Ijumaa, 12 Oktoba 2018

PROF. MDOE: MAAFISA MIKOPO MSIWE CHANZO CHA MIGOGORO KWA WANAFUNZI ELIMU YA JUU


Maafisa wanaosimamia madawati ya mikopo vyuoni wametakiwa kutokuwa chanzo cha migogoro ili kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma bora isiyokuwa na urasimu, kuacha umangimeza, rushwa na badala yake wahakikishe wanaimarisha madawati yao ili kuhakikisha wanafunzi wenye sifa na uhitaji   wananufaika na mikopo kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa James Mdoe wakati akizungumza katika kikao kazi cha siku mbili cha maafisa hao kilichoanza leo mjini Bagamoyo mkoani Pwani na kusisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya awamu ya Tano ni kuhakikisha watanzania wengi wanapata Elimu ya juu.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe aliyekaa katikati akizungumza na maafisa wanaosimamia madawati ya mikopo kwenye Taasisi za Elimu nchini, (hawapo pichani),wakati wa kikao Kazi kinachofanyika Wilayani Bagamoyo mkoani Pwani

Profesa Mdoe amesema kwa mwaka wa fedha 2018/19 serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 427. 5 ambapo jumla ya wanafunzi 124 watanufaika na mkopo huo, na kuwa ugawaji wa mikopo hiyo uzingatie haki, vigezo, kanuni na sheria.

“Nataka twende vizuri tukahakikishe huduma bora inatolewa katika mwaka huu mpya wa masomo ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora, kusimamia kumbukumbuku na kuhakikisha mawasiliano ya mara kwa mara yanakuwepo kati ya maafisa mikopo na bodi ya mikopo na kwamba haipendezi maafisa mikopo kuwa chanzo cha migogoro,” amesisitiza Profesa Mdoe.

Profesa Mdoe pia ameitaka bodi hiyo kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili kuboresha utendaji kazi, ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kuwasaka waajiri  warejeshe fedha ambazo wafanyakazi wao walisoma kwa mkopo, ili fedha hizo zitumike kwa wanafunzi wengine.
Maafisa mikopo wanaosimamia madawati ya mikopo katika Taasisi za Elimu ya juu hapa nchi wakiwa katika kikao kazi mjini Bagamoyo mkoani Pwani kwa lengo la kujitathmini na  kujengeana uwezo wa namna  bora ya kuboresha utendaji Kazi zao.

Akizungumza katika kikao kazi hicho Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya mikopo Abdul- Razq badru amesema kuwa maagizo yote yaliyolewa na Naibu Katibu Mkuu watayasimamia katika utekelezaji wa ugawaji wa mikopo kwa wnanafunzi huku akikiri kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo inayotolewa na serikali.

“Bodi ya mikopo inaahidi kusimamia haki, vigezo, kanuni na sheria katika utoaji wa mikopo hiyo kwa wanafunzi kama ambavyo sheria zinavyoelekeza, niwasihi sana maafisa mikopo kufanya kazi kwa weledi na kuacha mazoea ili kuondoa migogoro inayoweza kujitokeza,” alisisitiza Badru
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya juu Abdul-razaq Badru akizungumza na maafisa mikopo wakati wa kikao kazi cha siku mbili kinachofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni