Ijumaa, 17 Agosti 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA ARIDHISHWA NA UKARABATI WA CHUO CHA UALIMU NACHINGWEA


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mheshimiwa William Ole Nasha ametembelea Chuo Cha Ualimu Nachingwea na kuridhishwa na kiwango cha ukarabati kinachoendelea ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kimetolewa kwa ajili ya ukarabati huo. 

Akizungumza na watumishi katika Chuo hicho Naibu Waziri Ole Nasha amepongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha sita kwa mwaka 2018 kwa mkoa wa Lindi kushika nafasi ya pili Kitaifa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na Wazazi pamoja na Walimu (hawapo pichani) wa Shule ya Sekondari Nachingwea Mkoani Lindi mara baada ya kufanya ziara shuleni hapo. 

Naibu Waziri pia amewataka walimu kuhakikisha wanasimamia, wanahamasisha na kuelimisha jamii kuachana na  mila na desturi potofu zinazochangia watoto kuacha shule ikiwa ni pamoja na kushiriki katika unyago.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole Nasha ametembelea na kuipongeza Halmashauri kwa kuwa na wazo la kuwa na Shule ya Sekondari ya wasichana Nachingwea na kuwa hiyo itasaidia watoto wa kike kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafunzi kutembea umbali mrefu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa na Viongozi mbalimbali wa Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi akikagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na Wizara mara baada ya kupokelewa Chuoni hapo.

Mheshimiwa Ole Nasha amesema wazazi na wadau wana wajibu wa kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vinavyowanyima fursa, ambapo amewataka Walimu kuhakikisha wanasimamia wanafunzi ili waweze kufikia malengo yao.

Naibu Waziri ameahidi kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa viwili na nyumba 2 za walimu ili kupunguza changamoto za shule hiyo.
Muonekano wa Jengo la darasa lililokarabatiwa katika Chuo cha Ualimu Nachingwea Mkoani Lindi. Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameridhishwa na namna ukarabati wa jengo hilo ulivyofanyika.  

Alhamisi, 16 Agosti 2018

DK. SEMAKAFU: WATHIBITI UBORA NA MAAFISA ELIMU FANYENI UFUATILIAJI SHULENI


Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semakafu amewataka Maafisa Elimu na Wathibiti ubora kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji na kutoa taarifa kwenye Mamlaka zinazohusika ili changamoto hizo ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Dk. Semakafu ametoa kauli hiyo leo Wilaya Magu mkoani Mwanza wakati akishiriki zoezi la ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na washirika wa Maendeleo kuhusu ufundishaji na ujifunzaji AJESR.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Ave Maria Semkafu akizungumza na timu ya ufuatiliaji wa Maendeleo ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni (Hawapo Pichani), Wilayani Magu, mkoani Mwanza.

Dk. Semakafu amesema suala la ufuatiliaji kwa viongozi waliopewa Mamlaka ni la lazima kwani itasaidia zaidi kubaini changamoto lakini pia ni sehemu ya uwajibikaji katika kutimiza malengo ya Taifa.

“Viongozi ni lazima tuwajibike katika kushughulikia masuala ya wananchi na siyo kusubiri kiongozi wa juu aje atoe maelekezo ndiyo tuanze kukimbizana, mfano wewe mthibiti ubora wa shule, au Afisa Elimu unakagua shule zako? unatatua changamoto au unasubiri mpaka Mkurugenzi wa Halmashauri atoe maelekezo?” Alisisitiza Dk. Semakafu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Lutengano Mwalwiba ameahidi kuendelea kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizopo katika Halmashauri hiyo ili Taifa liweze kusonga mbele.
Baadhi ya wajumbe wa timu ya ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa na washirika wa Maendeleo wakipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Lutengano Mwalwiba, Mkoani Mwanza.

Amesema hakuna jambo ambalo litaweza kuwa mbadala wa Elimu, Elimu ni kila kitu sasa ikivurugwa Elimu Taifa haliwezi kusonga mbele.

“Tukiwa na misingi mizuri ya Elimu lazima Taifa tutafanikiwa, changamoto zipo na ndiyo maana viongozi tupo kama changamoto zisingekuwepo basi hata viongozi tusingekuwepo,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Naibu Katibu Mkuu Dk. Semakafu akipokelewa katika Kituo Cha Ufundi Ihushi kilichopo Wilayani Magu, mkoani Mwanza

NDALICHAKO AITAKA VETA MAKAO MAKUU KUPELEKA FEDHA KATIKA WILAYA NA MIKOA


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako ameigiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) kuhakikisha inapeleka fedha kwa wakati katika ofisi za Kanda na Vyuo vya  Wilaya na Mikoa ilikuharakisha utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Mamlaka hizo.

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani Katavi ambapo amesema VETA kanda, Mikoa na Wilaya zimekuwa na changamoto za kujiendesha kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha.
Waziri, Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akifalishwa skafu na Mwanafunzi wa Chuo cha VETA Mpanda  ikiwa ni ishara ya kumkaribisha katika Chuo hicho. Waziri Ndalichako aliwashauri vijana na wanafunzi kujiunga katika vikundi vya skauti ili kujiepusha na kujiingiza katika makundi hatarishi

Amesema amesikitishwa kuona baadhi ya mitambo katika Chuo cha VETA Mpanda iliyonunuliwa kwa gharama kubwa na Serkali haifanya kazi kwa kukosekana fedha kidogo za ufungaji wa mitambo hiyo katika karakana za chuo hicho .

“Ukiangalia VETA za mikoani na wilayani zinahitaji fedhak kidogo tu ili zipige hatua lakini hazitolewi, naagiza VETA Makao Makuu kuhakikisha katika mipango yenu mhakikishe mnaweka usawa wa upelekaji fedha kwa VETA zote nchini ili nazo ziweze kupiga hatua katika kutoa mafunzo,”amesema Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya mitambo katika moja ya karakana za Chuo cha VETA Mpanda alipokuwa katika ziara ya kukagua miradi ya Elimu katika Mkoa wa Katavi. Waziri ameitaka VETA Makao Makuu kuhakikisha mitambo yote katika Vyuo vya Wilaya na Mikoa inafanya kazi .

Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako ameahidi kutoa cherehani mbili kwa wanafunzi Gift Giles na Benitha William wwenye umri wa miaka kumi na tano ambao wamejiunga katika Chuo cha VETA Mpanda baada ya kutokuchaguliwa kuendeleana masomo ya kidato cha kwanza.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Amos Makala amenuahidi Waziri kuwa atakisimamia Chuo cha VETA Mpanda ili kiweze kuwa na tija kwa wanakatavi.

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA CHUO CHA VETA NKASI KUTOA MAFUNZO YA MUDA MFUPI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.  Joyce Ndalichako ameigiza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Kanda ya Kusini Magharibi kuhakikisha Chuo Cha Wilaya ya Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kinaanza kutoa mafunzo ya muda mfupi kuanzia  mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo akiwa ziarani mkoani Rukwa  kwa ajili ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa na wizara hiyo katika mkoa wa  Rukwa ambapo amesema majengo yaliyopo yanaweza kuendelea kutumika kutoa mafunzo ya muda mfupi huku serikali ikiendelea na utaratibu wa kufanya  ukarabati katika majengo hayo.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiangalia ramani ya Chuo Cha Wilaya ya Nkasi cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi wapofanya ziara katika majengo ya chuo hicho yaliyopo katika Wilaya ya Nkasi Mkoani Rukwa. Waziri aliagiza majengo hayo yaanze kutumika kwa kutoa kozi fupi.


Waziri Ndalichako amesema majengo hayo ni imara pamoja na kwamba hayajatumika kwa zaidi ya miaka mitatu lakini miundombinu ya majengo hayo bado ipo vizuri na inahitaji tu kupakwa rangi na kurekebisha  masuala ya umeme . 

“Ukiangali unaona raslimali ya serikali inapotea kuna majengo ambayo yangeweza kutumika kutoa mafunzo kwa vijana wa Nkasi ili kuwapatia ujuzi lakini hayatumiki, bado nasisitiza mtumie majengo haya kwa kuanzia yatumike kwa kutoa kozi za muda mfupi,”alisisitiza Waziri  Ndalichako
Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Magharibi Justine Ruta (Mwenye suti ya Khaki) akitoa ufafanuzi kuhusu Chuo cha VETA Nkasi kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akijadiliana na Mkuu wa Wilaya hiyo Iddi Kamanta 

Waziri Ndalichako amesema dhamira ya serikali ni kufikia vijana wengi katika kuwapatia ujuzi na maarifa na vijana wa Nkasi ni sehemu ya vijana hao wanahitaji kuwezeshwa kupata ujuzi na maarifa ili kuziona fursa nyingi za kimaendeleo.

Akiwa mkoani Rukwa Waziri Ndalichako pia ametembelea shule ya Sekondari ya Nkasi kwa lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa na wadau wa Elimu ambapo katika kuunga mkono juhudi hizo ametoa mifuko 100 ya simenti itakayosaidia katika ujenzi wa miundombinu hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Iddi Kimanta amesema serikali ya wilaya ipo tayari kushirikiana na VETA katika kuhakikisha Chuo hicho kinaanza mapema.

Jumatano, 15 Agosti 2018

SERIKALI KUJENGA MAJENGO MAPYA CHUO CHA UALIMU SUMBAWANGA

Serikali imesema itajenga majengo mapya ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga ili kukihamisha kutoka  kwenye majengo ya Kanisa Katoliki ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Joyce Ndalichako akiwa mkoani  Rukwa kwenye ziara  ya kukagua miradi ya Elimu inayotekelezwa katika mikoa ya Rukwa na Katavi ambapo amesema kwa sasa ni vigumu kufanyia ukarabati majengo yanayotumika kwa sababu si maliya serikali.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wanachuo, Wakufunzi na Wafanyakazi wa Chuo cha Ualimu Sumbawanga (Hawapo pichani) ambapo serikali imeahidi kujenga majengo mapya kwa ajili ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga

Waziri Ndalichako amesema suala la uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho lipo ingawa changamoto iliyopo ya eneo pamoja na majengo kuwa si mali ya chuo hicho na kwamba kanisa Katoliki wanalihitaji eneo hilo kwa matumizi mengine.

“Chuo Cha Ualimu Sumbawanga hakijasahaulika katika kufanyiwa ukarabati, changamoto iliyopo ni kuwa eneo hili mlikaribishwa lakini mkang’ang’ania sasa wenyewe wanataka eneo lao ” alisisitiza Waziri Ndalichako.

Aidha Waziri amesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19 kiasi cha shilingi bilioni 36 kimetengwa kwa  ajili ya kuvifanyia ukarabati vyuo saba vya Ualimu, huku Chuo Cha   Ualimu Murutunguru na Kabanga vikitarajia kujengwa upya.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokea taarifa ya Mkoa wa Rukwa kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dk. Khalifan Haule mara baada ya kufanya ziara ya Kikazi katika mkoa huo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo amesema anawashukuru Kanisa Katoliki jimbo la Sumbawanga kwa kuruhusu Chuo hicho kufanya shughuli zake katika eneo lake kwa muda mrefu, kwani mwanzoni kanisa hilo lilijenga majengo hayo ili kwa lengo la kuanzisha chuo cha kilimo.

Mkuu huyo wa mkoa amesema tayari  mkoa wake umeshatafuta eneo lingine ambalo Chuo hicho kitahamishiwa, na kuwa hivi sasa tayari Mkoa  umesharatibu taratibu  za kuanza kulipa fidia kwa wakazi ambao eneo Lao litachukuliwa kwa ajili ya matumizi ya Chuo hicho.


Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo akimuonyesha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako baadhi ya majengo ya Chuo cha Ualimu Sumbawanga









Alhamisi, 9 Agosti 2018

WAZIRI NDALICHAKO AIAGIZA NACTE KUFUNGIA VYUO VINAVYOTOA MAFUNZO KWA UBABAISHAJI


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako ameliagiza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuendelea kufungia vyuo vinavyotoa  mafunzo kwa ubabaishaji  ili kulinda ubora wa Elimu na Ujuzi kwa wanafunzi.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo Jijini Dar es salaam wakati akizindua Baraza la Uongozi la Taifa la Elimu ya Ufundi ambapo amewataka NACTE kufungia hata vyuo  vya serikali kama itabainika kutoa mafunzo yasiyo na ubora.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Baraza la Baraza la Uongozi la Taifa la Elimu ya Ufundi Prof. John Kondoro Sheria na Kanuni za Baraza hilo wakati wa uzindzi uliofanyika jijini Dar es Salaam

“Hatutaki kuwa na utitiri wa vyuo vingi ni bora kuwa na vichache lakini vitoe wahitimu wenye ujuzi na maarifa ambao wanaweza kuwa na mchango katika Taifa letu.” Amesisitiza Waziri Nalichako.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Leornald Akwilapo akizungumza na wananchi wa mtaa wa Majimatitu B Kata ya Kilungule mkutano huo ulifanyika katika viwanja vya shule mpya inayojengwa kwa ajili ya kupunguza mlundikano wa wanafunzi wa shule ya msingi Majimatitu A 

Pia Waziri Ndalichako amekagua Maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya Msingi inayojengwa Majimatitu Wilayani Temeke  yenye lengo la  kupunguza mlundikano wa wanafunzi katika shule ya Msingi Majimatitu A yenye wanafunzi zaidi ya 7000.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua madaftari ya wanafunzi wa Darasa la pili katika shule ya Msingi ya Majimatitu A. Waziri Ndalichako alifika shuleni hapo kujionea mrundikano wa wanafunzi katika shule hiyo

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA KUSIMAMISHWA KAZI MAAFISA WATATU WA WIZARA YA ELIMU.



Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Joyce  Ndalichako  amemuagiza  Katibu  Mkuu wa Wizara hiyo  Dk. Leonard Akwilapo kumsimamisha kazi Afisa manunuzi  Audifasy Myonga na watumishi wengine wawil wa Chuo cha Ualimu Morogoro.

Waziri Ndalichako ametoa maagizo hayo mkoani Morogoro baada ya kutembelea chuo Cha Ualimu Morogoro  na kukuta idadi kubwa ya vifaa vya maabara visivyotumika huku muda wa matumizi ya vifaa hivyo  ukikaribia kuisha muda wake wa matumizi.

Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua baadhi ya vifaa vya maabara katika Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro ambapo amekuta vifaa na madawa ya maabara ambayo yamehifadhiwa bila kutumika tangu mwaka 2016.
Ndalichako amesema ununuzi wa vifaa hivyo unaonyesha kuwa na shaka kwani vifaa hivyo vilinunuliwa kwa awamu mbili ndani ya mwezi mmoja huku gharama ya manunuzi ikionyesha kupanda mara mbili hadi tatu kutoka gharama ya awali.

“Mkuu wa Chuo ameeleza vizuri kabisa kuwa vifaa hivyo vilinunuliwa bila wao kushirikishwa, sasa unajiuliza mnunuzi amewezeje kununua vifaa vya maabara bila kuwashirikisha watumiaji,” alihoji Waziri Ndalichako .
Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na watumishi wa Chuo cha Ualimu Morogoro kilichopo mkoani Morogoro. Waziri pia alisikiliza changamoy=to walizonazo watumishi hao. 

Pia, Waziri Ndalichako  ametembelea shule ya Sekondari ya Mzumbe kwa lengo la kukagua maendeleo ya ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo unaofanywa na wizara ambapo amewataka walimu na wanafunzi kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao ili wafaulu kwa viwango vya juu.



Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako na Naibu Katibu Mkuu Dk. Avemaria Semakafu wakikagua baadhi ya miundombinu iliyokarabatiwa katika shule ya Sekondari Mzumbe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.