Jumanne, 23 Oktoba 2018

UFAFANUZI WATOLEWA KUHUSU WANAFUNZI KUJIUNGA UDSM


ALIYOYAZUNGUMZA NAIBU MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM PROF. BONAVENTURE RUTINWA KATIKA KIPINDI CHA JAMBO TANZANIA LEO TBC.

1. Wale wote waliiomba Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) wakafutiwa udahili kwa sababu ya kuwa wengi zaidi (over capacity) wamerudishwa wote bila masharti yoyote.

2. Prof. Rutinwa ameeleza kuwa wale walioko Dar es Salaam waendelee kuchukua barua zao za udahili (admission letter) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wale walioko mbali na Dar es Salaam watazipokea barua zao kuanzia tarehe 27/10/2018 watakapofika kwa usaili. 

3. Wataalamu wa mifumo ya kompyuta wanaandaa utaratibu ili waliodahiliwa wapokee barua zao kwenye akaunti zao za udahili.

4. Wanafunzi ambao wamekosa code au wameshindwa kuingiza codes UDSM au vyuo vingine watapewa utaratibu wa kwenda chuo wanachokitaka.

5. Kutakua na dirisha la wale waliokosa nafasi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa sababu ya Program hizo kujaa wapate nafasi ya kuomba tena.

6.Serikali imeendelea kuboresha Miundombinu katika Chuo hicho ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya vyumba vya madarasa na maabara kwa hali ya juu na ya viwango kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi ambao chuo hicho inataka kuwadahili.


7. Serikali pia inaendelea kukiwezesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuongeza idadi ya Wahadhiri wabobevu ili kukidhi uhitaji.

8. Leo ilikuwa ni siku ya mwisho kufunga udahili lakini mara baada ya kufanya kikao na Mhe. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako alielekeza kuongezwa kwa siku hizo ili kutoa fursa zaidi kwa wanafunzi.


9. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinamshukuru sana Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako kwa kusaidia kutatua changamoto iliyokuwepo katika udahili kwa UDSM.

Jumatatu, 22 Oktoba 2018

WAZIRI NDALICHAKO AWATAKATA WAHASIBU WA WIZARA ANAYOINGOZA KUACHA “WIZI WA KISHAMBA”


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa kuna baadhi ya wahasibu wa Wizara hiyo na Taasisi zake ambao wamekuwa wakitumia vibaya nafasi zao kwa kughushi nyaraka mbalimbali wakati wa kufunga mahesabu kwa lengo la kujipatia fedha ambazo si halali yao.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya uandaaji wa hesabu za Fedha za Serikali kwa wahasibu wa Wizara hiyo na Taasisi zake.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Wahasibu wa Wizara hiyo na taasisi zake wakati akifungua mafunzo ya uandaaji wa hesabu za fedha za serikali jijini Dar es Salaam, ambapo Waziri amesisitiza suala la uadilifu, uzalendo na kuwataka wahasibu kuacha kushughushi nyaraka kwa lengo la kujipatia fedha ambazo siyo halali yao.

Waziri Ndalichako amesema Wahasibu wa Wizara lazima wawe mfano katika kuonesha nidhamu kwa kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo Wizara mama kwani kada zote zinafundishwa na walimu ambao msingi wao ni Wizara hiyo hiyo anayoiongoza.

Waziri Ndalichako ameeleza kuwa kuna dalili kuwa kuna baadhi ya wahasibu katika Wizara hiyo wanachezea fedha za Umma, hivyo amewaeleza Wahasibu hao  kuwa hivi sasa kuna ukaguzi unaendelea kwenye Wizara hiyo na matokeo ya ripoti hiyo yatakapokamilika umma utajulishwa.

“Kuna misemo kuwa eti mbuzi anakula kwa urefu wa kamba yake, sasa kamba inakatika, tuwe makini na kanuni za kazi, Fedha za serikali katika awamu hii ya Tano ni sumu, nyaraka nyingi ambazo zimekuwa zikitumika kwenye kufunga hesabu ni za kughushi, majina yamekuwa yakijirudia katika semina ambazo zimekuwa zikifanyika, saini tofauti jambo linaloashiria kuwa kuna wahasibu wanachezea fedha za serikali na huo ni wizi wa kishamba, amesisitiza Waziri Ndalichako.
Mhasibu Mkuu wa Wizara ya Elimu CPA (T) Rose Waniha akizungumza na wahasibu wakati wa mafunzo ya uandaaji wa fedha za serikali mkoani dar es salaam
                                                                                                                  
Waziri huyo ameeleza kuwa zipo pia baadhi ya Taasisi za Wizara hiyo zinapokusanya fedha za ada hawaziingizi kwenye mfuko wa serikali.

Hivyo ameielekeza Wizara hiyo na Taasisi zake zote kuhakikisha kuwa hadi itapofika Novemba moja mwaka huu ziwe zimejiunga na mfumo wa serikali wa malipo ya kielektroniki (GePG- Government e - payment Gateway Systeam) ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo CPA(T) Rose Waniha wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uandaaji wa hesabu za Fedha za Serikali, mafunzo hayo ya siku Tano yameanza leo na yatakamilika oktoba 26, 2018 

Kwa upande wake Mhasibu Mkuu wa Wizara hiyo CPA (T) Rose Waniha amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wahasibu kuwa na uelewa wa pamoja wa namna bora ya uandaaji wa hesabu za fedha za serikali.

Mafunzo hayo ya siku Tano yaliyoanza leo yatahitimishwa oktoba 26, 2018.
Baadhi ya wahasibu wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uandaaji wa hesabu za Fedha za serikali, mafunzo yanayofanyika jijini Dar es salam.


Ijumaa, 19 Oktoba 2018

UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
MINISTRY OF EDUCATION, SCIENCE AND TECHNOLOGY

COMMONWEALTH SCHOLARSHIPS TENABLE IN THE UNITED KINGDOM 2019

The Ministry of Education, Science and Technology as a Nominating Agent in the county for the Commonwealth Scholarships is inviting applications from qualified Tanzanians for Master’s and Doctoral degree tenable in the United Kingdom academic year for 2019.

The Scholarship includes:-
·        One year taught Master degrees.
·        Doctoral degree of up to three years duration.

Qualification

(i)               Applicants must be holders of Bachelor or Master’s degrees
(ii)             Applicants for Master’s degree must have a Bachelor degree with a GPA of not less than 3.5
(iii)          Applicants for PhD must have a Master’s degree with a GPA of not less than 4.0

Mode of Application

·        All applications should be made directly to the Commonwealth Secretariat and should be online using the following link http://cscuk.dfid.gov.uk/apply/applicants.

·        It is important that applicants should read and understand all instructions when filing the application forms, and all applicants must attach all the required attachments such as certified copies of academic certificates, transcript, birth certificates  and submit them online through the above link;

·        All applicants must ensure that, their referees submit reference letter on time;

·        Applicants who are employees must attach letters from their employers confirming that, if granted scholarships will be allowed to utilize these opportunities;
·        In order to be nominated all applicants must submit the filled application forms accompanied with the attached certified photocopies of academic certificates, transcript, birth certificates to the address below before 19th December, 2018

Permanent Secretary,
Ministry of Education, Science and Technology,
College of Business and Law,
University of Dodoma,
Block 10,
P.O. Box 10,
Dodoma.

Jumatano, 17 Oktoba 2018

BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE) LATAKIWA KUHUISHA MITAALA ILI IENDANE NA SOKO LA AJIRA


Serikali imelitaka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha Vyuo inavyovisimamia vinahuisha mitaala yake kila baada ya miaka mitatu kwa mujibu wa sheria ili kile kinachofundishwa kiweze kuendana na mahitaji halisi ya soko kwa sasa ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.

Kauli hiyo ya Serikali imetolewa  na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha jijini Dar Es Salaam alipofanya ziara katika Taasisi hiyo ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kutembelea Taasisi zilizo chini ya Wizara na kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akizungumza na watumishi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi NACTE (hawapo pichani) alipofanya ziara katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam kuona namna wanavyotekeleza majukumu yao.

Ole Nasha alisema ufundi ni taaluma ambayo inabadilika kila siku hivyo ni vyema mitaala ikahuishwa ili kozi zinazotolewa ziendana na ushindani wa soko la ajira. 

Pia Naibu Waziri Ole Nasha amelitaka Baraza hilo kuendelea kufanya ukaguzi wa vyuo vyake na kuvifutia usajili vyuo vyote ambavyo havifuati sheria, kanuni na taratibu ikiwa ni pamoja na kuvichukulia hatua vinavyoendelea kufanya makosa kwa mujibu wa sheria.

“Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) tangu mwaka 2016 imefungia vyuo 74 ambavyo havifuati taratibu wakati mwaka huu vyuo 3 vimefungiwa huku vingine 21 vikizuiliwa kutoa baadhi ya kozi hii ni kutokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano iliyo nayo ya kuhakikisha Elimu itolewayo ni bora na sio bora Elimu” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.
Watumishi wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha alipofanya ziara katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es salaam

Katika hatua nyingine ameipongeza NACTE kwa kusimamia vizuri udahili wa wanafunzi kwa mwaka huu ikiwa ni pamoja na kutengeneza mifumo 14 ya TEHAMA ambayo imesaidia zoezi la udahili kufanyika kwa ufanisi hatua iliyopelekea kuongeza idadi ya wanafunzi elfu kumi zaidi kutoka ile ya mwaka jana ambayo walidahili wanafunzi 110,000.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ambayo imejipambanua katika kufikia uchumi wa kati na wa Viwanda ambao ili uweze kufanikiwa uanahitaji mafundi waliosoma vizuri, hivyo elimu ya ufundi ni moja ya vipaumbele vya Serikali na kuzitaka Mamlaka hizo kusimamia elimu itolewayo ili tolewe kama inavyostahili.

Naibu Waziri amehitimisha ziara yake ya siku moja jijini Dar es Salaam kwa kutembelea Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi stadi VETA ambapo amewataka kuandaa vijana ambao ni mahiri na wabobezi katika fani mbalimbali watakaofanya kazi katika viwanda ili kujenga uchumi wa viwanda.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akiwa katika picha ya pamoja na viongozi pamoja na watumishi wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA Makao makuu jijini Dar es Salaam.

Jumapili, 14 Oktoba 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA AWATAKA WAHITIMU FEZA KUEPUKA VITENDO VIOVU


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi Feza kuepuka vitendo viovu ambavyo vinaweza kukatisha ndoto zao katika maisha.

Ole Nasha ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 15 ya darasa la saba ya shule hiyo na kuwataka vijana hao kutambua kuwa kuhitimu katika hatua hiyo ndio mwanzo wa safari ndefu waliyonayo katika Elimu na kuwa nidhamu pekee ndio msingi wa mafanikio.

“Jamii yetu kwa sasa inakabiliwa na mmomonyoko wa maadili vitendo viovu kama vile vijana kujishirikisha katika masuala ya ngono, ulevi, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii jihadharini navyo sana katika maisha yenu, mkijiingiza tu mtaharibu ndoto zenu mlizojiwekea na matokeo yake mtashindwa kushiriki katika jitihada za kuijenga nchi yenu,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha


Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akihutubia wakati wa mahafali ya kumaliza Elimu ya Msingi Feza yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam. Amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, bidii na kutanguliza uzalendo katika yale watakayokuwa wakifanya ili kuweza kufikia malengo yao.

Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Sekta binasfi katika maendeleo ya Elimu nchini kwa kuwaandaa vijana kimaadili na kitaaluma ili kufikia dira ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayolenga kuwa na mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitizamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

“Mtaona Serikali sasa imefuta tozo na kodi ambazo zilikuwa ni kero kwa wamiliki wa Shule binafsi kama vile Tozo ya Uendelezaji Ujuzi (Skills Development Levy-SDL), Tozo ya Zimamoto, Kodi ya Mabango na Tozo ya Usalama Mahali pa Kazi (Occupational Safety and Health Administration-OSHA) hii yote ni kuthamini mchango mkubwa ambao mmekuwa mkiutoa katika kuelimisha vijana wa Taifa hili,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.


Wahitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Feza wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha wakati wa mahafali yao yaliyofanyika oktoba 13, 2018 jijini Dar es salaam.

Hata hivyo amewataka wamiliki wote wa shule nchini kutambua kuwa pamoja na shule kuwa zao wanatakiwa kufuata taratibu, sheria na kanuni katika uendeshaji wa shule hizo kwa ni bado elimu itolewayo ni mali ya umma na watoto ni wa kitanzania.

Naye Mkurugenzi wa Shule za Feza Ibrahimu Yunus anasema kwa sasa shule hiyo ya Msingi ina jumla ya wanafunzi 770 ambapo wanaohitimu darasa la saba mwaka huu ni jumla ya wanafunzi 75 huku shule hiyo ikijivunia kufanya vizuri kwenye masuala ya Elimu katika ngazi zote zinazotolewa shuleni hapo.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akigawa cheti kwa mmoja wa wanafunzi aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika shule ya Msingi Feza wakati wa mahafali yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 13, 2018


MILIONI 40 ZIMECHANGWA ILI KUJENGA MABWENI YA WASICHANA


WAZIRI NDALICHAKO AENDELEA KUSISITIZA KUWA ELIMU MSINGI NI MIAKA 7
Zaidi ya kiasi cha shilingi Milioni 40 zimechangwa na wadau wa Elimu na wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Pangani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana wa kidato cha tano na sita katika shule Sekondari Mwera mkoani Tanga.

Fedha hizo zimekusanywa mara baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kuongoza harambee hiyo wakati wa kongamano la wadau wa Elimu lililoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mbunge wa Pangani na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso kiasi cha Tsh. Milioni 3 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana  katika Shule ya Sekondari Mwera iiyopo Wilayni Pangani mkoani Tanga

Kupitia kongamano hilo la Elimu Waziri Ndalichako ameendelea kuwasisitiza wananchi kuwa muda wa elimu ya Msingi ni miaka 7 na kuwa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho, hivyo hata kama wanafunzi wanaosoma mtaala mpya hivi sasa watasoma kwa miaka saba na kuwa suala hilo ni la kisheria.

“Pamoja na kuwepo mtaala mpya bado elimu msingi ni miaka 7 na kuwa suala hilo lipo kisheria hivyo kama kutakuwa  na mabadiliko yoyote Serikali itashirikisha  wadau katika kutoa maoni na mwisho wa siku wadau watapata taarifa kamili, hata hivyo  serikali mkakati wake hivi  sasa ni wa kuhakikisha ina boresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia,”alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amezitaka kamati za shule kuhakikisha zinasimamia taaluma pamoja na kuhoji kuhusu matokeo ya elimu ambayo hayaridhishi lakini pia ushirikiano wa pamoja lazima uwepo ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kwenye taaluma Wilayani humo.

“ Mtumieni Mheshimiwa mbunge Juma Aweso awe ni mfano wenu wa kuiga, amekuwa akijitolea mfano kuwa mama yake alikuwa mama ntilie, lakini amezingatia sana elimu na hiyo ndiyo imemkomboa ndiyo maana leo hii ameweza  kuwa mbunge wa jimbo la Pangani na pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, yote hii ni kwa sababu amesoma, amesisitiza Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa Harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana kwenye shule y sekondari Mwera, ambapo zaidi ya Milioni 40 zilikusanywa katika harambee hiyo Wilayani Pangani mkoani Tanga.

Akizungumza na wananchi katika kongamano hilo la Elimu Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah alisema kuwa familia  nyingi Wilayani humo zina maisha magumu hivyo ni vyema Wilaya hiyo ikawa na  michepuo ya kidato cha tano na sita ili wanafunzi wanaoofaulu wabaki hapo hapo kuendelea na masomo badala ya wazazi kuanza kuingia gharama za kuwapeleka kwenye shule za mbali.

“Mheshimiwa Waziri Wilaya yetu ina shule moja tu yenye kidato cha tano na sita, sasa tumejiwekea malengo angalau tuwe na shule 3 tofauti ili wanafunzi waendelee kusoma hapa hapa pia tunahitaji Chuo cha Ufundi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wetu waweze kujiajiri,” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Majina Umwagiliaji Juma Aweso amesema Wilaya hiyo ilichelewa sana kuwekeza kwenye Elimu na hivyo amewataka wanapangani kubadilika na kuwa elimu pekee ndiyo Mkombozi wao.

“Kupitia Elimu, mtoto wa mama ntilie anaweza kuwa Mkemia, Profesa, Mhandisi, Daktari bingwa, kiongozi, hivyo elimu pekee ndiyo silaha ya kuifanya Jamii yoyote iweze kuwa na Maendeleo,”alisema Aweso.
Viongozi wa Wilaya ya Pangani akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Zainab Abdallah, Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso wakiwa na Waziri Ndalichako wakati wa kukagu Miundombinu ya vyumba vya madarsa katika shule ya sekondari Mwera iliyopo Wilayani humo.


Ijumaa, 12 Oktoba 2018

PROF. MDOE: MAAFISA MIKOPO MSIWE CHANZO CHA MIGOGORO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU


Maafisa wanaosimamia madawati ya mikopo vyuoni wametakiwa kutokuwa chanzo cha migogoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora isiyokuwa na urasimu, kuacha umangimeza, rushwa na badala yake wahakikishe wanaimarisha madawati yao ili kuhakikisha wanafunzi wenye sifa na uhitaji   wananufaika na mikopo kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati akizungumza katika kikao kazi cha siku mbili cha maafisa hao kilichoanza leo mjini Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuhakikisha watanzania wengi wanapata Elimu ya juu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe aliyekaa katikati akizungumza na maafisa wanaosimamia madawati ya mikopo kwenye Taasisi za Elimu nchini, (hawapo pichani),wakati wa kikao Kazi kinachofanyika Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

Profesa Mdoe amesema kwa mwaka wa fedha 2018/19 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 427. 5 ambapo jumla ya wanafunzi 124 watanufaika na mkopo huo, na kuwa ugawaji wa mikopo hiyo uzingatie haki, vigezo, kanuni na sheria.

“Nataka twende vizuri tukahakikishe huduma bora inatolewa katika mwaka huu mpya wa masomo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora, kusimamia kumbukumbuku na kuhakikisha mawasiliano ya mara kwa mara yanakuwepo kati ya maafisa mikopo na bodi ya mikopo na kwamba haipendezi maafisa mikopo kuwa chanzo cha migogoro,” amesisitiza Profesa Mdoe.

Profesa Mdoe pia ameitaka bodi hiyo kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kuwasaka waajiri  warejeshe fedha ambazo wafanyakazi wao walisoma kwa mkopo, ili fedha hizo zitumike kwa wanafunzi wengine.
Maafisa mikopo wanaosimamia madawati ya mikopo katika Taasisi za Elimu ya juu hapa nchi wakiwa katika kikao kazi mjini Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kujitathmini na  kujengeana uwezo wa namna  bora ya kuboresha utendaji Kazi zao.

Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya mikopo Abdul- Razq badru amesema kuwa maagizo yote yaliyolewa na Naibu Katibu Mkuu watayasimamia katika utekelezaji wa ugawaji wa mikopo kwa wnanafunzi huku akikiri kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo inayotolewa na serikali.

“Bodi ya mikopo inaahidi kusimamia haki, vigezo, kanuni na sheria katika utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi kama ambavyo sheria zinavyoelekeza, niwasihi sana maafisa mikopo kufanya kazi kwa weledi na kuacha mazoea ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza,” alisisitiza Badru
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu Abdul-razaq Badru akizungumza na maafisa mikopo wakati wa kikao kazi cha siku mbili kinachofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.