Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako amemuagiza Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Dkt. Leonard Akwilapo kuwaondoa mara moja Kaimu Mkurugenzi
wa Ualimu Basiliana Mrimi na Mratibu wa Miradi wa idara hiyo Fredrick
Shuma katika nafasi zao kwa kushindwa kusimamia majukumu yao kwa weledi.
Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo Wilayani Nzega mkoani Tabora alipokuwa akikagua maendeleo ya upanuzi wa Chuo cha Ualimu cha Ndala ambapo amesema viongozi hao wameshindwa kuzisimamia kampuni za ujenzi za Sky Ward na United Builders zilizopewa kazi ya kufanya upanuzi katika chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wanafunzi na watumishi wa chuo cha ualimu Ndala mara baada ya kukagua upanuzi wa Chuo hicho.
Waziri Ndalichako amesema kampuni ya Sky Ward ilipewa kiasi cha shilingi milioni 600 za awali kwa ajili ya kujenga majengo katika Chuo hicho toka mwezi wa saba lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika na wala hakuna taarifa yeyote inayoelezea kwa nini kazi hiyo imekwama.
Waziri Ndalichako amesema serikali haitaongeza muda uliowekwa katika Mkataba ambapo ameagiza kampuni hizo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kazi hizo zinakamilika kwa wakati.
“Sitaki kusikia maneno ninachotaka ni kuona kazi inayofanyika hapa ilingane na thamani ya fedha ambazo tumeshawalipa na baada ya siku 30 nitakuja kukagua kama kweli kazi imeanza,”alisisitiza Waziri Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akikagua moja ya nyumba iliyojengwa katika Chuo cha Ualimu Ndala ambapoo hajaridhishwa na kasi ya Wakandarasi wa ujenzi huo na ameagiza mradi huo ukamilike katika muda uliopangwa.
Waziri huyo alisema Serikali haitasita kuvunja mkataba na Mkandarasi
yeyote atakaeonekana hana uwezo wa kutekeleza mradi kwa mujibu wa mkataba.
Katika hatua nyingine Waziri Ndalichako alimtaka Mhandisi Mshauri kuhakikisha anawasimamia wakandarasi hao ili waweze kutimiza wajibu wao na kuhakikisha kazi hizo inafanyika kwa viwango na kwa wakati, endapo atashindwa kuwasimia wakandarasi hao Serikali italazimika kumfukuza kazi.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako akipokelewa na wakufunzi
na watumishi wa Chuo cha Ualimu Ndala mara baada ya kuwasili chuoni hapo kwa ajili
ya ziara ya kikazi