Jumatatu, 30 Julai 2018

WATHIBITI UBORA WA SHULE NCHINI WAPATIWA MAFUNZO YA MFUMO MPYA WA UKAGUZI WA SHULE


Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kutoa mafunzo kwa wathibiti ubora wa shule kote nchini ya namna ya kutekeleza mfumo mpya wa Uthibiti Ubora wa Elimu.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Jijini Dodoma Mthibiti Mkuu wa Shule kutoka Wizara hiyo Euphrasia Buchuma amesema mfumo huo unaondoa mfumo ambao wathibiti ubora wamekuwa wakitazamwa kama polisi pindi wanapofika shuleni na kuwa watu ambao wanatakiwa kutoa msaada katika shule.

Buchuma amesema mfumo huo mpya unashirikisha jamii nzima ya shule Viongozi wote, Wazazi, Kamati za Shule, Bodi ya shule na walimu ambao wanapaswa kufahamu Mthibiti Ubora wa Shule anapoingia katika Shule anafanya nini katika shule hiyo na taarifa za ukaguzi ni lazima ziwafikie viongozi wote wenye mamlaka na kutoa maamuzi.

Amesema kwa kuwa mfumo huu ni shirikishi unaleta uwazi zaidi na kuondoa usiri ambao ulikuwapo katika mfumo uliokuwa ukitumika zamani katika kukagua shule ambao uliitaji usiri kuanzia unapokagua shule uandikaji wa ripoti na hata uwasilishaji wa taarifa ya ukaguzi.

Mthibiti Mkuu wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchuma akiongea na Wathibiti Ubora wa Shule wakati wa ufunguzi wa mafunzo eelekezi ya namna ya kutumia mfumo mpya wa ukaguzi wa Shule Jijini Dodoma.

Amewataka wathibiti ubora wa shule kushiriki mafunzo hayo kikamilifu kwa kuwa wana dhamana kubwa ya Elimu na kwamba kila mmoja kwa nafasi yake atambue wajibu wake, abadili mtizamo, afanye kazi kwani kunahitajika mabadiliko makubwa katika kuhakikisha Elimu ya nchi hii inatolewa kama inavyopaswa kutolewa.

“Tumekuwa tukinyooshewa vidole sana kwamba hatufanyi kazi na ni kwa sababu matokeo yanaonekana kama hatupo kumbe tupo, hatuonekani katika utendaji kazi na ndio maana kila panapotokea tatizo tunaonekana hatupo na hatufanyi kazi tubadilike tufanye kazi kwa moyo, bidii na weledi,” alisisitiza Buchuma
Baadhi ya Wathibiti Ubora wa Shule wakifuatilia hotuba ya Mthibiti Mkuu wa Shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Euphrasia Buchuma wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekeze kwa Wathibiti Ubora wa Shule ya nama ya kutumia mfumo mpya wa ukaguzi wa Shule.
                                    
Katika hatua nyngine Buchuma amewataka wathibiti ubora wa shule mara baada ya mafunzo hayo kukamilika, wahakikishe wanakagua Shule zote za Sekondari ambazo ni Kongwe kwani zinaonesha kutofanya vizuri katika miaka ya hivi karibuni.

“leo ukienda katika shule nyingi ukiukwaji wa sheria za Shule ni mkubwa lakini na sisi tupo na hatusemi tunasema hatuhusiki, kimsingi sisi ndio wasimamia Sera, Miongozo, taratibu na kanuni zote za uendeshaji wa shule kuanzia ngazi ya Shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Ualimuhivyo tukafanye kazi,” aliongeza Buchuma

Mafunzo elekezi ya namna ya kufanya ukaguzi kwa mfumo mpya wa uthibiti ubora wa Shule yanafanyika kwa siku nne kuanzia Julai 30, mwaka huu nchi nzima.

Jumamosi, 21 Julai 2018

OLE NASHA AZITAKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KUZINGATIA UBORA WA MAFUNZO WANAYAYOTOA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha  amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuzingatia suala la ubora wa mafunzo wanayoyatoa katika programu zao ili kupata wahitimu wenye ujuzi unaotakiwa kwenye uchumi wa viwanda.

Naibu Waziri Ole Nasha amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga   Maonesho ya 13 ya Elimu ya Juu ambapo amesema Serikali ina mategemeo makubwa ya kupata rasilimali watu bora itakayofanya kazi katika viwanda hivyo suala la ubora wa mafunzo linahitaji kupewa kipaumbele.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akizungumza na wanashiriki (Hawapo pichani) katika maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu wakati wa kufunga wa maonesho hayo katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es alaam.

“Tunataka mzalishe wahitimu wanaoonekana wamepata Elimu bora na si bora Elimu ambao wataweza kufanya kazi kulingana na mahitaji na matarajio ya taifa letu lakini pia watakaokidhi vigezo na matarajio ya wadau mbalimbali,” Alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha.


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akisikiliza ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya elimu  kutoka kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Alisema wizara yake itaendelea kusimamia na kufuatilia kwa karibu zaidi suala la ubora wa Elimu katika ngazi zote na kuzitaka Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha inafuatiali vyuo kwa karibu ili kuhakikisha wanafuata miongozo iliyopo na kwamba Serikali haitavumilia taasisi au mtu yeyote anayejaribu kukiuka miongozo hiyo kwa sababu yoyote ile.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Wiliam Ole Nasha akikabidhi cheti cha ushiriki kwa mmoja wa wadau wa Elimu ya Juu walioshiriki maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Maonesho ya Elimu ya Juu yamehitimishwa leo na yalikuwa na kauli mbiu ELIMU YA JUU BORA KWA MAPINDUZI YA VIWANDA


Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka akijadiliana masula mbalimbali kuhusu Elimu na baadhi ya washiriki wa maonesho ya Elimu Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia yaliyofanyika jijini Dar es Salaam 

Alhamisi, 19 Julai 2018

WIZARA YA ELIMU YAKABIDHI MAGARI 47 KWA WADHIBITI UBORA WA SHULE


Wathibiti Ubora wa Shule nchini wametakiwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa taaluma shuleni kwani matokeo bora ya ujifunzaji yanahitaji usimamizi na tathmini ya mara kwa mara.

Hayo yameelezwa leo mkoani Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako wakati wa hafla ya kukabidhi magari 45 kwa Wathibiti Ubora wa Shule wa Kanda na Wilaya na magari 2 kwa ajili ya Baraza la Mitihani Tanzania.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji magari kwa Wathibiti Ubora wa Shule Kanda na Wilaya, pamoja na Baraza la Mitihani la Tanzania. Amesisitiza matumizi bora ya magari hayo ili yaweze kutimiza lengo lililokusudiwa.

Waziri Ndalichako amesema lengo la Taifa ni kuwa na watu walioelimika,  mahiri na wabunifu katika  kuelekea uchumi wa viwanda ifikapo 2025, hivyo ili kufikia malengo hayo  usimamizi wa karibu na tathmini ya mara kwa mara inahitajika.

Waziri Ndalichako amewasisitiza Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanafanya  ufuatiliaji wa karibu wa kitaaluma ikiwa ni pamoja na kuhakikisha  walimu wanafika  shuleni  kwa  wakati  wanaingia  kwenye  vipindi  na wanafundisha.

 “Nataka nione mnasimamia kwa karibu taaluma na nataka  kuona  mabadiliko makubwa katika shule zetu za   Serikali  kuanzia  upande  wa  nidhamu na  taaluma ili mabadiliko yaweze kujitokeza  kwenye Shule zetu,  na tuone shule zetu  zinafanya vizuri katika matokeo ya Taifa ya kidato  cha  Nne,’’ alisisitiza Prof. Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa magari ambayo ameyagawa kwa Wathibiti Ubora wa Shule ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.


Profesa Ndalichako ametaka magari hayo kutotumika katika malengo yasiyokusudiwa badala yake yatumike tu kwa ufuatiliaji wa taaluma shuleni.

“Haya ni magari kwa ajili ya ufuatiliaji wa Elimu, ninaagiza magari haya yasitumike kwa matumizi mengine yoyote tofauti na masuala ya Elimu, naomba hili likazingatiwe sana na yeyote atakayekikuka hatua za kinidhamu  zitachukuliwa,”alisisitiza Waziri Ndalichako.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua moja ya gari lililonunuliwa na Wizara kama nyenzo na kitendea kazi kwa Wathibiti Ubora wa  Shule.



Pia Waziri Ndalichako amewataka Wakuu   wa  Shule  kuendelea  kusimamia  nidhamu  na kutowaonea huruma  wanafunzi wanaokiuka taratibu za Shule  kwani Serikali haitakuwa  na huruma na watendaji pale mambo yatakapokuwa hayaendi vizuri. 

“Angalieni  Mkuu wa Shule ya Sekondari Jangwani ameng’oka  kwa  hiyo  Serikali haitakuwa na huruma nanyi  pale mtakapowalea wanafunzi wenye 
utovu wa nidhamu Shuleni, wanafunzi hawatakiwi kuwa na simu shuleni  lakini bado wanafunzi wameendelea kuwa na simu, hakikisheni mnasimamia maadili na nidhamu za wanafunzi kwa mujibu wa taratibu zinavyoelekeza.

Mapema mwanzoni mwa Mwezi Julai Wizara iligawa pikipiki 2,894  kwa  ajili ya Waratibu Elimu kata ikiwa ni muendelezo wa kutatua changamoto ya usafiri kwaWathibiti Ubora ili wazeze kufikia shule zote na kufuatilia  hali  ya ufundishaji shuleni.
Baadhi ya Magari ambayo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imenunua kwa ajili ya Wathibiti Ubora wa Shule Kanda na Wilaya pamoja na Baraza la Mitihani  Tanzania

Jumatano, 18 Julai 2018

NDALICHAKO AZITAKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU ZENYE MAPUNGUFU ZIJIREKEBISHE


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amezitaka Taasisi za Elimu ya Juu nchini ambazo matokeo ya uhakiki yalibainisha kuwa na mapungufu kurekebishe kasoro hizo kama walivyoelekezwa na Mamlaka husika.

Waziri Ndalichako ametoa  agizo hilo Leo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi   wa Maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu ambapo amesema taasisi hizo zisipofanya hivyo basi hatua stahiki zitachukuliwa, ikiwa ni pamoja na kufutiwa usajili.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa Elimu ya Juu (hawapo pichani) ambao wanashiriki katika maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es alaam ambapo amezitaka Taasisi zote za Elimu nchini kuzingatia ubora wa Elimu wanayoitoa.

Waziri  Ndalichako pia amewaagiza Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuendelea kusimamia kwa karibu na kwa  umakini masuala yote yanayohusu ubora wa Elimu inayotolewa na Taasisi za Elimu ya Juu.

” Katika Awamu hii ya Tano watu wanaofanya kazi kwa mazoea hawana nafasi, lazima muwe wabunifu nampitie upya zana mnazotumia kuhakiki ubora wa vyuo. Haiwezekani kila siku tunasikia malalamiko kuhusu ubora wa wahitimu wakati TCU na NACTE mpo” amesisitiza Prof. Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe wakisikiliza ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya elimu  kutoka kwa mmoja wa washiriki wa maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo washiriki hao wametakiwa kujitadhimini kuhusu utoaji wao wa Elimu ya Juu 

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo  Prof. James Mdoe amesema maonesho hayo ya Elimu ya Juu yatazisaidia Taasisi mbalimbali za Elimu kujitathmini na kupata mrejesho kutoka  kwa wadau namna  wanavyotekeleza majukumu yao.

Maonesho ya Taasisi za Ellimu ya Juu ambayo yatafanyika kwa siku nne yanalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu fursa zinazopatikana kwenye Taasisi za Elimu ya  Juu,  kutoa nafasi kwa wananchi wanaotarajia kujiunga na Elimu ili elimu ya kujiridhisha na programu za masomo na huduma zinazotolewa.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. James Mdoe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Tume ya Vyuo Vikuu ambao ni waandaaji wa maonesho ya kumi na tatu ya Elimu ya Juu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Jumanne, 17 Julai 2018

SERIKALI YAZINDUA MFUKO WA KUENDELEZA UJUZI


Serikali imezindua Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi.

Akizindua Mfuko huo Jijini Dar es Salaam Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema mfuko huo unalenga kuboresha stadi za kazi, uwezo wa kujiajiri na kuchangia ongezeko la wataalam  wenye stadi mbalimbali katika taaluma za Kilimo, Utalii, Nishati, Ujenzi, Uchukuzi na TEHAMA.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wadau wa Elimu (hawapo pichani) waliohudhuria uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) Jijini Dar es Salaam utakaowezesha watoa huduma za mafunzo ya ufundi katika ngazi mbalimbali kutoa mafunzo yenye tija yatakayoweza kukuza stadi za kazi uliofanyika.

Prof. Ndalichako amesema katika kuleta ufanisi wa kukuza ujuzi Wizara yake itaanzisha kwa mara ya kwanza Baraza la Taifa la Ujuzi (National Skills Council – NSC) ambalo litasimamia mabaraza ya kisekta ya kukuza ujuzi (Sectoral Skills Council).

“Tayari Wizara ina makubaliano rasmi ya ushirikiano (MoU) na Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) itakayosaidia uanzishwaji wa mabaraza hayo na  Baraza la Taifa la Ujuzi (NSC) litakuwa waangalizi wa mfuko huu wa SDF tunaouzindua leo, hivyo sekta binafsi itakuwa na fursa ya kutoa mchango wake katika ukuzaji ujuzi hapa nchini. “alisisitiza Prof. Ndalichako



Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leonard Akwilapo akizungumza na washiriki wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika jijini Dar es Salaam ambapo amewataka wote watakaopata fedha za Mfuko huo kuzitumia kwa malengo yaliyowekwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Dk. Erasmus Kipesha amesema Taasisi yake ina jukumu la kuusimamia Mfuko huo na imedhamiria kuhakikisha kuwa rasilimali zilizoelekezwa katika Mfuko huo zinatumika kwa weledi, taratibu, haki, ubora, na ufanisi wa hali ya juu.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania Dk. Erasmus Kipesha mfano wa hundi kwa ajili ya Taasisi za Elimu ya Ufundi zitakazoshiriki katika kukuza na kuendeleza ujuzi. Makabidhiano hayo yamefanyika wakati wa uzinduzi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Jumatano, 11 Julai 2018

WAZIRI NDALICHAKO AMTAKA KATIBU MKUU WIZARA YA ELIMU KUWACHUKULIA HATUA WALIOHUSIKA NA SAKATA LA VIFAA VYA MAABARA CHUO CHA UALIMU KASULU


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amemtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuwachukulia hatua wale wote waliohusika na uagizaji na upokeaji wa vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Wilayani Kasulu mkoani Kigoma.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo Wilayani Kasulu alipofanya ziara katika Chuo hicho na kukuta idadi kubwa ya kemikali za maabara zisizohitajika lakini pia vifaa vya maabara kutokuwa na ubora huku chuo kikiomba kununuliwa tena vifaa vya maabara na kemikali.

“Haiwezekani kwa sasa manasema mna upungufu wa vifaa pamoja na kemikali wakati mmevijaza hapa chuoni tena kwa utaratibu usiofaa, huku mkisema vitaharibika kwa kuwa havihitajiki, ni nani aliviagiza na ni kwanini mliviagiza bila ya kuwa na uhitaji, kwa hili sio la kufumbia macho ni lazima hatua zichukuliwe kwa wale wote waliohusika katika suala hili”alisema Profesa Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipokelewa na Mwenyekiti wa Bodi pamoja na Watumishi wa Chuo cha Ualimu Kasulu kilichopo Mkoani Kigoma wakati alipowasili chuoni hapo. 
Waziri Ndalichako pia ameitaka Idara ya Elimu ya Ualimu katika Wizara hiyo pamoja na Chuo cha Ualimu Kasulu kutoa taarifa ya kina ya uagizaji na upokeaji wa vifaa hivyo kwa kuwa kumekuwepo na kutokuelewana baina yao ni nani alitoa mahitaji halisi ya vifaa hivyo hali iliyoisababishia Serikali hasara ya kununua vifaa visivyohitajika wakati zipo shule za Sekondari zingeweza kupata vifaa hivyo.

“Bahati mbaya bodi yenu haina taarifa ya manunuzi haya, wakuu wa vyuo muache tabia ya kuficha mambo yanayoendelea chuoni hapa nachukua hatua na bodi iangalie hatua za kuchukua hatuwezi kuruhusu mtu anayefanya uhalifu huu akabaki salama,” alisema Profesa Ndalichako.
Wzairi wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua kemikali za Maabara katika Chuo cha Ualimu Kasulu

Awali Mkuu wa Chuo cha Ualimu Kasulu Josephat Mwangamila katika hotuba yake alisema Chuo hicho kina deni la takribani shilingi milioni 64 kwa ajili ya ununuzi wa Kemikali na Vifaa kwa ajili ya matumizi ya ofisi (stationary) kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha sita waliofanya mitihani.

Mkuu wa Chuo alisema walifikia uamuzi wa kununua kemikali hizo kwa kuwa hawakuwa nazo chuoni hapo lakini pia zilizokuwepo hazihitajiki kwa matumizi chuoni hapo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya majengo ya Chuo Cha Ualimu Kabanga Mkoani Kigoma. Akiwa Chuoni hapo Profesa Ndalichako amezungumza na wakufunzi pamoja na watumishi wa chuo na kuahidi kujenga upya Chuo hicho kwa kuwa miundombinu yake imechakaa. 

Serikali imenunua vifaa vya maabara  vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni Moja ambavyo vimesambazwa katika vyuo vyote vya ualimu nchini ikiwa ni juhudi za kuhakikisha walimu wanapata mafunzo kwa vitendo ili wakaweze kufundisha kwa umahiri pindi wanapomaliza masomo yao.

Waziri wa Elimu pia ametembelea Chuo cha Ualimu Kabanga ambapo ameahidi kujenga upya chuo hicho katika mwaka wa fedha ulioanza 2018/19 kwa kuwa majengo yake ni chakavu na kuvitaka vyuo ambavyo vimekarabatiwa kuwa na dhamira ya dhati ya kutunza miundombinu ya vyuo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akikagua miundombinu ya ngazi za mabweni ambayo imechakaa katika Chuo Cha Ualimu Kasulu, Wilayani Kasulu Mkoani Kigoma