Jumatatu, 14 Septemba 2020

KATIBU MKUU DKT AKWILAPO AAGIZA KUFANYIKA TATHMINI YA MAZINGIRA NA MIUNDO MBINU YA SHULE ZOTE

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt Leonard Akwilapo amewataka Wathibiti Ubora wa shule nchini kufanya tathmini ya mazingira na miundombinu ya shule katika kudhibiti majanga ya moto yaliyokithiri katika siku za hivi karibuni.

 Dkt Akwilapo amesema hayo kufuatia tukio la moto lililosababisha vifo vya wanafunzi 10 na kujeruhi wengine lililotokea katika shule ya Msingi Byamungu Islamic iliyoko Kyerwa Mkoani Kagera.

Akwilapo amewataka Wathibiti ubora wa shule kushirikiana na wataalamu kubaini vyanzo vya moto katika shule  na amesema sheria zipo na pindi shule itakapogundulika kukiuka taratibu wasisite kuzichukulia hatua.

 “Asubuhi ya leo tumepokea taarifa ya kuungua kwa shule ya msingi ya Byamungu  na watoto wamepoteza maisha, lakini matukio haya yamekuwa yanaongezeka hivyo kama Wizara tunawajibu kuhakikisha hili linapatiwa suluhisho kwa kutumia wataalamu,"aliongeza Dkt. AKwilapo

Aidha Dkt.Akwilapo amesema Wathibiti Ubora wa shule zaidi ya 400 wameajiriwa mmepewa ofisi na vitendea kazi, nataka kuona mabadiliko ya namna tunavyosimamia shule”alisisitiza Dkt. Akwilapo.

Katibu Mkuu Akwilapo ametumia fursa hiyo kutoa pole kwa wazazi, walezi na Shule ya Msingi Byamungu iliyopo mkoani Kagera kwa kuondokewa na wanafunzi na kuwatakia uponyaji wa haraka majeruhi 6 ambao wanaendelea na matibabu.

Jumatano, 2 Septemba 2020

DR. LEONARD AKWILAPO ATAKA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KUANZISHA PROGRAMU ZA VIPAUMBELE VYA TAIFA

 Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo ametoa wito kwa Vyuo Vikuu nchini kuhakikisha vinaanzisha programu za masomo zinazoendana na vipaumbele vya kitaifa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akifungua  maonesho  ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam

Dkt. Akwilapo ametoa wito huo Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia ambapo amesema kwa kuanzisha programu hizo nchi itaongeza ujuzi wa wataalamu na pato la taifa. 

Kiongozi huyo ametaja baadhi ya programu za kipaumbele kuwa ni mafuta na gesi, afya, hususani udaktari bingwa kwa ngazi za Uzamivu katika nyanja zote za magonjwa ya upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu, upandikizaji figo, ini na uboho (bone marrow), tiba za ndani za moyo, na uhudumiaji wa wagonjwa wa dharura na mahututi (emergency medicine and critical care).


 “Tusingependa kama nchi kupeleka wagonjwa wetu nchi za nje kutibiwa, bali nchi za nje waje kutafuta tiba kwetu (medical tourism). Kwa kufanya hivyo tutaongeza ujuzi wa wataalamu wetu pamoja na pato la taifa,” amesisitiza Dkt. Akwilapo. 

Katibu Mkuu Akwilapo ameongeza kuwa pamoja na kuanzisha programu za vipaumbele, nchi kwa sasa inatekeleza miradi mingi mikubwa ambayo inahitaji wasomi wa kuendesha na kusimamia miradi hiyo, hivyo ni jukumu la Taasisi za Elimu ya Juu kuhakikisha hili linafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu kwa kuhakikisha wanatoa elimu bora na kwamba Serikali itaendelea kusomesha kwa wingi wataalamu katika fani na ujuzi adimu na maalum kwa mahitaji ya nchi. 

Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo akiwa katika picha ya pamoja na wakuu wa vyuo mbalimbali vya elimu ya Juu nchini mara baada ya kufungua maonesho  ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika katika viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam

“Ni jambo la kutia moyo kuona kwamba hivi sasa baadhi ya vyuo vikuu vimeanza kuelekeza jitihada zao katika kutoa elimu ambayo inalenga kushughulikia changamoto za jamii na kuweka msisitizo katika maeneo ya kimkakati ya nchi kama vile Kilimo, Madini, Utalii, Uvuvi, Maliasili na Misitu na Afya,” amesema Dkt. Akwilapo.  

Katika hatua nyingine Dkt. Akwilapo ameendelea kuzitaka Taasisi za Elimu ya Juu kuona namna bora ya kupanua udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kutokana na ongezeko la udahili wa wanafunzi katika ngazi ya msingi na sekondari na kwamba wanapohitimu lazima wapate nafasi katika vyuo vya kati na vya juu ili kuweza kuwapa ujuzi wa kujiajiri na hivyo kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa Taifa. 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Mayunga Nkunya  amesema Tume pamoja na mambo mengine imefanikiwa kuimarisha mfumo wa utoaji ithibati ya mtaala, jambo ambalo lilionekana kuwa tatizo kwa muda mrefu na kwamba itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania katika sekta ya elimu ili kuhakikisha Watanzania wa ngazi zote wanapata elimu bora yenye kukidhi viwango vya ubora Kitaifa, Kikanda na Kimataifa.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini, Profesa Charles Kihampa amesema lengo la maonesho hayo ni kutoa fursa kwa vyuo vikuu kujitangaza na kuonesha huduma na kazi wanazofanya pamoja na mchango wao katika ustawi wa elimu ya juu kwa mustakabali wa maendeleo ya sayansi, teknolojia na manuufaa yake kiuchumi na kijamii. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi waliotembelea maonesho hayo wamesema wamefurahishwa na kuwepo kwa maonesho hayo kwani yanatoa fursa ya kuonana na wahusika na kupata taarifa zinazowawezesha kuomba programu zinazoendana na ufaulu wao.

Jumla ya taasisi 67 za elimu ya juu zimeshiriki katika maonesho hayo.

Brass Band ikitumbuiza wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 15 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayofanyika Jijini Dar es Salaam

Jumanne, 1 Septemba 2020

WALIMU 100 NCHINI KUFUNDISHWA MBINU ZA KUFUNDISHIA LUGHA YA KIFARANSA

Serikali za Tanzania na Ufaransa zimeingia makubaliano ya kutoa mafunzo ya mbinu za kufundishia lugha ya Kifaransa kwa walimu 100 nchini ambao watakuwa na uwezo wa kufundisha wanafunzi 5,000 wa Kitanzania katika ngazi ya sekondari.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kati ya Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Frederic Clavier na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo kilichofanyika Jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya Dola za Kimarekani 250,000 zitatumika ili kufanikisha mpango huo.
Katika kikao hicho wamekubaliana kufanyika kwa vikao vya kitaalamu kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Kituo cha Ubalozi wa Ufaransa (Alliance Francais) ili kupanga utekelezaji wa mafunzo hayo ya walimu.

Aidha, Balozi Clavier ameonesha kuwepo kwa fursa za Watanzania kusoma programu zisizopungua 2,000 za Kiingereza nchini Ufaransa. Ameeleza kuwa  Ufaransa inaandaa Maonesho ya Elimu ya Juu (Higher Education Fair) yatakayofanyika nchini Mei 2021 ambapo vyuo 20 vya Ufaransa vitashiriki kutafuta ushirikiano na Vyuo Vikuu vya Tanzania na Sekta binafsi. 
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Akwilapo ameushukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kuendeleza ushirikiano katika kukuza na kuimarisha elimu ya Juu nchini kupitia ufadhili wa mafunzo hayo na kuagiza wahusika katika Wizara anayoisimamia kuhakikisha vikao vya kitaaluma vinafanyika ili mafunzo hayo yaweze kuanza kwa wakati uliopangwa.

Katibu Mkuu Akwilapo pia ameahidi kuweka wazi kwa Watanzania kuhusu kuwepo kwa fursa hiyo ya kusoma programu za Kiingereza nchini Ufaransa ili Watanzania waweze kuchangamkia fursa hiyo.

SEMAKAFU: VYUO VYA FDC TOENI MAFUNZO YENYE UHITAJI NA AJIRA

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kujikita katika kutoa mafunzo ya fani zinazopendwa na zinazotoa ajira badala ya kuendelea kuwa na fani ambazo hazina wanafunzi katika eneo husika.


Dkt. Semakafu ametoa agizo hilo alipofanya ziara ya kukagua ukarabati na uendeshaji wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same kilichopo Mkoani Kilimanjaro ambapo amesema ni vizuri vyuo  vikajiimarisha kwenye utoaji mafunzo kwa fani zenye wanafunzi  wengi na kuachana na zile zenye wanafunzi wachache.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akizungumza na baadhi ya watumishi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu chuoni hapo.

“Kuanzia mwaka huu, kila chuo cha wananchi kitafundisha fani ambazo zinahitajika katika maeneo husika kwa maana ya kuwa na wanafunzi wa kutosha, hakuna chuo chochote kusajili fani ambazo zina wanafunzi wachache ama chini ya kumi na mbili, Serikali haiajiri walimu kufundisha wanafunzi wawili hivyo hakuna haja ya kuweka fani ambazo hazina wanafunzi wa kutosha,” amesisitiza Dkt. Semakafu.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amesema mpango wa 'Elimu haina mwisho' unaotolewa katika vyuo hivyo ni utaratibu wa kutoa fursa kwa watoto waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kiuchumi na kijamii ili kuwasaidia kupata elimu na ujuzi wa kuwawezesha kuendelea na masomo na kuendesha maisha yao pindi watakapohitimu hivyo wanapaswa kufundishwa kama wanafunzi wengine bila kuwatenga.  
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu akitoa maelekezo ya namna ya kuboresha eneo la utoaji wa mafunzo ya umeme wa magari kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi, Edward Mdee.

Amesema Serikali iliamua watoto hao wasome katika vyuo hivyo kupitia mfumo usio rasmi bila malipo yoyote kwa lengo la kuhakikisha wanapata fursa nyingine ya kuendelea na masomo na kuutaka Uongozi wa chuo cha Maendeleo Same  kuwarudisha chuoni wanafunzi wote walioacha masomo kwa sababu mbalimbali ili waweze kumaliza masomo yao.

“Tumeanza programu hii kwa lengo la kupata watoto wote walioacha shule na ndio maana unaona hata wasichana walioacha shule kutokana na changamoto mbalimbali tumewarudisha katika mfumo huu ili waje waendelee na masomo na na wale wenye watoto hata tuna shule za chekechea kwa ajili ya watoto wao,” amesema Dkt. Semakafu.

Naibu Katibu Mkuu Dkt. Semakafu amekagua miundombinu iliyokarabatiwa na kuboreshwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambapo ameuagiza uongozi wa chuo hicho kufanya marekebisho katika baadhi ya miundombinu ambayo haikukarabatiwa vizuri.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Same, Edward Mdee akitoa taarifa  ya chuo hicho kwa Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Ave Maria Semakafu alipofika chuoni hapo kukagua maendeleo ya chuo hicho.
Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same, Edward Mdee  ameishukuru Wizara kwa ukarabati ambao umefanyika chuoni hapo, na kusema kuwa chuo hicho chenye wanafunzi 301 kipo katika mkakati wa kuboresha utoaji wa mafunzo ili kuhakikisha kinatoa vijana wenye ujuzi na maarifa yatakayowawezesha vijana wa Same kujiajiri ama kuajiriwa.
Muonekano wa baadhi ya majengo ya miundombinu ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Same yaliyojengwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.