Jumapili, 14 Oktoba 2018

MILIONI 40 ZIMECHANGWA ILI KUJENGA MABWENI YA WASICHANA


WAZIRI NDALICHAKO AENDELEA KUSISITIZA KUWA ELIMU MSINGI NI MIAKA 7
Zaidi ya kiasi cha shilingi Milioni 40 zimechangwa na wadau wa Elimu na wananchi mbalimbali wa Wilaya ya Pangani kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana wa kidato cha tano na sita katika shule Sekondari Mwera mkoani Tanga.

Fedha hizo zimekusanywa mara baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kuongoza harambee hiyo wakati wa kongamano la wadau wa Elimu lililoandaliwa na mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Mbunge wa Pangani na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso kiasi cha Tsh. Milioni 3 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa mabweni ya wasichana  katika Shule ya Sekondari Mwera iiyopo Wilayni Pangani mkoani Tanga

Kupitia kongamano hilo la Elimu Waziri Ndalichako ameendelea kuwasisitiza wananchi kuwa muda wa elimu ya Msingi ni miaka 7 na kuwa sheria hiyo haijafanyiwa marekebisho, hivyo hata kama wanafunzi wanaosoma mtaala mpya hivi sasa watasoma kwa miaka saba na kuwa suala hilo ni la kisheria.

“Pamoja na kuwepo mtaala mpya bado elimu msingi ni miaka 7 na kuwa suala hilo lipo kisheria hivyo kama kutakuwa  na mabadiliko yoyote Serikali itashirikisha  wadau katika kutoa maoni na mwisho wa siku wadau watapata taarifa kamili, hata hivyo  serikali mkakati wake hivi  sasa ni wa kuhakikisha ina boresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia,”alisisitiza Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako pia amezitaka kamati za shule kuhakikisha zinasimamia taaluma pamoja na kuhoji kuhusu matokeo ya elimu ambayo hayaridhishi lakini pia ushirikiano wa pamoja lazima uwepo ili kuhakikisha wanafunzi wanafanya vizuri kwenye taaluma Wilayani humo.

“ Mtumieni Mheshimiwa mbunge Juma Aweso awe ni mfano wenu wa kuiga, amekuwa akijitolea mfano kuwa mama yake alikuwa mama ntilie, lakini amezingatia sana elimu na hiyo ndiyo imemkomboa ndiyo maana leo hii ameweza  kuwa mbunge wa jimbo la Pangani na pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, yote hii ni kwa sababu amesoma, amesisitiza Ndalichako.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa Harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wasichana kwenye shule y sekondari Mwera, ambapo zaidi ya Milioni 40 zilikusanywa katika harambee hiyo Wilayani Pangani mkoani Tanga.

Akizungumza na wananchi katika kongamano hilo la Elimu Mkuu wa Wilaya ya Pangani Zainab Abdallah alisema kuwa familia  nyingi Wilayani humo zina maisha magumu hivyo ni vyema Wilaya hiyo ikawa na  michepuo ya kidato cha tano na sita ili wanafunzi wanaoofaulu wabaki hapo hapo kuendelea na masomo badala ya wazazi kuanza kuingia gharama za kuwapeleka kwenye shule za mbali.

“Mheshimiwa Waziri Wilaya yetu ina shule moja tu yenye kidato cha tano na sita, sasa tumejiwekea malengo angalau tuwe na shule 3 tofauti ili wanafunzi waendelee kusoma hapa hapa pia tunahitaji Chuo cha Ufundi kwa lengo la kuwajengea uwezo wanafunzi wetu waweze kujiajiri,” alisisitiza Mkuu huyo wa Wilaya.

Naye Mbunge wa Jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Majina Umwagiliaji Juma Aweso amesema Wilaya hiyo ilichelewa sana kuwekeza kwenye Elimu na hivyo amewataka wanapangani kubadilika na kuwa elimu pekee ndiyo Mkombozi wao.

“Kupitia Elimu, mtoto wa mama ntilie anaweza kuwa Mkemia, Profesa, Mhandisi, Daktari bingwa, kiongozi, hivyo elimu pekee ndiyo silaha ya kuifanya Jamii yoyote iweze kuwa na Maendeleo,”alisema Aweso.
Viongozi wa Wilaya ya Pangani akiwemo Mkuu wa Wilaya hiyo Zainab Abdallah, Mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Juma Aweso wakiwa na Waziri Ndalichako wakati wa kukagu Miundombinu ya vyumba vya madarsa katika shule ya sekondari Mwera iliyopo Wilayani humo.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni