Likwelile kwa niaba ya Serikali na Benki
ya Dunia iliwakilishwa na Mkurungezi Mkazi wa Benki hiyo nchini, Philippe
Dongie. Makubaliano hayo yamefanyika leo jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi Dkt.
Servacius Likwelile amesema fedha zilizopatikana zitasaidia Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu kuboresha ubora wa Elimu ya Msingi na
Sekondari.
Aidha,
Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa katika Elimu umelenga
pamoja na masuala mengine Kuimarisha ufaulu na kuboresha uwazi shuleni kwa
kupitia upangaji wa shule kitaifa kwa kuzingatia matokeo ya mitihani kwa shule
za msingi na sekondari kwa kuzingatia ubora wa ufaulu na kutekeleza upimaji wa
ujuzi wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa darasa la pili katika
shule zilizochaguliwa.
Mpango
huo pia umelenga kutoa motisha kwa shule
zote za Msingi na Sekondari zilizoonyesha maendeleo katika ufaulu na zilizofanya vizuri ili kuboresha viwango vya ufaulu na kutoa motisha zisizo za
kifedha na kuondoa madai ya muda mrefu ya walimu wa shule za Msingi na Sekondari ili Kuondoa malalamiko
ya walimu hao.
Aidha,
Dkt. Likwelile alisema Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa umelenga kuzisaidia shule
na kuondoa ugawaji wa rasilimali usiozingatia usawa kwa kutengeneza na
kusambaza vifaa vya kujifunzia kwa vitendo kwa shule za Msingi na Sekondari,
kuandaa Mafunzo ya KKK kwa walimu wa shule za Msingi, utekelezaji wa programu ya kujenga uwezo wa walimu na
wanafunzi katika ufundishaji na
Ujifunzaji na kuboresha mfumo wa ufuatiliaji wa Ruzuku za Uendeshaji wa Shule.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Mwakilishi wa Benki ya Dunia aliipongeza Tanzania kwa kupata
mkopo huo na kuitaka Serikali kutumia vizuri fedha ilizozipata kama ilivyokusudiwa ili kuboresha Elimu nchini.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
Profesa Sifuni Mchome, ameishukuru Benki ya Dunia kwa fedha itakayotolewa
ambayo itasaidia katika kuhakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) katika sekta ya Elimu unafanikiwa.
Aidha,
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dkt. Deo Mutasiwa
alisema Wizara yake imejiandaa kikamilifu kuhakikisha kuwa fedha zitakazopatikana
zinatumika kama zilivyokusudiwa na kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Jisajili kwenye:
Machapisho (Atom)