Jumatano, 9 Agosti 2017

TANGAZO LA NAFASI ZA KAZI KWA WALIMU WA SHULE ZA MSINGI NA SEKONDARI.



1.0     Serikali inatarajia kuajiri Walimu 92 wa Shahada na 174 wa Stashahada wa masomo ya Fizikia, Hisabati, Kilimo na Biashara kwa Shule za Sekondari na Walimu 2,767 wa Cheti kwa Shule za Msingi.

2.0     Waombaji kwa shule za Sekondari wawe waliohitimu mafunzo ya Ualimu mwaka 2016 au kabla, na wale wa Shule za Msingi wawe waliohitimu mafunzo yao mwaka 2014 au kabla. 

3.0     Sifa za Waombaji:

3.1     Walimu wa Sekondari:
(i)          Shahada ya Elimu (Bachelor with Education) au Shahada ya Ualimu (Bachelor of Education) yenye somo moja la kufundishia au zaidi au Shahada isiyo ya Ualimu/Elimu yenye somo moja la kufundishia au zaidi pamoja na Stashahada ya Uzamili ya Elimu (Postgraduate Diploma in Education) kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu vinavyotambulika na Serikali. Masomo ya kufundishia ni kati ya Fizikia, Hisabati, Kilimo au Biashara.
(ii)        Stashahada ya Ualimu katika masomo yaliyoainishwa kwenye kipengele Na. 2.1 (i) hapo juu.
(iii)      Cheti cha Kidato cha Sita
(iv)       Cheti cha Kidato cha Nne

3.2     Walimu wa Shule za Msingi:
(i)          Astashahada ya Ualimu iliyotolewa na Chuo kinachotambuliwa na Serikali.
(ii)        Cheti cha Kidato cha Nne (wenye cheti Kidato cha Sita watapewa kipaumbele).

4.0     Utaratibu wa Kutuma Maombi:
(a)        Maombi yatumwe kupitia Posta kwa njia ya Rejesta (EMS).  Juu ya bahasha iandikwe kwa mkono "Maombi ya Kazi ya Ualimu - Sekondari au Maombi ya Kazi ya Ualimu - Msingi".

(b)        Mwombaji aambatishe nakala za Vyeti vilivyothibitishwa (Certified) na Mwanasheria pamoja na "Transcript".

NB:  Barua za maombi zisiwasilishwe kwa mkono.  Barua zitakazowasilishwa kwa mkono hazitapokelewa.


5.0     Masuala Mengine ya Kuzingatia:
(a)        Mwombaji aandike majina yake yote matatu.  Kama Vyeti vina majina mawili, utaratibu wa kisheria wa kuongeza jina uzingatiwe.
(b)        Mwombaji aambatishe nakala ya Cheti cha Kuzaliwa.

Mwisho wa kupokelewa maombi ni tarehe 31/08/2017.

Maombi yatumwe kwa:
Katibu Mkuu,
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
             S. L. P. 10,
           40479 DODOMA.           

Imetolewa na:

KATIBU MKUU

WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA

Alhamisi, 27 Julai 2017

Waziri Mkuu afungua Maonyesho ya 12 ya Vyuo vya Elimu ya Juu


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassimu Majaliwa Majaliwa ameitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania TCU kuhakikisha programu za masomo zinazoanzishwa na Vyuo vya elimu ya juu nchini zinazingatia mahitaji ya Taifa na soko la ajira.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo katika ufunguzi wa maonyesho ya kumi na mbili (12) ya vyuo vya elimu ya juu yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam ambapo amesema serikali inayathamini maonesho hayo kwa kuwa yanatoa fursa ya vijana kujifunza na kupata taarifa za vyuo na programu wanazoendesha  moja kwa moja

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Saimon Msanjila ameitaka TCU kuhakikisha utaratibu uliotumika kufanya uhakiki wa vyuo na programu na kupelekea baadhi ya vyuo na programu kufungiwa utumike huohuo kuhakiki pindi vitakaporekebisha  mapungufu yaliyojitokeza awali. Aidha, amevitaka vyuo vyote vilivyofungiwa kupeleka TCU majibu ya maeneo  walioambiwa yana mapungufu  kama utaratibu unavyotaka badala ya kuyapeleka Wizarani.






Ijumaa, 21 Julai 2017

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia ampongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kwa kusimamia vizuuri ujenzi wa miundombinu ya shule


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya amempongeza Mkuu wa Wilaya ya Korongwe Mhandisi Robert Gabriel kwa kuhamasisha wananchi kuchangia katika sekta ya elimu ambapo mchango huo wa wananchi umewezesha mradi wa ujenzi madarasa uliofadhiliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia mradi wa Mradi wa lipa kulingana na matokeo kufanikiwa kwa kiwango kikubwa pamoja na ujenzi wa miundombinu mengine ya elimu inayofanywa na Halmashauri.

Mhandisi Manyanya ametoa pongezi hizo leo wilayani Korongwe Mkoani Tanga katika wakati wa ziara yake wilayani humo yenye lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati unaofanywa na Mradi wa Lipa kwa Matokeo (P4R). Amesema Mkuu wa wilaya huyo pamoja na kamati yake wameweza kuhamasisha wananchi kuchangia katika mradi huo na kuwezesha kujengwa madarasa zaidi ya yaliyokuwa yamelengwa hapo awali kwani wananchi walichangia nguvu kazi zao, mifuko ya saruji na vifaa vinine vya ujenzi.

Naibu Waziri ametolea mfano wa ujenzi wa miundombinu ya vyoo katika shule ya Msingi Kilimani ambapo wameweza kuijenga matundu ya vyoo 12 kwa gharama ya shilingi milioni 11 wakati sehemu nyingine ambazo ameshazitembelea wameshindwa kumaliza ujenzi wa vyoo kama hvyo kwa gharama hiyo.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korongwe Mhandisi Robert Gabriel amemueleza Naibu Waziri kuwa Halmashauri yake imejipanga kuhakikisha wanaondoa tatizo la miundombinu ya madarasa katika wilaya yake kwa kujenga madarasa 360 pamoja na ofisi za walimu 70 ndani ya kipindi cha miezi 12 kwa kutumia nguvu za wananchi.

Katika ziara hiyo Mhe Naibu Waziri alitembelea shule za Msingi Kilimani, Bagamoyo, Matondoro, Kilole, Kwasemangube, Shule ya Sekondari Semkiwa pamoja na Chuo cha Ualimu Korogwe.











Ijumaa, 14 Julai 2017

Naibu Waziri wa Elimu akagua ujenzi na Ukarabati katika shule ya Sekondari Mbweni Tete


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya ameonyesha kutokuridhishwa na hatua ya Halmashauri ya Kinondoni kuhamisha fedha za ujenzi wa madarasa, mabweni na vyoo zilizokuwa zimetolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknlojia kupitia mradi wa lipa kwa matokeo kwa shule ya Sekondari ya Kambwangwa na kupelekwa katika Shule ya sekondari Mbweni tete bila kufuata utaratibu wa kuitaarifu wizara iliyotoa fedha hizo.

Mhandisi Manyanya ameyaeleza hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kuzitembelea shule mbalimbali kwa lengo la kukagua utekelezaji wa ujenzi na ukarabati unaofanywa na Mradi wa Lipa kwa Matokeo (P4R). Amesema kuhamishwa kwa mradi si tatizo lakini kuhamisha bila kutoa taarifa ndo tatizo lilipo kwani wizara imetoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi huo hivyo ni lazima kufanya ufatiliaji ili kuweza kujirizisha kama ujenzi unafanyika lakini wakati najiandaa kwenda Kambagwa ndipo alipotaarifa kuhusu kuhamishwa kwa  mradi huo.

“Leo wakati tunataka kuanza kwenda kuangalia ujenzi ulipofikia lakini tukapewa taarifa kuwa mradi huo haupo Kambangwa na ulihamishwa kupelekwa eneo jingine, hivyo ni muhimu kupeana taarifa maana kuhamishwa kwa mradi kunaleta hoja za ukaguzi” alisisitiza Mhandisi Manyanya.

Naibu Waziri amesema ujenzi wa miundombinu hiyo katika Halmashauri mbali mbali imekuja baada ya wizara ya Elimu kwa kushirikiana na TAMISEMI uwepo wa umuhimu wa kuongeza  miundombinu ya madarasa, mabweni na vyoo katika baadhi ya shule ili kuongeza idadi ya wanafunzi  wanaodahili kwa ajili ya kujiunga na masomo ya kidato cha tano. Amesma lengo la serikali ni kuona wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kuendelea na masomo yao ya kidato cha tano bila mmoja kuachwa.




Naibu Waziri wa Elimu agiza shule zilizotengwa kwa ajili ya elimu maalum kupatiwa mahitaji muhimu


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha shule zilizotengwa kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum zinapewa haki zake ikiwa ni pamoja na kupatiwa vifaa vya kufundishia na kujifunzia  ili kuwezesha wanafunzi hao kupata elimu sawa na wanafunzi wengine.

Naibu Waziri Manyanya ametoa agizo hilo alipofanya ziara kwenye shule ya msingi  Sinza Maalum iliyopo jijini Dar es Salaam kwa lengo la kujionea mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji katika shule hiyo, mbapo  pia amezitaka halmashauri hizo kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni yatakayosaidia kupunguza ugumu wa wanafunzi hao kuhudhuri masomo  kutokana na sababu mbalimbali za kimaumbile za watoto hao na hivyo kuwafanya wengine kushindwa kutembea umbali  mrefu kufuata shule.

Pia Naibu waziri alitembelea shule ya sekondari ya Mbweni Teta kukagua ujenzi wa madarasa, mabweni na vyoo unaofanywa na Wizara ya Elimu, Sayasni na Teknolojia Kupitia Programu ya lipa kulingana na matokeo, P4R kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha Tano wanaotarajiwa kuanza shule Julai 17, mwaka huu.






Jumanne, 11 Julai 2017

Naibu Waziri wa Elimu akabidhi Bendera ya Taifa kwa wanafunzi wa Sayansi


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya leo amekabidhi Bendera ya Taifa kwa wanafunzi saba wanaosoma masomo ya sayansi wanaokwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya First Global Challenges nchini Marekani. Makabidhiano hayo yamefanyika katika shule ya Sekondari ya  wasichana Jangwani.

Katika makabidhiano hayo Mhandisi Manyanya amewataka wanafunzi wote nchini kusoma kwa bidii masomo ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuhakikisha ndoto ya Tanzania ya kuwa na uchumi wa kati kupitia viwanda na biashara inafanikiwa na kwamba wizara tutaendelea na jukumu lake la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili wanafunzi wote waendelee kufanya vizuri katika masomo ya sayansi.

Shule zilizotoa wanafunzi watakaoshiriki katika mashindano hayo ni pamoja na Jangwani, Azania, Jamhuri, Benjamini Mkapa, Feza na Kisutu.

Naye mratibu wa mashindano hayo kwa upande wa Tanzania ndugu Mkufu Shabani Tindi alisema mashindano haya yameanzishwa na kufadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Marekani liitwalo FIRST yenye maana ya for inspiration and recognition of science and technology lenye lengo la kuhamasisha ulimwenguni kote vijana wanaosoma masomo ya sayansi, uhandisi, teknolojia na hesabu kuweza kutatua changamoto mbalimbali ulimwenguni

Wanafunzi watakaoshiriki wanatarajia kuondoka kesho Juni 12, 2017 na watakuwa nchini Marekani kwa ajilia ya mashindano hayo makubwa  kiulimwengu ambapo  zaidi ya nchi 170 zitashiriki.

Naye mmoja wa washiriki Raymond Benedict kutoka Shule ya Sekondari Jamhuri amesema yeye wenzake wamejiandaa vizuri katika kuhakikisha wanaiwakilisha nchi katika mashindano hayo vizuri na kwa ufahari.